Monthly Archives: June 2017

Hivi Ndivyo Unavyojizuia Kunufaika Na Mtandao Wa Intaneti.

Mtandao wa intaneti, ni fursa bora sana kwa zama zetu. Ni kitu ambacho kimempa nguvu kila mtu ya kufanya kile ambacho, miaka michache iliyopita, kilifanywa na wachache pekee, ambao walichaguliwa au walipendelewa.

Siku za nyuma ili uweze kuandika kitabu, kutengeneza kipindi cha tv au redio, kuandika makala, ilikuw ampaka ukubalike na vyombo vinavyozalisha vitu hivyo. Kama hukuchaguliwa au kukubalika basi ndiyo umekosa fursa.

Lakini sasa hivi, kama unataka kuandika kitabu ni wewe tu unajizuia, kwa sababu unaweza kukiandika mwenyewe na hata kukiuza mwenyewe kwenye mtandao wa intaneti, wala hata huhitaji kukichapa. Kama unataka kutengeneza kipindi cha tv, ni wewe tu uchukue simu yako, urekodi video yako na kuiweka kwenye mtandao. Hakuna wa kukuzuia au wa kukuambia usubiri mpaka akuchague.

Pamoja na fursa hii kubwa, bado watu wanajizuia kuchukua hatua.

Bado watu wanapenda kuandika, lakini wanasubiri, hawaandiki na wanasubiri wasijue wanachosubiri ni nini.

Bado watu wana mawazo mazuri ya kutengeneza vipindi vizuri vya tv au redio, lakini hawazalishi, wanasubiri mpaka mtu aje kuwaambia wanaweza.

Ninachotaka kukuambia leo ni hichi, wazo ulilonalo, hakuna wakati bora wa kulifanyia kazi kama sasa.

Kama ni wazo la kuandika, anza na blog, andika kile ambacho ungependa wengine wajifunze. Andika kile ambacho wewe mwenyewe unapenda kujifunza.

Una wazo la kipindi cha tv au redio? Unasubiri nini? Chukua simu yako, rekodi sauti au video yako na washirikishe watu kwenye mtandao wa intaneti. Mitandao karibu yote ya kijamii inaruhusu kuweka video, mtandao wa youtube ni mahususi kwa ajili ya video, kama unasubiri, umeamua kujichelewesha wewe mwenyewe.

SOMA;Sheria Muhimu Ya Kwenye Mtandao, Kwanza Kuwa Mtu Halisi.

Huu siyo wakati wa kusubiri rafiki, huu ni wakati wa kuinuka na kuingia kwenye mchezo. Mtandao wa intaneti umeleta usawa kwenye kila aina ya mchezo, kila aina ya biashara. Kinachokuzuia sasa, ni wewe mwenyewe, hakuna mwingine yeyote.

Unaposubiri mpaka watu wakuambie unaweza, au unaruhusiwa kufanya, ndiyo unajizuia wewe mwenyewe kunufaika. Ni vyema ukachukua hatua sasa kwa sababu unakosa mengi kwa kutochukua hatua.

Chochote ambacho unafikiria kufanya, ambacho kitawanufaisha wengine, anza kufanya sasa. Anza kwa kuandika kwenye mitandao ya kijamii, andika kwenye blog yako na rekodi sauti na video kisha weka kwenye intaneti. Endelea kuboresha kile unachofanya na baada ya kuwa utakuwa umetengeneza jukwaa utakalotumia kuwafikia wengi zaidi na hata kunufaika kwa kipato pia.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Kabla Hujafikiria Kulipwa Kwenye Mtandao, Andika Kwanza Makala 100.

Kila siku nimekuwa napokea maombi wa watu wanaotaka kuanza kutengeneza kipato kwenye mtandao kwa kutumia blog zao. Ninapoangalia blogu za watu hao, nakutana na kitu kimoja, bado hazijafikia hatua ya kuweza kutengeneza kipato cha uhakika.

Watu wamekuwa na haraka sana ya kutengeneza kipato kwenye mtandao, na haraka hii imewafikisha kwenye mikono ya watu ambao wanawadanganya na kuwalia fedha zao. Wanawaambia ili blog zao zitengeneze kipato basi watengenezewe adsense, hii ni program ya google ya kuweka matangazo kwenye blog.

