Zingatia Misingi Hii Mitatu(03) Ya Kutengeneza Kipato Kwenye Mtandao Wa Intaneti.

Kila kitu kwenye maisha kina misingi yake,

Ni wale wanaoijua misingi na kuisimamia ndiyo mara zote wanabaki salama. Wengine ambao wanaipuuza misingi kwa sababu ya vitu vinavyoonekana vya haraka, huwa wanaishia kupotea kabisa.

Nakumbuka wakati naanza safari hii ya kutengeneza kipato kupitia mtandao wa intaneti, nilikuwa sijui wapi pa kuanzia. Hivyo nilikuwa naangalia watu wanafanya nini. Au naingia google na kuandika HOW TO MAKE MONEY ONLINE, yanakuja majibu mengi, mengine hata sikuwa naelewa.

Nikawa naona watu wanatoa maelezo ya kupewa link halafu unabonyeza matangazo na unaona namna dola zinasoma kwenye akaunti yako. Nilijiunga na moja ya aina hiyo, nikabonyeza matangazo kweli, mpaka nikafikisha dola 25, ambacho kilikuwa ndiyo kiwango cha chini kulipwa. Basi nikaanza mchakato wa kutaka nilipwe changu, hapo ndipo nilipojifunza somo kubwa sana, kwamba kutengeneza fedha kwenye mtandao unahitaji misingi. Kwa kifupi sikulipwa, lakini nilipata somo, ambalo nitakwenda kukushirikisha wewe leo ili usipoteze muda wako.

Misingi ya kutengeneza kipato kwenye mtandao ipo mingi, yapo mengi ya kuzingatia, nimeyaandikia mpaka kitabu (unaweza kukisoma hapa), lakini leo nataka nikupe misingi mitatu ambayo ukiifuata, hutakuja kudanganywa na utaijenga biashara yako vizuri sana.

Msingi wa kwanza; fanya utafiti.

Unahitaji kufanya utafiti mzuri sana wa namna gani utatengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti. Nilishasoma kitabu kimeandika njia 1000 za kutengeneza kipato kwenye mtandao! Sasa hebu jiulize hapo unaanzia wapi.

Ni muhimu ufanye utafiti, kwa kuangalia kile ambacho unafanya wewe kwenye mtandao, na kuona watu wanaweza kukulipaje. Angalia njia zote ambapo unaweza kuongeza thamani kwa watu na wao wakakulipa. Na utafiti huu siyo unaufanya kwanza ndiyo unakuwa na blog, badala yake unakuwa na blog huku ukiendelea kuufanya.

Njia ambazo nimekuwa nawashauri watu waanze nazo, baada ya kuwa wamepata wasomaji kiasi kwenye blog zao ni kuandika kitabu, kuendesha semina au kozi fupi, kuwa na makala maalumu kwa waliolipia, kuwa na kundi la wasap au facebook kwa wale wanaolipia, na pia ushauri kwa wanaolipia.

Sasa kwa njia hizi, wewe unahitaji kufanya utafiti kwa wasomaji wako. Kama ni kitabu unafikiria kuandika, je ni kitabu gani? Kinachowasaidia nini? Utakiuza kwa bei kiasi gani? Lazima haya yote uyafanyie utafiti, ili unapokaa chini na kuandika kitabu, uje na kitu ambacho watu wanakihitaji, na kwa bei ambayo wanaweza kuimudu.

Unaweza kuendesha utafiti wako kwa kuwauliza wasomaji maswali, kwa kuangalia mwitikio wao na hata maswali wanayouliza na ushauri wanaoomba mara kwa mara.

Kwa mimi nimejiwekea kasheria kadogo kwamba nikiombwa ushauri na zaidi ya watu 10 kwenye kitu kimoja, basi napaswa kuandika kitabu chenye kutoa mwongozo juu ya jambo hilo. Kwa njia hii yeyote atakayeomba ushauri kwenye jambo hilo, kwanza nitamwelekeza asome kitabu, halafu ndipo tushauriane kwa kuanzia hapo. Nilichogundua wengi wanasaidiwa na kitabu na hata wanakuwa hawana maswali tena.

Utafiti ni muhimu kwenye maisha yako yote ya kibiashara kwenye intaneti. Fanya utafiti kwenye kila jambo, na hakikisha unachukua hatua ili kuboresha zaidi.

Msingi wa pili; jielimishe.

