Kabla Wasomaji Wako Hawajakuamini, Unapaswa Mambo Haya Mawili Muhimu.

Kiu ya mwandishi yeyote yule, ni kuaminika na wasomaji wake. Na kama nilivyokuambia kwenye MASHABIKI WA UKWELI 1000, unaweza kutengeneza kipato cha kukutosha kuendesha maisha yako kupitia uandishi, iwapo utakuwa na wasomaji elfu moja ambao wanakuamini kweli. Hawa ni watu ambao watasoma kila kazi yako, watalipia kila unachouza, na watakuwa mstari wa mbele kukuunga mkono kwenye kila unachofanya.

Sasa swali kubwa ni je unawezaje kuwafanya wasomaji na wafuatiliaji wako wakuamini? Jibu la haraka ni kwamba huwezi kuwalazimisha kufanya hivyo, wala huwezi kuwashawishi wakuamini. Kuwaambia jamani niaminini mimi, nitakuwa na nyie siku zote, hakutawafanya wakuamini.

Wasomaji wako watachagua wao wenyewe kukuamini, kutokana na jinsi wewe unavyopeleka uandishi wako. Watachagua wao kukuamini au kutokukuamini kutokana na yale unayofanya, na siyo unayotaka wao wachukue kutoka kwako.

Yapo mambo mawili ambayo wasomaji wako wanayaona wazi kwenye kila kazi yako, na yanawafanya wakuamini au wasikuamini.

Jambo la kwanza ni imani yako wewe kwenye kile unachofanya.

Je unaamini kwenye kile unachofanya? Unaamini kwenye kile unachoandika? Au unaandika tu ili upate watu wa kusoma na baadaye upate fedha? Hichi ni kitu ambacho kila msomaji wako anaweza kukibeba wazi kutoka kwenye kazi zako. Yaani kwa msomaji wako kusoma ulichoandika, anajua wazi kama unaamini bila ya shaka kwenye kitu hicho, au umeandika tu kwa sababu unataka wajue.

Ni muhimu sana wewe kama mwandishi, kuamini bila ya shaka juu ya kile ambacho unaandika. Kuwa na uhakika ya kwamba yale unayomwambia msomaji wako ni kweli na yatamsaidia. Na pale msomaji anapokuomba ushauri au kuuliza swali, unamjibu ukiwa na uhakika huo.

Imani juu ya unachoandika unaweza kuijenga kwa njia mbili; kufanya utafiti wa kutosha na kujaribu kwenye maisha yako.

Unaweza kufanya utafiti wa kutosha kabla ya kuandika kitu, ili unapoandika uwe una taarifa za kutosha kabisa, ambazo ni sahihi na zinaweza kumsaidia mtu.

SOMA;Hatua Tano (05) Za Uandishi Wa Makala Yenye Kuvutia Wasomaji Na Kuwafanya Kuchukua Hatua.

Pia unaweza kujaribu vitu na kuona vinafanya kazi kwako binafsi kisha kuwashirikisha wasomaji wako. Au ukawashirikisha uzoefu ulionao wewe juu ya jambo unaloandikia.

Lazima uamini kwenye chochote unachoandika, chini ya hapo, msomaji hawezi kukuamini wewe.

Jambo la pili, umekuwepo kwa muda gani?

Watu wengi, wanataka waanze kuandika, na mara moja wapate wasomaji wengi na wanaowaamini. Mambo huwa hayafanyi kazi kwa njia hiyo. Unahitaji muda mpaka watu wakuamini kweli.

Kwa mfano mtu anaweza kukutana na andiko lako siku moja, akaona haya ni yale yale, hakuna jipya na asisome. Akakutana na andiko laki jingine tena, akalipuuza, akakutana na jingine tena, kumbuka hapo ni muda mrefu anakutana nayo, labda haya mwaka mzima. Siku moja anasema huyu mtu nakuta na maandiko yake karibu kila siku, hebu nisome nione ana nini. Na hapo anafungua na kusoma, anaona kuna kitu kinaweza kumsaidia. Hapo bado hajakuamini. Sasa anaendelea kusoma mara kwa mara, inaweza kumchukua mwaka mwingine. Kadiri anavyokwenda anaanza kujenga imani kwako kidogo kidogo, anaanza kukuelewa, anaanza kufanyia kazi yale anayojifunza, mara anaanza kupata matokeo mazuri. Hapo sasa ndiyo anakutafuta na kutaka mengi zaidi kutoka kwako.

Sasa unapoanza na kuishia njiani, unawapoteza watu wengi ambao walikuwa wanakufuatilia kimya kimya bila hata ya kukuambia. Ndiyo maana nimekuwa nakusisitiza sana, ANDIKA KILA SIKU. Hiyo ndiyo njia rahisi ya kuwatengeneza wasomaji wanaokuamini na wanaofuatilia kazi zako na kuwa tayari kununua kutoka kwako.

Wape wasomaji wako sababu ya kukuamini ili pia waweze kuwa wateja wako na MASHABIKI WAKO WA UKWELI, andika vitu ambavyo unaviamini kweli na ANDIKA KILA SIKU, bila ya kuacha.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

1 thought on “Kabla Wasomaji Wako Hawajakuamini, Unapaswa Mambo Haya Mawili Muhimu.

  1. Pingback: Vitu Viwili Muhimu Ambavyo Kila Mwandishi Anapaswa Kujua Kuhusu Wasomaji Wake. | MTAALAMU Network

Leave a Reply