Watu hufikiri wakishakuwa na adsense basi pesa nje nje, na hakuna uongo kama huo. Ili uweze kutengeneza fedha kwa kutumia adsense, unahitaji kuwa na watembeleaji wengi, wengi mno, malaki kwa siku. Na hapo siyo kwamba utakuwa na uhakika wa kutengeneza kipato kikubwa kwa siku, ni dola chache pekee.

Sasa kwa jamii yetu, hasa ya kitanzania, kuna kitu kimoja kinaweza kukuletea wasomaji wengi sana kwenye blog yako kwa siku, kitu hicho ni habari za udaku na picha za uchi. Ukiwa na blog ya aina hiyo, utapata wasomaji wengi na huenda ukapata dola chache kila siku kwenye adsense. Lakini kwa blog za mafunzo, blog ambazo zinatoa maarifa, unapoanza huwezi kuwa na wasomaji wengi kiasi hicho.

Na swali muhimu sana, unafikiri ukiwa na blog ya udaku na picha za uchi inakufikisha wapi, hasa siku za baadaye? Kama unataka fedha tu sawa, ila kama unataka kujenga jina lako kama mtaalamu, blog ya udaku haikufai, ni kupoteza muda wako na heshima yako.

Hivyo nimekuwa nasisitiza, njia ya mtu kulipwa kwenye mtandao wa intaneti kupitia blogu yake ni kutoa huduma zake mwenyewe. Unakuwa na wasomaji, ambao wanakuamini na kukufuatilia, na hapo unawapa makala za bure, na baadaye unawauzia huduma zako nyingine. Huduma kama vitabu, ushauri wa kulipia, mafunzo ya semina na njia nyingine nyingi.

SOMA;Njia Kumi (10) Unazoweza Kuanza Kutumia Leo Kutengeneza Fedha Kwenye Mtandao Wa Intaneti.

Sasa, unapoanzisha blogu yako, kuanza kutaka kulipwa ni kujidanganya. Kama una makala 10, 20 au 30 na unataka watu wakulipe unajidanganya. Watu hata hawajakujua bado, hawajakuzoea bado, unakimbilia wapi?

Ninachowashauri wanaoanza blogu ni hichi, andika kwanza makala 100, ndiyo namaanisha makala MIA MOJA, kabla hujaanza kuwauzia watu kitu. Andika kuwapa watu maarifa sahihi juu ya kile unachoandikia, wape watu na wape zaidi. Hakikisha wanapokuwa na shida kuhusiana na eneo unaloandikia, wa kwanza kufikiriwa ni wewe. Baada ya hapo ndipo unaweza kuja na huduma nyingine na watu wakakusikiliza.

Kwa nini makala 100? Kwa sababu 100 siyo namba ndogo. Kwa kuandika makala 100, kama ni makala moja kwa siku, itakuchukua labda miezi mitatu, na inaweza kwenda mpaka mwaka mmoja kulingana na idadi ya makala unazoandika kwa wiki. Hichi ni kipindi kizuri cha wewe kujitengeneza kama mtaalamu. Wewe mwenyewe unajijua kiundani, unaona ni maeneo gani ambayo unaweza zaidi. Kipindi hichi pia utawajua wasomaji wako vizuri, kwa maswali watakayokuuliza na ushauri watakaokuomba.

Hivyo kabla hujaanza kuwauliza watu wakulipe, kwa namna yoyote ile, andika kwanza makala 100, makala za maana zenye kutoa maarifa kweli kwa wasomaji wako. Na hapo utakuwa umejiweka kwenye nafasi nzuri ya kuweza kutengeneza kipato.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Jinsi Unavyoweza Kupata Mawazo Ya Kuandika Makala Kila Siku Kwenye Blog Yako.

Kwa mtu yeyote ambaye anataka kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti, kitu cha kwanza kabisa anachopaswa kufanya ni kuwa na blog. Blog ndiyo nyumbani kwako kwenye mtandao wa intaneti. Hapa ndipo unapoweka kila kitu kinachokuhusu wewe. Mitandao ya kijamii ni sehemu muhimu, ila haiwezi kukusaidia sana iwapo huna blog yako mwenyewe.

