Watu wakikutafuta kwenye mtandao wanaona nini?

Zama zimebadilika, zamani ilikuwa ukiomba kazi mahali, unaandika wasifu wako na watu wanatumia wasifu huo kujua wewe ni mtu wa aina gani. Ndiyo maana kwenye wasifu watu walikuwa wanakazana kuandika vitu vizuri na vya kuvutia. Mfano kwenye eneo la mambo ambayo mtu unapendelea (interests) wengi walikuwa wanaweka kusoma vitabu, kujifunza, kusafiri na kadhalika.

Waliokuwa wanapitia wasifu wa watu, hawakuwa na njia nzuri ya kuweza kudhibitisha lile asemalo mtu, labda kwa kumuuliza tu, kitu ambacho pia hakikuwa na uhakika kwa sababu mtu akiulizwa anajibu kile alichoandika.

Sasa zimekuja zama za mitandao, ambapo watu hawana tena shida ya kujua kama wasifu wa mtu ni kweli au la. Bali wanachofanya ni kuingia GOOGLE na kuandika jina la mtu huyo kisha kutafuta. Kitu kimoja unachopaswa kujua ni kwamba, mtandao wa intaneti huwa hausahau chochote, wanasema INTERNET DOES NOT FORGET. Chochote ambacho umewahi kuandika au kuweka kwenye mtandao wako, mtu akitafuta google anakipata chini ya sekunde moja.

kutafuta google

Mtu akitafuta kitu kwenye mtandao kupitia Google

Sasa kuna umuhimu gani wa wewe kujua hili?

Umuhimu ni mkubwa sana kwa sababu mtandao utasema kila kitu ambacho umekuwa unafanya na kuweka kwenye mtandao, kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii. Kama unataka kuonekana mtu ambaye ni mchapakazi, mpenzi wa kusoma vitabu na sifa nyingine za aina hiyo, inakupasa uwe mara kwa mara unashirikisha sifa zako hizo kwenye mtandao wa intaneti. Washirikishe watu vitabu unavyosoma, waambie watu yale unayojifunza na andika na kuweka mambo yanayoendana na zile sifa ambazo unataka kujulikana nazo kwa wengi.

Unahitaji kuepuka kuweka kwenye mtandao wa intaneti kitu chochote ambacho usingefurahia kama kingechapwa kwenye kurasa za mbele za magazeti yote. Kwa sababu kwa sasa mtandao hauna tofauti na kurasa za mbele za magazeti, mtu yeyote, popote alipo, anaweza kujua kila unachofanya kwenye mtandao wa intaneti.

Hatua mbili ninazokushauri uchukue sasa.

  1. Tengeneza mitandao yako ya kijamii kitaalamu.

Hakikisha mitandao yako yote ya kijamii unayotumia, inaakisi zile sifa ambazo unataka wengine wazione kwako na kukuchukulia wewe hivyo. Japo unahitaji pia kuweka mambo ya kijamii, lakini hakikisha hayaharibu sifa unayotaka kuijenga. Kwa mfano kuweka picha mpo na ndugu, jamaa au marafiki mkifurahi siyo vibaya, lakini kuweka picha ukiwa umelewa siyo kitu kizuri, kutakuharibia sifa unayotaka kujenga.

      2. Kuwa na blog yako binafsi.

Nimekuwa nasisitiza sana kwamba kila mtu anapaswa kuwa na blog. Mpaka watu wanahoji kila mtu akiwa na blog nani anatoma ya mwenzake, na jibu ni hili, siyo lazima uwe na blog ambayo itasomwa na wengine. Bali unaweza kuw ana blog yako binafsi, ambayo utaitumia kuandika yale mambo ambayo unajifunza au unapenda kufuatilia. Kwa mfano kama wewe ni mpenzi wa kusoma vitabu, unaweza kutumia blog yako kuweka kumbukumbu ya vitabu ambavyo umesoma, na hata yale ambayo umejifunza kwenye kila kitabu ulichosoma. Unaweza usikusudie mtu kusoma kabisa, lakini siku moja mtu akawa anakutafuta kwenye mtandao, akaletwa kwenye blog yako na kukutana na vitu vizuri. Au mtu akawa anatafuta kitabu kwenye mtandao akaishia kwenye blog yako.

Tumia mtandao wa intaneti kutengeneza sifa yako ambayo unataka wengine wakuchukulie kwa sifa hiyo. Hakuna wa kukuzuia na wala huhitaji gharama kubwa kufanya hivyo.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Leave a Reply