Kabla Hujafikiria Kulipwa Kwenye Mtandao, Andika Kwanza Makala 100.

Kila siku nimekuwa napokea maombi wa watu wanaotaka kuanza kutengeneza kipato kwenye mtandao kwa kutumia blog zao. Ninapoangalia blogu za watu hao, nakutana na kitu kimoja, bado hazijafikia hatua ya kuweza kutengeneza kipato cha uhakika.

Watu wamekuwa na haraka sana ya kutengeneza kipato kwenye mtandao, na haraka hii imewafikisha kwenye mikono ya watu ambao wanawadanganya na kuwalia fedha zao. Wanawaambia ili blog zao zitengeneze kipato basi watengenezewe adsense, hii ni program ya google ya kuweka matangazo kwenye blog.

Watu hufikiri wakishakuwa na adsense basi pesa nje nje, na hakuna uongo kama huo. Ili uweze kutengeneza fedha kwa kutumia adsense, unahitaji kuwa na watembeleaji wengi, wengi mno, malaki kwa siku. Na hapo siyo kwamba utakuwa na uhakika wa kutengeneza kipato kikubwa kwa siku, ni dola chache pekee.

Sasa kwa jamii yetu, hasa ya kitanzania, kuna kitu kimoja kinaweza kukuletea wasomaji wengi sana kwenye blog yako kwa siku, kitu hicho ni habari za udaku na picha za uchi. Ukiwa na blog ya aina hiyo, utapata wasomaji wengi na huenda ukapata dola chache kila siku kwenye adsense. Lakini kwa blog za mafunzo, blog ambazo zinatoa maarifa, unapoanza huwezi kuwa na wasomaji wengi kiasi hicho.

Na swali muhimu sana, unafikiri ukiwa na blog ya udaku na picha za uchi inakufikisha wapi, hasa siku za baadaye? Kama unataka fedha tu sawa, ila kama unataka kujenga jina lako kama mtaalamu, blog ya udaku haikufai, ni kupoteza muda wako na heshima yako.

Hivyo nimekuwa nasisitiza, njia ya mtu kulipwa kwenye mtandao wa intaneti kupitia blogu yake ni kutoa huduma zake mwenyewe. Unakuwa na wasomaji, ambao wanakuamini na kukufuatilia, na hapo unawapa makala za bure, na baadaye unawauzia huduma zako nyingine. Huduma kama vitabu, ushauri wa kulipia, mafunzo ya semina na njia nyingine nyingi.

SOMA;Njia Kumi (10) Unazoweza Kuanza Kutumia Leo Kutengeneza Fedha Kwenye Mtandao Wa Intaneti.

Sasa, unapoanzisha blogu yako, kuanza kutaka kulipwa ni kujidanganya. Kama una makala 10, 20 au 30 na unataka watu wakulipe unajidanganya. Watu hata hawajakujua bado, hawajakuzoea bado, unakimbilia wapi?

Ninachowashauri wanaoanza blogu ni hichi, andika kwanza makala 100, ndiyo namaanisha makala MIA MOJA, kabla hujaanza kuwauzia watu kitu. Andika kuwapa watu maarifa sahihi juu ya kile unachoandikia, wape watu na wape zaidi. Hakikisha wanapokuwa na shida kuhusiana na eneo unaloandikia, wa kwanza kufikiriwa ni wewe. Baada ya hapo ndipo unaweza kuja na huduma nyingine na watu wakakusikiliza.

Kwa nini makala 100? Kwa sababu 100 siyo namba ndogo. Kwa kuandika makala 100, kama ni makala moja kwa siku, itakuchukua labda miezi mitatu, na inaweza kwenda mpaka mwaka mmoja kulingana na idadi ya makala unazoandika kwa wiki. Hichi ni kipindi kizuri cha wewe kujitengeneza kama mtaalamu. Wewe mwenyewe unajijua kiundani, unaona ni maeneo gani ambayo unaweza zaidi. Kipindi hichi pia utawajua wasomaji wako vizuri, kwa maswali watakayokuuliza na ushauri watakaokuomba.

Hivyo kabla hujaanza kuwauliza watu wakulipe, kwa namna yoyote ile, andika kwanza makala 100, makala za maana zenye kutoa maarifa kweli kwa wasomaji wako. Na hapo utakuwa umejiweka kwenye nafasi nzuri ya kuweza kutengeneza kipato.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

1 thought on “Kabla Hujafikiria Kulipwa Kwenye Mtandao, Andika Kwanza Makala 100.

  1. Pingback: Jinsi Ya Kuendelea Kuwa Na Makala Zinazoenda Hewani Kila Siku Hata Kama Huna Mtandao Kila Siku. | MTAALAMU Network

Leave a Reply