Kuwa na blog pekee haitoshi, kwa sababu watu hawataijua blog yako kwa sababu ipo. Bali wataijua blog yako kutokana na kazi unazoweka kwenye blog yako. Unahitaji kuwa na makala nyingi kwenye blog yako, makala zinazowasaidia watu kutatua matatizo yao na kuwapa maarifa ya kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi.

Njia ya uhakika ya kuifanya blog yako kuwa na makala nyingi, na kuwa karibu na watu ni kuandika kila siku. Unapoandika kila siku inakuwa rahisi kwako kuikuza blog, na pia makala zinakuwa mpya kila siku. Tofauti na kuandika makala nyingi siku moja kwa wiki au mwezi, ambapo muda unaweza usiwe rafiki kwako, na makala zikawa hazina utofauti mzuri.

Changamoto ya kuandika kila siku ni hii; kuna wakati mwandishi unakosa cha kuandika. Unapanga muda wa kuandika, lakini muda unapofika unaona huna cha kuandika. Unakazana kufikiria lakini ndiyo kabisa unakosa cha kuandika.

Hapa nakupa njia za kukuwezesha kupata mawazo ya kuandika kila siku, na kamwe hutakosa kitu cha kuandika.

  1. Soma sana vitabu vinavyoendana na yale mambo unayoandika.

Hakikisha kila siku kuna kitabu unachosoma kinachohusiana na mambo unayoandikia. Vitabu vipo vingi sana kama utatafuta na kutenga muda wa kusoma kila siku. Kupitia vitabu unaweza kupata mawazo ya kuandikia. Na kizuri zaidi, unaweza kuchambua kitabu unachosoma. Hivyo kitabu kimoja kinaweza kukupa makala nyingi uwezavyo.

Hivyo kama utapanga kusoma angalau kitabu kimoja kila wiki, hutakosa mawazo matatu ya kuandikia na pia kuandika makala ya uchambuzi wa kitabu hicho.

Usiniambie huna muda wa kusoma, mwandishi ambaye hasomi hajui kile anachoandika.

  1. Angalia matatizo yako binafsi, na yale unataka kujifunza.

Kila siku jiulize ni tatizo gani unalo ambalo ungependa kulitatua? Au ni kitu gani ambacho ungependa kujifunza zaidi? Tatua tatizo lako, au jifunze kile unachotaka kujifunza, kisha washirikishe wasomaji wako kwa kuwaandalia makala zinazoendana na kitu kile. Hii ni njia nzuri sana kwa sababu chochote unachotaka kujifunza, wapo wengine kama wewe ambao wanataka kujifunza pia. Wakijua unajifunza, watakuwa wafuatiliaji wako wa karibu.

  1. Angalia matatizo ya wengine.

Kwenye lile eneo unaloandikia, angalia matatizo ya wengine, angalia watu wanasumbuka na nini zaidi. Angalia makosa watu wanafanya, angalia changamoto watu wanakutana nazo. Na wewe zifanyie kazi, jifunze namna ya kutatua na washirikishe kwenye makala. Hakikisha kila changamoto watu wanaipitia unaitafutia suluhisho na kuwashirikisha wasomaji wako.

Habari njema ni kwamba, matatizo ya watu hawaishi, changamoto hazitakuja kukoma duniani, hivyo kila wakati utakuwa na mambo mengi ya kuandikia.

SOMA; Changamoto Mbili Zinazowakwamisha Waandishi Wa Makala Na Jinsi Ya Kuzishinda.

  1. Wafundishe watu kitu ambacho hawajui.

Kuna mambo mengi sana ambayo watu hawajui juu ya eneo unaloandikia. Yajue mambo hayo na wafahamishe watu. Waandishi wengi wamekuwa wanafikiri kwamba kile wanachojua wao basi kila mtu anajua. Utashangaa sana ukiwauliza watu, utagundua uelewa wao ni mdogo sana kuliko ulivyofikiri. Na wakati mwingine hata kama wanajua, taarifa nyingi walizonazo siyo sahihi. Hivyo kila wakati wape watu maarifa sahihi kwa maeneo muhimu ambayo kila mtu anapaswa kuyajua.

