Changamoto Mbili Zinazowakwamisha Waandishi Wa Makala Na Jinsi Ya Kuzishinda.

Kuna changamoto kuu mbili ambazo waandishi wa makala na hata vitabu wanakutana nazo.

Moja ni kukosa kitu cha kuandika, hapa unapanga kuandika, lakini unaona hakuna unachoweza kuandikia. Unaweza kukaa ukitoa macho kwenye eneo lako la kuandika na usipate kabisa uandike nini.

Changamoto ya pili ni kutumia muda mwingi kwenye kuandika na hata kuahirisha unapokuwa umefika katikati. Ukishaachia kuandika katikati, inakuwa vigumu zaidi kuja kuanza tena kuandika.

Changamoto hizi mbili zimewakwamisha waandishi wengi na hivyo kuzitatua kutakuwezesha kupiga hatua. Muhimu zaidi ni kwamba, kama mwandishi, kila siku unapaswa kuandika, hivyo kukosa kitu cha kuandika, au kutumia muda mwingi kwenye uandishi, kunakuwa kikwazo kwa mafanikio yako.

Unatatuaje changamoto hizi mbili?

Changamoto hizi mbili zinaweza kutatuliwa na ukaweza kuwa na mawazo mengi ya kuandika na hata kuandika ndani ya muda mfupi. Zifuatazo ni hatua muhimu kufuata ili changamoto hizi zisikuzuie.

  1. Panga utakachokwenda kuandika kabla ya muda wa kuandika.

Usisubiri mpaka muda wa kuandika ndipo ufikirie uandike nini. Kwa kufanya hivyo utakosa uandike nini na kadiri utakavyokazana ndivyo unazidi kukosa.

Badala yake panga mapema unakwenda kuandika nini, kabla ya muda wa kuandika haujafika. Kama utaratibu wako ni kuandika asubuhi, basi jioni andaa kabisa utaandika nini siku inayofuata. Hili pia linakupa faida, maana unapokuwa na wazo la kuandikia, ukilala na kuamka nalo, unakuwa umelitafakari kwa kina zaidi.

  1. Fanya utafiti kabla ya muda wa kuandika.

Kinachowakwamisha waandishi wengi, na kuwapelekea kutumia muda mwingi ni kufanya utafiti. Siku hizi kufanya utafiti ni rahisi kupitia njia ya intaneti. Na hivyo wengi husubiri mpaka muda wa kuandika, hivyo wanaandika huku wakifanya utafiti kwenye intaneti. Hili linafanya zoezi la kuandika kuwa refu.

Unachopaswa kufanya ni kufanya utafiti wako kabla ya muda wa kuandika haujafika. Unachofanya ni unapokuwa na wazo la kuandika, lifanyie utafiti kabisa, chagua ni hoja gani unakwenda kuiongelea na vitu gani vitaitetea hoja yako. Unapofika wakati wa kuandika, kazi yako ni kuandika na siyo tena kufanya utafiti.

  1. Tenga muda maalumu wa kuandika, na andika, usifanye kingine.

Ukishajua unatumia muda gani kuandika makala yako, tenga muda maalumu ambao utakuwa unaandika kila siku. Na kila siku andika kwenye muda ule. Muda huo wa kuandika ulinde kabisa, usikubali uingiliwe na kelele yoyote. Na unapoanza kuandika, andika mpaka ualize, usiishie njiani. Kwa sababu unapoishia njiani, itakuchukua muda mrefu unapokuja kuanza tena kuandika.

Haya ni mambo matatu ambayo ukiweza kuyafanya, utaboresha uandishi wako, kila wakati utakuwa na kitu cha kuandika, utapunguza muda wa kuandika na pia utaacha kuahirisha uandishi wako na kuishia njiani. Yafanyie kazi kila siku na endelea kuboresha uandishi wako kila siku.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

1 thought on “Changamoto Mbili Zinazowakwamisha Waandishi Wa Makala Na Jinsi Ya Kuzishinda.

  1. Pingback: Jinsi Unavyoweza Kupata Mawazo Ya Kuandika Makala Kila Siku Kwenye Blog Yako. | MTAALAMU Network

Leave a Reply