Njia tano(05) za kuepuka kupoteza muda kwenye mitandao ya kijamii kama mwandishi.

Kwa sababu sehemu kubwa ya kazi yako ni kutoa maarifa kupitia intaneti na mitandao ya kijamii, unaweza kushindwa kutofautisha kufanya kazi na kupoteza muda.

Kwa sababu nimekuwa naona watu wengi wakipotea muda kwenye mtandao, kwa kujidanganya kwamba wanafanya kazi. Labda wanatafiti kitu, au wanawafuatilia wasomaji wao ili kujua wanahitaji nini.

Kuna mstari mwembamba sana kati ya kufanya kazi na kupoteza muda kwenye mtandao. Kwa sababu mara nyingi unaweza kujiambia unaingia kwenye mtandao kuangalia kitu fulani, ukajikuta umepotelea kabisa kwenye mitandao ya kijamii au ukiangalia mambo mengine ambayo siyo yaliyokupeleka pale.

Lakini unajua utajidanganya nini? Kwamba siku moja nitahitaji maarifa haya, acha niyapitie na kuyasave.

Unahitaji kuwa makini sana kwa sababu kazi yako ipo karibu sana na usumbufu. Na hivyo usipokuwa na mfumo mzuri, utajikuta kila wakati unapopanga kufanya kazi, hukamilishi kwa wakati.

Ili kuepuka kupoteza muda kwenye intaneti kwa kisingizio cha kufanya kazi, zingatia yafuatayo.

  1. Tenga muda maalumu wa kuandaa maarifa unayowashirikisha wasomaji wako. Muda huu uwe ambao utakuwa na utulivu, na katika muda huo, usiwe kwenye mtandao wa intaneti. Kwa maneno rahisi, kwenye muda huo zima data.
  2. Fanya utafiti kabla ya muda wa kuandika. Usisubiri mpaka muda unapoandika ndiyo ujiulize sasa niandike nini, au useme ngoja niingie google nitafute mawazo zaidi ya kutetea kile unachoandika. Kwa njia hii utapoteza muda mwingi. Fanya maandalizi mapema kabisa, na unapofika wakati wa kuandika, andika, kwa yale maarifa uliyonayo. Yanakutosha sana kama ukiyatumia vizuri.
  3. Pangilia muda wa makala kwenda hewani na itenge kwenda hewani kabla ya muda huo. Siyo lazima kila muda wa makala kwenda hewani basi na wewe unapaswa kuwa hewani. Badala yake unahitaji kupangilia kwenye blog yako na mengine yatafanyika, hata kama haupo hewani muda huo. Kwenye kila blog kuna sehemu ya SCHEDULE, ukienda hapo unapanga makala yako iende hewani siku gani, saa ngapi na dakika ngapi. Kwa kutumia njia hiyo, unaweza kuandika makala zako hata saa nane usiku, ukaischedule kwenda hewani asubuhi.
  4. Tenga muda maalumu wa kuingia kwenye mitandao ya kijamii, na usiruhusu kuletewa taarifa ya kinachoendelea. Kwa maneno mengine, ondoa kabisa notification kwenye kifaa chako. Hivyo utapunguza usumbufu wa ujumbe unaopokea kwamba kuna mtu ka-like ulichopost. Pia usiwe kwenye mitandao muda wote. Kumbuka unahitaji kusoma vitabu, unahitaji kufanya tafiti, na huenda una kazi zako nyingine, au una kitabu unaandika, au unaandaa makala nyingine.
  5. Pitia email zako mara moja kwa siku. Kama mawasiliano yako ya email yapo wazi kwa wasomaji, au kama una email list na unawatumia wasomaji wako makala kwenye email, utakuwa unapokea email nyingi kila siku. Sasa ukianza mchezo wa kujibu kila email kila inapoingia, hutaweza kufanya kazi. Badala yake tenga muda kila siku wa kupitia email na kuzijibu. Kwa kufanya hivi utaokoa muda wako na kuweza kufanya mengine.

Mambo haya matano yatakusaidia sana kwenye kutumia muda wako vizuri kwenye mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii. Kwenye yote hayo, kumbuka kitu muhimu sana, kila kitu kinaweza kusubiri, kasoro tu kusoma na kuandika. Yaani iwe ni mtu ametuma email au ujumbe kwenye mtandao, unaweza kusubiri mpaka pale utakapopata muda, lakini kusoma na kuandika, ni vitu ambavyo haviwezi kusubiri, lazima uvifanye, kila siku na kwa wakati wake.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Leave a Reply