  1. Angalia kile ambacho kila mtu anakubaliana nacho, halafu pingana nacho.

Wakati mwingine unaweza kuamua kuwa tofauti na wengine. Mara nyingi kitu kikiwa kinashabikiwa na kukubaliwa na wengi, huwa kuna matatizo watu huwa hawayaoni. Mapenzi yao yanawapa upofu na hivyo kujikuta kwenye changamoto. Wewe kaa chini na angalia kwa kina, kisha andika makala ya kuwaonesha watu kile ambacho hawaoni.

Unapochagua hili kuwa makini, kuna watu watakupinga na hata kukuchukia, hivyo hakikisha chochote unachopinga, una udhibitisho wa kufanya hivyo. Usiandike tu kujitafutia umaarufu.

  1. Soma tafiti mbalimbali zinazohusiana na unachoandika.

Kuna tafiti nyingi huwa zinafanywa kwenye kila eneo la maisha yetu. Tafiti hizi mara nyingi huwa ni kwa sababu za kitaaluma na hivyo wanataaluma ndiyo wanazifaidi. Wananchi wa kawaida huwa hawazielewi tafiti hizo. Unaweza kutumia fursa hii kuzisoma tafiti na kujaribu kuzielezea kwa lugha ambayo mwananchi wa kawaida anaweza kuielewa.

Kwa njia hii utapata makala nzuri za kuandika na watu watanufaika na tafiti zinazofanywa kila siku.

Haya ni maeneo sita unayoweza kuyatumia kila mara na ukawa na makala za kuandika kila siku. Muhimu ni wewe kuwa na mpangilio mzuri ili kuweza kuwa na makala nzuri na zenye msaada kwa wasomaji wako.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Changamoto Mbili Zinazowakwamisha Waandishi Wa Makala Na Jinsi Ya Kuzishinda.

Kuna changamoto kuu mbili ambazo waandishi wa makala na hata vitabu wanakutana nazo.

Moja ni kukosa kitu cha kuandika, hapa unapanga kuandika, lakini unaona hakuna unachoweza kuandikia. Unaweza kukaa ukitoa macho kwenye eneo lako la kuandika na usipate kabisa uandike nini.

Changamoto ya pili ni kutumia muda mwingi kwenye kuandika na hata kuahirisha unapokuwa umefika katikati. Ukishaachia kuandika katikati, inakuwa vigumu zaidi kuja kuanza tena kuandika.

Changamoto hizi mbili zimewakwamisha waandishi wengi na hivyo kuzitatua kutakuwezesha kupiga hatua. Muhimu zaidi ni kwamba, kama mwandishi, kila siku unapaswa kuandika, hivyo kukosa kitu cha kuandika, au kutumia muda mwingi kwenye uandishi, kunakuwa kikwazo kwa mafanikio yako.

Unatatuaje changamoto hizi mbili?

Changamoto hizi mbili zinaweza kutatuliwa na ukaweza kuwa na mawazo mengi ya kuandika na hata kuandika ndani ya muda mfupi. Zifuatazo ni hatua muhimu kufuata ili changamoto hizi zisikuzuie.

  1. Panga utakachokwenda kuandika kabla ya muda wa kuandika.

Usisubiri mpaka muda wa kuandika ndipo ufikirie uandike nini. Kwa kufanya hivyo utakosa uandike nini na kadiri utakavyokazana ndivyo unazidi kukosa.

Badala yake panga mapema unakwenda kuandika nini, kabla ya muda wa kuandika haujafika. Kama utaratibu wako ni kuandika asubuhi, basi jioni andaa kabisa utaandika nini siku inayofuata. Hili pia linakupa faida, maana unapokuwa na wazo la kuandikia, ukilala na kuamka nalo, unakuwa umelitafakari kwa kina zaidi.

  1. Fanya utafiti kabla ya muda wa kuandika.

Kinachowakwamisha waandishi wengi, na kuwapelekea kutumia muda mwingi ni kufanya utafiti. Siku hizi kufanya utafiti ni rahisi kupitia njia ya intaneti. Na hivyo wengi husubiri mpaka muda wa kuandika, hivyo wanaandika huku wakifanya utafiti kwenye intaneti. Hili linafanya zoezi la kuandika kuwa refu.

