Ukitaka Kuandika Vizuri, Ondokana Kwanza Na Huu Usumbufu.

Kitu kikubwa ambacho nimejifunza kwenye uandishi ni kwamba inachukua muda mpaka mtu uweze kujenga tabia yako ya uandishi, ambayo itakuwezesha kuandika kila siku na kutoa kazi nyingi. Na hii ni kama utaweka juhudi kubwa bila ya kukata tamaa pale unapokutana na vikwazo mbalimbali.

Uandishi, kama ilivyo kwenye mambo yote ya maisha, ni tabia. Kuweza kukaa chini na kuandika, ni tabia ambayo kila mtu anaweza kujitengenezea na ikamnufaisha sana. Lakini wengi sana wamekuwa wanashindwa kwenye hili, kwa sababu wanaruhusu usumbufu mbalimbali kuingilia tabia hiyo.

Kwa mfano, iwapo unaandika huku kuna watu wanakusemesha, huwezi kutuliza akili yako na kutoa kitu kizuri. Iwapo unaandika huku simu zinaingia, ujumbe unatumwa, hutaweza kuweka akili yako sehemu moja. Kama unaandika huku unachungulia mitandao ya kijamii, hutaenda muda mrefu kabla hujaahirisha na kusema nitaandika baadaye.

Unapofika wakati wa kuandika, chochote kile utakachofanya nje na kuandika ni usumbufu. Na usumbufu huo una gharama kubwa kwa sababu akili haipendi kuteseka, hivyo unapoisukuma itoe vitu vizuri, inakimbilia kuangalia wapi kuna usumbufu ili uipumzishe.

Ndiyo maana ni muhimu sana kama unataka kujijengea tabia ya uandishi, uhakikishe huna usumbufu wa aina yoyote ile unapoandika. Uwe sehemu tulivu ambayo hakuna mwingiliano mkubwa wa watu, usiwe kwenye mitandao ya kijamii na simu yako isiwe na kelele ya kukutoa kwenye uandishi.

Na hii ndiyo sababu kubwa nashauri sana uandike asubuhi na mapema kabla dunia haijaamka, hapo hakuna watu wengi wanaokupigia simu. Au uandike usiku sana ambapo wengine tayari wameshalala. Katika muda wa aina hiyo, ni mara chache sana utapata usumbufu.

Unaweza kuchagua kuandika muda wowote wa siku yako, lakini unahitaji uwe na nidhamu kubwa sana. Hivyo kama ndiyo unaanza kujenga tabia hii, ni vyema ukaanza kwa kutumia muda ambao hakuna usumbufu, ukishaweza kuutawala vizuri hapo unaweza kuchagua kuandika muda wowote na popote. Lakini usijaribu hilo ukiwa bado hujajenga tabia ya uandishi, utaishia njiani..

SOMA;Usijisumbue Kuandika Kitabu Kama Huna Kitu Hichi Kimoja Muhimu Sana. Soma Hapa Kukijua.

Kujenga tabia ya uandishi na kuweza kuandika kila siku, epuka usumbufu ambao unaitoa akili yako kwenye kufikiri kwa kina ili uweze kuandika vizuri.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

1 thought on “Ukitaka Kuandika Vizuri, Ondokana Kwanza Na Huu Usumbufu.

  1. Pingback: Unawezaje Kuandika Pale Unapokuwa Hujisikii Kuandika? | MTAALAMU Network

Leave a Reply