Msomaji Bora Sana Wa Makala Na Blogu Yako Ni Huyu.

Kosa kubwa ambalo waandishi wengi wapya wamekuwa wanalifanya ni kutaka kuandika kitu ambacho kitasomwa na kila mtu. Yaani unataka uandike na kila mtu awe msomaji wako. Kwa njia hii siyo tu utashindwa kumpata kila mtu, ila pia hutapata msomaji hata mmoja.

Unapoandika makala ambayo unataka kumlenga kila mtu, unaishia kuwa na makala ambayo haimlengi mtu yeyote. Hivyo unakuwa umepoteza muda wako na rasilimali zako kufanya kitu ambacho hakuna uzalishaji.

Njia bora kabisa unayoweza kuitumia kwenye uandishi, ni kuanza na msomaji mmoja. Unahitaji kuwa na msomaji mmoja wa mfano, ambaye utakuwa unamwandikia yeye. Hapa unakuwa na mtu ambaye unajua ana uhitaji fulani, au ana changamoto fulani anazotaka kutatua, sasa unamwandikia mtu huyo.

Kwa kufanya hivi, makala yako itakuwa na msaada wa moja kwa moja kwa yule mwenye ile shida au changamoto uliyoandikia kwenye makala yako. Uzuri ni kwamba watakuwepo watu wanaohangaika na lile ambalo umeliandika. Watu hawa wataona makala ile ni yao moja kwa moja na wataweza kuondoka na hatua za kuchukua.

Unaweza kuwa na watu wengi uwezavyo, kulingana na maeneo ambayo unaandikia, lakini kwa kuanza usiwe na watu wengi sana wa mfano. Unaweza kuchagua kuwa na watu watatu wa mfano ambao unawaandikia kila siku.

Katika kutengeneza watu wa mfano, zipo njia mbili;

Njia ya kwanza ni kuamua kumtengeneza mtu mwenyewe kulingana na namna unavyoona watu wanasumbuka na kile ambacho umechagua kufanya. Hapa wewe mwenyewe unachagua kuandika makala za kutatua changamoto fulani, au kutoa maarifa fulani.

Njia ya pili ni kwa kufanya utafiti wa wasomaji wako ambao tayari unao. Hapa unaandaa fomu fupi ya wasomaji wako kujaza. Katika fomu hii utataka wajaze umri wao, wanakopatikana, shughuli zao, changamoto zao, kipato chao na sifa nyingine zitakazokuwezesha wewe kuwaandalia makala zitakazowasaidia vizuri.

Kwa vyovyote vile, ni muhimu unapoandika makala yoyote, ndani ya akili yako kuwe kuna mtu ambaye unamlenga moja kwa moja. Iwe ni kwa kumtengeneza, au kwa utafiti uliofanya.

Kama hujapata mtu wa kuweza kumwandikia moja kwa moja, basi jiandikie wewe moja kwa moja. Jiangalie wewe mwenyewe unasumbuka na nini, ni changamoto zipi unataka kutatua, ni vitu gani unahitaji kujifunza. Jiandikie makala itakayokusaidia wewe, na watakuwepo watu wengine wanaosumbuka kama wewe na makala yako itawasaidia sana.

Waandishi wengi wanaogopa kutumia mbinu hii ya kuandaa makala inayowalenga watu wachache, kwa kuhofia watapata wasomaji wachache. Lakini ukweli ni kwamba, unachotaka wewe siyo wasomaji wengi, bali wasomaji ambao watajali kile unachoandika, ambao watasubiri kwa hamu kusikia kutoka kwako, ambao watachukua zile hatua ambazo umewashauri kuchukua.

Kama wasomaji hawa watakuwa kumi, upo pazuri, kama watakuwa 100 unafanya kazi kubwa sana, na kama watakuwa 1000, umeshaijua siri ya mafanikio kupitia uandishi.

Chagua mtu au watu wachache wa mfano, ambao utawaandikia moja kwa moja kwenye kila makala unayoandika. Usipoteze muda wako kuandika makala ambayo unafikiri kila mtu ataipenda, utakosa kila mtu.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK.

Makirita Amani,

Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Karibu sana kwenye MTAALAMU NETWORK uweze kutengeneza kipato kupitia mtandao wa intaneti.

Kujua huduma za blog tunazotoa BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kusoma makala zetu za mbinu na maarifa ya kutengeneza kipato kupitia mtandao wa intaneti BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Leave a Reply