Unachopaswa kufanya ni kufanya utafiti wako kabla ya muda wa kuandika haujafika. Unachofanya ni unapokuwa na wazo la kuandika, lifanyie utafiti kabisa, chagua ni hoja gani unakwenda kuiongelea na vitu gani vitaitetea hoja yako. Unapofika wakati wa kuandika, kazi yako ni kuandika na siyo tena kufanya utafiti.

  1. Tenga muda maalumu wa kuandika, na andika, usifanye kingine.

Ukishajua unatumia muda gani kuandika makala yako, tenga muda maalumu ambao utakuwa unaandika kila siku. Na kila siku andika kwenye muda ule. Muda huo wa kuandika ulinde kabisa, usikubali uingiliwe na kelele yoyote. Na unapoanza kuandika, andika mpaka ualize, usiishie njiani. Kwa sababu unapoishia njiani, itakuchukua muda mrefu unapokuja kuanza tena kuandika.

Haya ni mambo matatu ambayo ukiweza kuyafanya, utaboresha uandishi wako, kila wakati utakuwa na kitu cha kuandika, utapunguza muda wa kuandika na pia utaacha kuahirisha uandishi wako na kuishia njiani. Yafanyie kazi kila siku na endelea kuboresha uandishi wako kila siku.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Sheria Muhimu Ya Kwenye Mtandao, Kwanza Kuwa Mtu Halisi.

Mitandao ya kijamii imerahisisha sana mawasiliano baina ya watu. Na pia imewezesha mawasiliano kwenye biashara kuwa rahisi zaidi. Hasa mfanyabiashara kumfikia mteja wake na kumpa kile ambacho anakitoa.

Pamoja na uzuri huu wa mitandao ya kijamii, changamoto bado ni kubwa. Watu wengi wamekuwa wakitumia mitandao hii kama njia rahisi kwao kutangaza biashara zao. Na chochote kinachochukuliwa kwa urahisi, huwa kinaleta matokeo ambayo siyo mazuri.

Watu wengi wamekuwa hawachukui muda na kujifunza matumizi sahihi ya mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii katika kukuza biashara zao. Badala yake wamekuwa wakitumia kwa mazoea. Wanafanya kile ambacho kila mtu anafanya, na hatimaye kuwa katikati ya kelele na wateja hawawaoni.

Katika kutafuta urahisi wa kutumia mitandao hii kwenye biashara, watu wamekuwa wanasahau eneo moja muhimu mno. Eneo hilo ni utu. Pamoja na yote, watu wanapenda kuwasiliana na watu kupitia mitandao ya kijamii.

Nikuulize swali, iwapo una rafiki yako, na kila wakati mnapokutana anakutangazia tu anachouza, utamchukuliaje? Utakuwa na shauku kweli ya kukutana naye mara kwa mara?

Lakini vipi kama una rafiki ambaye kila mkikutana mnapiga soga mbalimbali, mnataniana, mnabadilishana mawazo mazuri. Bila shaka unakuwa na shauku ya kukutana na rafiki huyo mara kwa mara.

Hivyo pia ndivyo ilivyo kwenye mitandao ya kijamii, japokuwa unaitumia kibiashara, lakini usiwe muda wote unatangaza tu. Badala yake tengeneza urafiki baina yako na wateja wako. Itumie mitandao yako kama sehemu ya kuwasiliana na wateja wako kwa mambo mbalimbali, na siyo biashara pekee.

Kwa kifupi kuwa mtu, na usiwe biashara. Tengeneza mahusiano baina ya mtu na mtu, wewe na wateja wako. Wateja wako watakuamini na watakuwa tayari kununua chochote unachouza, hasa pale unapowapatia kwa njia ambayo kinawasaidia kutatua matatizo yao.

Usiwe mtu wa kusukuma vitu wakati wote, nunua hichi, nunua kile na kadhalika, watu watachoka na wakiona jina lako tu wanapita haraka. Lakini unapokuwa mtu wa kujumuika, na kushirikisha mambo mbalimbali yenye faida kwa watu, watakuwa na hamasa ya kusikia kutoka kwako kila wakati.