Soma vitabu, soma blog za wengine.

Nimesema mengi kwenye msingi wa kwanza, sitasema mengi hapa. Ninachokusisitiza ni hichi, soma vitabu, tena vingi kadiri uwezavyo. Naweza kusema kiwango cha chini kiwe angalau kitabu kimoja kwa wiki. Na kama huwezi kabisa, umebanwa kabisa, basi soma vitabu viwili kwa mwezi. Kama huwezi kusoma vitabu kabisa, yaani mwezi unaisha hujasoma kitabu chochote, funga bloga yako na kafanye mambo mengine yanayokufaa.

Kwa kusoma vitabu unaongeza maarifa, juu ya mambo mbalimbali. Na pia unajifunza njia bora za uandishi. Ili uwe mwandishi bora, lazima uwasome waandishi wengine. Utaona namna watu wanapangilia mawazo yako na wewe kujifunza na kuboresha zaidi.

SOMA;Kama Unataka Kutengeneza Fedha Kwenye Mtandao, Jukumu Lako Kubwa Ni Hili.

Na kama nilivyoeleza kwenye makala hii ya kupata mawazo ya kuandika, kupitia vitabu unaweza kupata mawazo mazuri ya kuandika, au hata kuchambua kitabu ulichosoma na kuwashirikisha wasomaji wako. Faida ni nyingi za kusoma vitabu.

Soma pia blog za waandishi unaowakubali na unaopenda kujifunza kwao. Hakikisha unatembelea blog zao kila siku kama wanapost kila siku. Hawa watakupa maarifa ya ziada, lakini usiyatumie kama mawazo yako ya kuandika, vinginevyo utajikuta unaiga vitu vyake na wasomaji wakuone wewe siyo halisi.

Usiache kutembelea mtandao huu wa www.mtaalamu.net/pesablog kila siku, yapo mengi ya kujifunza kuhusu kutengeneza fedha kwenye mtandao.

Msingi wa tatu; weka kazi.

Huwa haipiti siku sijapata ombi la ushauri kutoka kwa vijana, ambao wanaangalia fursa ya kutengeneza kipato kwenye mtandao kama njia ya mteremko ya kupata fedha. Huwa najichekea mwenyewe kwa sababu nashindwa kuelewa watu wanatoa wapi dhana hii.

Hadithi ya kweli, wiki hii kuna kijana alikuwa ananipigia simu mara nyingi akiniuliza kuhusu kutengeneza kipato kwenye youtube. Nikamuuliza una video ngapi umeshaweka? Akaniambia sita, nikamwambia una watu wangapi wanaziangalia, akaniambia kama 50. Nikamwambia hebu weka kazi kwanza, hebu fikisha video 100 na waangaliaji zaidi ya 1000 kwenye video halafu uje tuongee. Akaendelea kusisitiza nimpe tu mwanga, nikamwambia anipe link ya chanel yake nione video zake, kwa kweli hakuna alichokuwa anafanya. Kwa nilivyoona video zake ni kama anafika mahali, anachukua simu yake na kurekodi kitu anachoona, halafu anaweza kwenye youtube. Sikuona kitu chochote ambacho anafundisha watu au watu wananufaika, na yeye anafikiria kutengeneza kipato, bila ya kuweka kazi yoyote.

Kufupisha maelezo rafiki ni hivi, weka kazi, weka kazi tena siyo kazi ya kitoto. Nilishaeleza hili kwenye kuandika makala 100, na nimekuwa nalisisitiza mara nyingi. Andika kila siku, sambaza kazi zako kwa watu wengi. Njoo na maarifa bora zaidi, wasaidie watu kutatua matatizo yao. Na endelea kuweka juhudi, hapo ndipo unaweza kuwa na uhakika na kutengeneza kipato.

Kama unafikiria kutengeneza kipato kwenye mtandao lakini hupo tayari kuweka kazi, nakushauri uache kupoteza muda wako kwa jambo hili. Jipange na uweke kazi, au tafuta jambo jingine la kupotezea muda wako.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

1 thought on “Zingatia Misingi Hii Mitatu(03) Ya Kutengeneza Kipato Kwenye Mtandao Wa Intaneti.

  1. Pingback: Unachojua Wewe, Wapo Wengi Hawakijui, Washirikishe Utengeneze Kipato. | MTAALAMU Network

Leave a Reply