Jinsi Ya Kuandika Kitabu Ndani Ya Siku 10 Na Kuweza Kukiuza Kwa Urahisi.

Kitu kimoja ambacho nimekuwa naamini ni hichi; kila mtu ni kitabu ambacho kinatembea. Maisha yako ni kitabu, ambacho watu hawajakijua kwa sababu hawawezi kuyasoma moja kwa moja.

Wewe ni wa kipekee sana hapa duniani, hakuna mtu kama wewe na wala hatakuja kutokea mtu kama wewe. Una historia, uzoefu, elimu na makuzi ambavyo ukivichanganya kwa pamoja, unapata kitu ambacho hakiwezi kupatikana kwa wengine.

Mengi ambayo unayajua yanaweza kuwasaidia wengi kama yakiwa kwenye mfumo mzuri. Na mfumo mzuri wa kuweza kuwasaidia wengine, hata kwa kidogo unachojua, ni kuandika kitabu.

Unaweza kuandika kitabu kuhusu jambo lolote ambalo ungependa wengine walijue. Au jambo lolote unalopenda kujifunza au kufuatilia. Kwa njia hii ukawawezesha wengine kujifunza ziadi.

kuandika kitabu

Muhimu zaidi, ni kupitia maandishi ndiyo unaweza kuacha alama ya kudumu hapa duniani. Yote tunayojifunza kwenye falsafa na dini sasa hivi, ni kupitia maandiko waliyofanywa na watu walioishi kipindi cha nyuma. Kama yasingekuwepo maandiko, leo tusingejua kuhusu Yesu, Mohammad, Budha, Mfalme Selemani na wengine wengi.

Hivyo ni muhimu sana wewe uandike kitabu kwenye maisha yako, hata kama hutakichapa wala kukiuza, kinaweza kuwasaidia watoto wako na vizazi vijavyo pia.

Lakini wengi wamekuwa wanashindwa kuandika vitabu vilivyopo ndani yao, kwa sababu wanaona kukaa chini na kuandika kitabu ni kazi hasa. Kwa sababu kitabu cha kawaida, chenye kurasa zaidi ya 200, kinapaswa kuwa na maneno elfu 60. Na vitabu vidogo, ambavyo vina kurasa zaidi ya 100 vinapaswa kuwa na maneno yasiyopungua elfu 20. Sasa kukaa chini na kuandika maneno elfu 20 mpaka yaishe siyo kazi ndogo.

Hapa nakupa njia ya kuandika kitabu ndani ya siku kumi na uwe umemaliza.

Nimekuwa nawakochi watu kuandika vitabu, ambao wamekuwa wanakazana lakini hawamalizi. Lakini ndani ya muda mfupi, usiozidi mwezi, wanakuwa wamekamilisha vitabu vyao.

Ili uweze kuandika kitabu ndani ya siku kumi, unahitaji kupitia hatua hizi sita;

Hatua ya kwanza; fikiria jina la kitabu.

Hapa unakaa chini na kufikiria jina ambalo utakipa kitabu chako. Unaweza kufikiria jina kulingana na kile unachoandika. Jina linapaswa liwe la kuvutia watu kutaka kusoma kitabu. Lakini pia jina lisiwe refu sana. Kwenye makala zijazo nitajadili kwa kina kuhusu njia bora ya kupata jina zuri la kitabu.

Hatua ya pili; fikiria sura kumi za kitabu chako.

Kwenye hatua ya pili, unafikiria mambo makuu kumi ambayo ungetaka mtu aondoke nayo kwenye kusoma kitabu chako. Mambo haya kumi yafanye kuwa sura za kitabu chako. Unaweza kuwa na pungufu ya hapo au zaidi ya hapo, hapa nimekuambia kumi ili twende vizuri na siku zetu kumi.

Hatua ya tatu; kwenye kila sura weka ambo mawili muhimu.

Baada ya kuwa na sura 10 za kitabu chako au idadi nyingine kama ulivyopanga wewe, unahitaji kuchagua mambo mawili muhimu unayotaka mtu aondoke nayo kwenye kila husika. Hapa pia unaweza kuwa na pungufu au zaidi, ni wewe tu utakavyo.

Hatua ya nne; kila siku andika maneno yasiyopungua elfu 2.

Baada ya kuwa na vichwa viwili kwenye kila sura, sasa unaanza kazi ya kuandika. Kila siku kamilisha kuandika sura moja na hakikisha unaandika siyo chini ya maneno elfu 2. Kwa kwenda hivi, siku 10 utakuwa umemaliza sura zako kumi.

Hatua ya tano; hitimisha kitabu chako.

Hapa unaweka maelezo ya kuhitimisha, unaweka maelezo ya utangulizi, unaweka maneno ya shukrani na hitimisho la kitabu chako.

Hatua ya sita; chapa kitabu au kisambaze kama nakala tete.

Ukishakamilisha kitabu, unaweza kukichapa kama nakala ngumu kwa kuwasiliana na wachapaji mbalimbali na kuchagua. Hapo watakusaidia kukipangilia vizuri na kutengeneza ganda la nje lenye mvuto.

Kama huna uwezo wa kukichapa kwa kuanzia, unaweza kukisambaza kama nakala tete, kwa kuwatumia watu kwenye email au mitandao kama wasap.

Hapo kuna vitu muhimu ya kuzingatia kama bei ya kitabu na njia ya kusambazao.

Kwa upande wa bei, kama utachapa utaangalia gharama za uchapaji na usambazaji kisha utaweka bei ambayo watu wanaweza kuimudu na wewe kupata faida.

Kama utasambaza kama nakala tete, utapanga bei kulingana na uwezo wa soko unalolenga na faida unayotaka kupata.

Hivyo ndivyo unavyoweza kuwa na kitabu chako ndani ya siku kumi. Kama kuandika maneno elfu 2 kwa siku ni mengi, basi andika maneno elfu 1 kila siku na itakuchukua siku 20 mpaka mwezi. Au andika maneno mia tano kila siku na ndani ya miezi miwili una kitabu chako. Vyovyote utakavyochagua, muhimu ni kuwa na ramani ya kitabu chako na kuandika kila siku.

 

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

1 thought on “Jinsi Ya Kuandika Kitabu Ndani Ya Siku 10 Na Kuweza Kukiuza Kwa Urahisi.

Leave a Reply