Wakati wowote unapoweka kitu kwenye mitandao ya kijamii, jiulize je hapa nakuwa mtu au nasukuma tu kitu? Kama jibu siyo kuwa mtu, fanya marekebisho. Kazana kujenga mahusiano bora na wateja wako kupitia mawasiliano yako ya mitandao hii.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Hatua Tano (05) Za Uandishi Wa Makala Yenye Kuvutia Wasomaji Na Kuwafanya Kuchukua Hatua.

Habari za wakati huu mwandishi na mwanabloga?

Kama ambavyo wengi tunajua, uandishi ni sanaa, na kazi yoyote ya sanaa, huwa haina ukamilifu. Kila kazi ya sanaa inaweza iuboreshwa zaidi. 

Lakini pia hili halitupi sababu ya kufanya kazi mbovu ya uandishi. Hivyo basi, leo nimekuandalia makala nzuri kuhusu uandishi wa makala zenye mvuto na kuwapelekea watu kuchukua hatua.

Makala yoyote inapaswa kuwa na sehemu kuu tano, ambazo unapaswa kuziandika vizuri ili msomaji avutiwe kusoma, akuelewe na aweze kuchukua hatua.

Sehemu ya kwanza ni kichwa cha makala au tittle.

Hii ndiyo inamvutia msomaji mpaka afungue makala.

Hivyo kichwa kinapaswa kuwa na ushawishi, kiwe na ahadi kwa msomaji.

 Vichwa vyenye namba au idadi vinavutia zaidi.

Kwa mfano; 

1. mambo ya kuzingatia ili kufanikiwa,

Na 

2. mambo matano muhimu ya kuzingatia ili kufanikiwa,

Namba mbilo itafunguliwa zaidi.

Hivyo weka mvuto kwenye makala, na ikiwezekana, weka idadi au namba. Kama makala haihusu idadi basi usiweke, ila andika kichwa kinachovutia.
Sehemu ya pili ni ufunguzi wa makala au introduction.

Hapa unamkaribisha msomaji kwa kumtambulisha kwenye kile unachokwenda kumshirikisha. Hapa unapaswa kuweka maneno mazurim yanayoeleweka na kuvutia msomaji aendelee na makala. Pasipokuwa na maneno ya kuvutia, utawapotezea wengi bapo. Aya moja inatosha hapo.
Sehemu ya tatu ni makala yenyewe.

Hapa ndipo unapompa mtu kile ambacho umemwandalia. Makala inapaswa kuwa imejibu kile ambacho msomaji wako anataka kujua. Hii ina maana akimaliza kusoma makala, basi ana jibu fulani.

Makala ikiwa na orodha inavutia zaidi, kama tulivyoona kwenye kichwa.

Kama haina orodha ya namba basi pangilia vizuri maelezo yapangiliwe vizuri.
Sehemu ya nne ni hitimisho la makala au conclusion.

Hapa unamaliza kwa kumpa msomaji hitimisho, au yote aliyojifunza yana maana gani kwake.
Sehemu ya tano ni hatua ya kuchukua au CALL TO ACTION,

Hii ni hatua muhimu sana. Hapa unampa msomaji hatua ya ya kichwa baada ya kuwa amesoma makala yako.

Hii inaweza kuwa mwishoni mwa makala au hata katikati.

Unahitaji kumpa msomaji kitu cha kufanya,

Na yafuatayo ni mambo unayoweza kumshawishi msomaji afanye;

1. Kujiunga na email list yako, hivyo unahitaji kuwa na email list.

2. Kuweka maoni yake kuhusiana na ulichomshirikisha.

3. Kununua kitu unachouza.

4. Kuwashirikisha wengine nao wajifunze.

Kwa vyovyote vile, hakikisha kuna hatua msomaji unataka achukue akishasoma makala yako.

Zingatia msingi huu kwenye kila makala unayoandika, wasomaji wako wataweza kukufuatilia vizuri na watakuelewa na kuweza kuchukua hatua.

Kama una swali lolote au kuhitaji ufafanuzi juu ya uliyojifunza kwenye makala hii, weka maoni hapo chini.

Kupata blog nzuri na ya kitaalamu unayoweza kuitumiankutengeneza kipato, tuwasiliane kwa wasap namba 0717 396 253.

Karibu sana,

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani.