Monthly Archives: July 2017

Vitu Viwili Muhimu Ambavyo Kila Mwandishi Anapaswa Kujua Kuhusu Wasomaji Wake.

Pamoja na kwamba wewe mwandishi unapaswa kuandika kutokana na ujuzi wako, uzoefu na mapenzi yako, unapaswa kukumbuka kwamba hujiandikii wewe mwenyewe. Unawaandikia watu wengine, ambao ni wasomaji wako. Hivyo unapoandika, lazima pia uwaangalie wasomaji wako ili kuweza kuwaandikia kitu ambacho kinawasaidia kutoka pale walipo sasa na kwenda mbele zaidi.

Katika kuwajali wasomaji wako, yapo mambo mawili muhimu sana ambayo wewe kama mwandishi, lazima uyajue kuhusu msomaji wako. Katika makala yetu hii ya leo, tutakwenda kujifunza mambo hayo mawili kwa kina.

JAMBO LA KWANZA; CHANGAMOTO GANI KUBWA WANAYOPITIA KWA SASA?

Watu wana changamoto, watu wana matatizo, watu wanakwama kwenye mambo mbalimbali wanayofanya kwenye maisha yao.

Ni muhimu wewe ujue changamoto kubwa ambayo wasomaji wako wanaipitia kwa sasa, inayohusiana na lile eneo unaloandikia wewe.

Jua ni nini wanahangaika nacho sasa, wapi ambapo wamekwama katika mipango yao na malengo yao.

Kwa kujua hili, utaweza kuwaandalia makala zinazowawezesha kuondokana na changamoto hiyo na pia kupiga hatua. Makala unazowaandikia zitaendana nao na hivyo kukufuatilia kwa karibu.

Ukishajua changamoto wanazopitia wasomaji wako, unawaandalia makala zenye hatua za kuchukua ili kutoka pale walipo sasa na kuweza kufika kwenye malengo waliyonayo.

Hili ni jambo muhimu sana unapaswa kulijua, na mara zote hakikisha unajua na unafanyia kazi, ili uweze kwenda vizuri na wasomaji wako.

JAMBO LA PILI; NINI MATARAJIO NA MATUMAINI YAO KWA SIKU ZIJAZO?

Kitu pekee kinafanya maisha yaweze kwenda licha ya watu kupitia matatizo na changamoto, ni matumaini kwamba kesho itakuwa bora kuliko leo. Matumaini hayo yanawawezesha kuendelea kuweka juhudi bila ya kukata tamaa, licha ya mambo kuwa magumu.

SOMA;Kabla Wasomaji Wako Hawajakuamini, Unapaswa Mambo Haya Mawili Muhimu.

Hili ni muhimu sana wewe mwandishi kulijua kuhusu wasomaji wako kuhusiana na eneo unaloandikia. Jua matarajio na matumaini waliyonayo kwa siku zijazo. Jua nini wanategemea na wapi wanajiona kwa siku zinazokuja.

Kwa kujua matarajio na matumaini haya, utaweza kuwasaidia kuyafikia kwa kuwapa mbinu na njia bora za kufuata ili kufika pale ambapo wanataka kufika. Kwa sababu wakati mwingine watu wanajua wanakotaka kufika, ila hawajui wanafikaje hapo. Wewe ukiwasaidia namna ya kufika, watakuwa wafuasi wako wakati wote.

Swali ni je unajuaje hayo mawili kuhusu wasomaji wako?

Jibu ni hakuna muujiza wala utabiri, badala yake unawauliza. Waulize wasomaji wako maswali hayo mawili, ili uweze kujua kwa hakika wapi wamekwama na wapi wanaangalia.

Unaweza kuwauliza kwa kuandika makala kwenye blog yako kisha ukawaomba wawele maoni yao kuhusiana na maeneo hayo mawili. Pia unaweza kuwauliza kwa kuwatumia email kwenye email list yako na kuomba wakujibu maswali hayo.

Zipo njia nyingine pia za kuwauliza, kama kutumia mitandao ya kijamii, unaweza kuwauliza na wakakujibu kupitia mitandao hiyo. Pia ipo njia bora zaidi ya kufanya hili ambapo ni kuandaa mfumo wa utafiti (survey) kwa kuwa na fomu yenye maswali hayo na sehemu ya wasomaji kujibu. Unaweza kufanya hilo kwa kutumia google drive au programu kama survey monkey. Unaandaa maswali yako na kuwatumia wasomaji wako link na wao kufungua na kuyajibu.

Fanyia kazi mambo haya mawili muhimu sana ili uweze kuwa karibu na wasomaji wako, kwa kuweza kuwasaidia kupiga hatua zaidi kwenye maisha yao.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

SIRI MUHIMU YA UANDISHI; Tengeneza Sauti Yako Na Mtiririko Wako Wa Uandishi.

Nimekuwa natania kwamba sababu ya wanamuziki wengi kushindwa kuwafikia wanamuziki wakubwa, ni wao kuimba kwa mtindo wa wanamuziki hao wakubwa. Kwa mfano, Diamond ni mwanamuziki mkubwa, sasa nyuma yake wapo vijana wengi ambao nao wanapenda kuwa kama Diamond, ila kosa kubwa wanalofanya, ni kuimba kama anavyoimba Daimond. Ni kosa kubwa sana wanalofanya kwa sababu kama mtu anaweza kumsikiliza Diamond, kwa nini aje kukusikiliza wewe? Lazima uwe na kitu cha tofauti, ambacho mtu hawezi kukipata popote.

Kadhalika hivi ndivyo ilivyo kwenye uandishi. Kila mwandishi ana mwandishi ambaye anamhamasisha. Yupo mwandishi ambaye utasoma kila analoandika, utanunua kila kitabu chake, utahudhuria kila mafunzo anayotoa. Sasa hilo linapelekea wewe kuandika kama yeye, kufanya vile anavyofanya yeye.

Hii inakuwa hatari kwa waandishi wapya na wachanga, kwa sababu kama mtu anaweza kusoma unachoandika kwa mwandishi mwingine ambaye amekutangulia, unafikiri kwa nini aje kusoma kwako?

Kila mwandishi anahitaji kuwa na sauti yake ya kipee, kuwa na aina yako ya uandishi, ambayo wasomaji wako wataielewa kwako, na hawawezi kuipata sehemu nyingine.

Na aina yako hiyo haiwezi kuigwa na mwingine, kwa sababu umeitengeneza mwenyewe, waliokutangulia hawawezi kuiiga kwa sababu tayari wana aina zao, na wanaokuja wanaweza kukuiga lakini wewe tayari umeshatangulia.

SOMA;Jinsi Ya Kutumia Lugha Ya Kiswahili Kwenye Uandishi Na Uhariri Wa Makala.

Tengeneza sauti yako ya uandishi, tengeneza mtiririko wako wa uandishi, fikia hatua kwamba, msomaji akisoma andiko sehemu yoyote, hata kama halina jina lako, basi ajue ni wewe, kwa sababu anajua namna unavyoandika.

Na hili siyo zoezi gumu, kama utaacha kuigiza. Usiigize kwenye uandishi, andika kile unachojua, kile unachoamini kweli. Andika kila ambacho upo tayari kukisimamia na kukitetea, kwa namna yoyote ile. Andika kwa namna unavyotaka wengine wachukue hatua.

Usitake kuandika kumfurahisha yeyote, kwa sababu kumbuka wanaokuelewa watakuelewa, na wasiokuelewa, nikimaanisha wasioendana na unachoandika, hawatakubaliana na wewe, hata kama utaandika kwa kubembeleza kiasi gani.

Tengeneza sauti yako rafiki, tengeneza mtiririko wako wa uandishi, na utatengeneza wasomaji wanaoenda na wewe vizuri. Kuiga ni kujipeleka kwenye njia ya kupotea, hakuna anayehangaika na kopi wakati orijino ipo.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Unawezaje Kuandika Pale Unapokuwa Hujisikii Kuandika?

Mwandishi mmoja mashuhuri, aliulizwa tofauti ya mwandishi aliyebobea na mwandishi mchanga. Na bila ya kusita alisema mwandishi mchanga anaandika pale anapojisikia, ila mwandishi aliyebobea anaandika wakati wote, iwe anajisikia au hajisikii.

Nimekuwa nakusisitiza mara nyingi ya kwamba, kuweza kufikisha uandishi wako kwenye ngazi kubwa ya kuweza kupelekea kulipwa, kwanza uandike kila siku, KILA SIKU.

Ila sasa changamoto inakuja unawezaje kuandika kila siku iwapo kuna siku hujisikii kuandika?
Hapa sina muujiza wowote wa kukupa, zaidi ya kukuambia unahitaji kujijengea nidhamu ya kuandika kila siku. Inabidi upange ratiba yako ya uandishi, muda unaoandika na kila siku andika, ndani ya muda ule.

Ni vyema muda huo ukawa asubuhi, kabla hujafanya jambo jingine lolote. Amka kaa chini na andika. Iwapo hujisikii kuandika, kaa na andika. Kaa pale mpaka uandike kitu.

Usikimbilie kujisumbua, maana wengi wanapokuwa hawajisikii kuandika, husema labda wachungulie facebook kuna nini, au instagram, au wasap. Kote huko ni usumbufu na kunazidi kukuondoa kwenye kuandika.

SOMA;Ukitaka Kuandika Vizuri, Ondokana Kwanza Na Huu Usumbufu.

Dawa ya kutokujisikia kuandika ni kuandika. Hivyo tu. Kaa chini na andika.

Andika chochote, anza kuandika, bila ya kujihukumu au kujikosoa. Anza kuandika neno moja na nenda neno jingine linalofuatia. Kaa hapo mpaka uandike kitu chenye kuweza kumsaidia mtu. Halafu ukumbuke una uwezo wa kufuta chochote ulichoandika, hivyo kama mwanzo ulianza kwa kuandika kitu cha hovyo, usiwe na wasi wasi, unaweza kufuta wakati wowote.

Kuwa mwandishi mbobezi, andika siyo kwa sababu unajisikia kuandika, ila andika kwa sababu unataka kuandika, ndiyo jukumu lako, ndiyo wajibu wako, kila siku.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Ukitaka Kuandika Vizuri, Ondokana Kwanza Na Huu Usumbufu.

Kitu kikubwa ambacho nimejifunza kwenye uandishi ni kwamba inachukua muda mpaka mtu uweze kujenga tabia yako ya uandishi, ambayo itakuwezesha kuandika kila siku na kutoa kazi nyingi. Na hii ni kama utaweka juhudi kubwa bila ya kukata tamaa pale unapokutana na vikwazo mbalimbali.

Uandishi, kama ilivyo kwenye mambo yote ya maisha, ni tabia. Kuweza kukaa chini na kuandika, ni tabia ambayo kila mtu anaweza kujitengenezea na ikamnufaisha sana. Lakini wengi sana wamekuwa wanashindwa kwenye hili, kwa sababu wanaruhusu usumbufu mbalimbali kuingilia tabia hiyo.

Kwa mfano, iwapo unaandika huku kuna watu wanakusemesha, huwezi kutuliza akili yako na kutoa kitu kizuri. Iwapo unaandika huku simu zinaingia, ujumbe unatumwa, hutaweza kuweka akili yako sehemu moja. Kama unaandika huku unachungulia mitandao ya kijamii, hutaenda muda mrefu kabla hujaahirisha na kusema nitaandika baadaye.

Unapofika wakati wa kuandika, chochote kile utakachofanya nje na kuandika ni usumbufu. Na usumbufu huo una gharama kubwa kwa sababu akili haipendi kuteseka, hivyo unapoisukuma itoe vitu vizuri, inakimbilia kuangalia wapi kuna usumbufu ili uipumzishe.

Ndiyo maana ni muhimu sana kama unataka kujijengea tabia ya uandishi, uhakikishe huna usumbufu wa aina yoyote ile unapoandika. Uwe sehemu tulivu ambayo hakuna mwingiliano mkubwa wa watu, usiwe kwenye mitandao ya kijamii na simu yako isiwe na kelele ya kukutoa kwenye uandishi.

Na hii ndiyo sababu kubwa nashauri sana uandike asubuhi na mapema kabla dunia haijaamka, hapo hakuna watu wengi wanaokupigia simu. Au uandike usiku sana ambapo wengine tayari wameshalala. Katika muda wa aina hiyo, ni mara chache sana utapata usumbufu.

Unaweza kuchagua kuandika muda wowote wa siku yako, lakini unahitaji uwe na nidhamu kubwa sana. Hivyo kama ndiyo unaanza kujenga tabia hii, ni vyema ukaanza kwa kutumia muda ambao hakuna usumbufu, ukishaweza kuutawala vizuri hapo unaweza kuchagua kuandika muda wowote na popote. Lakini usijaribu hilo ukiwa bado hujajenga tabia ya uandishi, utaishia njiani..

SOMA;Usijisumbue Kuandika Kitabu Kama Huna Kitu Hichi Kimoja Muhimu Sana. Soma Hapa Kukijua.

Kujenga tabia ya uandishi na kuweza kuandika kila siku, epuka usumbufu ambao unaitoa akili yako kwenye kufikiri kwa kina ili uweze kuandika vizuri.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Usijisumbue Kuandika Kitabu Kama Huna Kitu Hichi Kimoja Muhimu Sana. Soma Hapa Kukijua.

Maendeleo yanayotokea kwenye mtandao wa intaneti yamebadili kwa kiasi kikubwa sana uandishi na uchapaji wa vitabu. Siku za nyuma ilikuwa unaandaa pendekezo la kuandika kitabu, unatuma kwa wachapaji, wanachambua kama ni kitabu kitakachofaa kuuza, wanakubali, kama hakifai wanakataa mapendekezo hayo.

Hali hiyo ilipelekea mapendekezo ya wengi ya kuandika vitabu kukataliwa. Mtu aliweza kutuma mapendekezo kwa wachapaji hata kumi na wote wakakataa.

Sasa hivi sheria za mchezo zimebadilishwa. Siyo lazima tena kutuma maombi kwa wachapaji ili kuweza kuandika na kuchapishiwa kitabu. Sasa hivi mtu unaweza kuchagua kuandika kitabu chako mwenyewe, kukichapa mwenyewe na hata kukiuza mwenyewe.

Urahisi huu kwenye kuandika na kuchapa vitabu bila ya kusubiri mtu akukubali, umepelekea watu wengi kuandika vitabu.

Hapo sasa ndipo wengi wanakutana na ukweli mchungu, baada ya kuweka muda wao kuandika kitabu, kukichapa, lakini wanakosa wateja wa kutosha kununua vitabu vyao. Wakati mtu anaandika anakuwa na matumaini makubwa kwamba kitabu chake ni kizuri, kitawasaidia wengi na pia kitamwingizia kipato. Lakini akishamaliza kuandika kitabu na kukichapa, haoni watu wakikishambulia kama alivyofikiri.

Pia kuna uwezekano wa kuuza kitabu katika nakala tete, bila hata ya kukichapa. Hapo pia wengi wamekuwa hawapati wateja wa kutosha kununua vitabu ambavyo wameviandika.

Ili kukusaidia usikutane na hali hii ya kukatisha tamaa, leo nimekuandalia makala ya kitu gani ufanye kabla hujaandika kitabu. Yaani kama una wazo la kuandika kitabu, ni vizuri. Lakini kabla hujaandika au kutoa kitabu chako, kwanza lipo jambo la msingi kuzingatia.

Kitu unachopaswa kuzingatia kabla hujatoa kitabu ni KUWA NA WAFUASI. Lazima kwanza uwe na watu ambao wanakujua, na siyo kukujua kama ndugu au jamaa, bali wanaokujua kupitia kazi zako za uandishi. Lazima uwe na wafuasi, wasomaji ambao wanakufuatilia.

Wafuasi hawa unawatengeneza kupitia blogu yako, kwa kuanza kuandika makala zinazoendana na kile ambacho unataka kukiandikia kitabu. Baada ya kuwa na wafuatiliaji wa kutosha kupitia blogu yako, hapo ndipo unapoweza kuandika kitabu.

Kwa kufanya hivi, utakuwa na wateja wa kuanza kuwauzia vitabu vyako, na hawa wataweza kuwashawishi wengine kuja kununua na kusoma kazi zako zaidi.

Kwa sasa nchi kama Marekani, ili mchapaji akubali kuchapa kitabu cha mwandishi, kwanza amuoneshe idadi ya watu wanaomfuatilia. Na kipimo kizuri wanachotumia ni email list, ile idadi ya watu ambao wamejiandikisha kupokea email kutoka kwako.

Tumia blogu yako, mitandao ya kijamii na email list kutengeneza wasomaji wako, ambao wanakujua na kufuatilia kazi zako. Ukishakuwa na wasomaji hawa, unaweza kuandika kitabu na kukiuza kwa urahisi zaidi. Usikimbilie kuandika kitabu kabla hujawa na wasomaji, utakata tamaa na kuona hakuna wasomaji. Wasomaji wapo wengi, ila ni mpaka uwatengeneze wewe mwenyewe kwanza.

Kama unapenda kuandika lakini bado hujajua utumieje mtandao wa intaneti kukuza uandishi wako, tuwasiliane wasap 0717396253. Karibu sana.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Acha Kukimbizana Na Vitu Vipya, Ijue Misingi Na Ifanyie Kazi.

Upo ugonjwa wa kukimbizana na kila kitu kipya ambacho kinatoka. Kutaka kujaribu kila mtandao mpya wa kijamii unaokuja, kutaka kujaribu mbinu mpya za kutengeneza kipato kwenye mtandao ambazo watu wanakuambia. Watu wengi wamekuwa wakikimbizana na vitu hivyo vipya, na kupoteza muda wao mwingi na hivyo kujizuia kufanya makubwa.

Leo nataka nikupe siri moja kubwa, kabla hujaana kukimbizana na mambo mapya unayoyaona kila mahali, ijue kwanza misingi na hakikisha umeifanyia kazi. Kwa sababu huwa tunapenda kufanya mambo rahisi ambayo hayana matokeo makubwa kwetu. Na kuepuka mambo ya msingi ambayo ni magumu ila yana matokeo makubwa kwetu.

Mambo ya msingi kabisa katika kutengeneza kipato kwenye mtandao ni kuandika, kuwafikia wasomaji na kutatua changamoto zao. fanya ufanyavyo, lazima uandike au urekodi kile ambacho unafundisha. Hivyo badala ya kutafuta njia za kukwepa hilo, ni vyema ukalifanya kwa muda wake ndipo uendelee na mambo mengine. Pia kuwafikia wasomaji na kutatua changamoto zao ni jambo la msingi kabisa kwako kufanya.

Ukishafanya hayo ndiyo unaweza kuendelea na mengine yasiyo ya msingi. Kutembelea mitandao ya kijamii, kujaribu mitandao mipya ya kijamii, kubadilisha picha kwenye mitandao ya kijamii, kupokea na kupiga simu, yote hayo yanapaswa kufanyika baada ya kuwa umemaliza kufanya yale ya msingi.

SOMA;Zingatia Misingi Hii Mitatu(03) Ya Kutengeneza Kipato Kwenye Mtandao Wa Intaneti.

Ichukulie kazi yako ya uandishi kwa umakini wa hali ya juu. Jiwekee utaratibu wa kuhakikisha yale ya msingi yanafanyika, kabla yale ambayo siyo ya msingi hayajaingilia siku yako.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Njia Ya Uhakika Ya Kujenga Jina Lako Kwenye Mtandao; TAFUTA UTAKACHOSIMAMIA.

Moja ya matumizi mazuri ya mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii, ni kujenga jina lako kupitia kazi unazofanya au biashara zako. Mitandao ya kijamii ni uwakilishi wako kwa watu ambao hawajawahi kukutana na wewe. Mtu anapotembelea mitandao yako ya kijamii, au blog yako, kwa kupitia yale unayoandika, anajijengea picha wewe ni mtu wa aina gani, hata kama hajawahi kukutana na wewe.

Hii ni dhana muhimu sana tunayopaswa kuielewa na kuitumia vizuri kwenye kujijengea jina lako, kama unavyotaka liwe. Yaani vile ambavyo unataka watu wakuchukulie, unaweza kutumia mitandao ya kijamii kutengeneza hilo.

Hapa unachopaswa kufanya, ni kuchagua kitu kimoja au vichache ambavyo utavisimamia. Na ninaposema kuvisimamia namaanisha kweli unavisimamia, unaamini katika vitu hivyo kiasi kwamba huoni aibu kuitangazia dunia juu ya hilo. Chochote unachoandika kwenye mitandao hii, kinakuwa kinaendana na kile ambacho unasimamia.

Mtu anapokutana na kazi zako, kupitia mtandao wa intaneti, anajionea wazi kabisa unasimama upande gani. Kadiri msimamo wako unavyokuwa wazi, ndivyo watu wanavyoweza kukutegemea linapokuja swala linalohusiana na kile unachosimamia.

Lakini pia kusimamia kitu kunakuja na changamoto zake. Na moja ya changamoto hizo ni kukosolewa na kupingwa na wale ambao wanaamini tofauti na unachosimamia. Chochote kile utakachosimamia, hata kama kingekuwa kizuri kiasi gani, wapo watu ambao watakupinga, na kukukosoa. Na kadiri unavyokuwa na msimamo mkali, ndivyo wa kukukosoa na kukupinga wanavyozidi kuwa wengi. Hivyo jiandae kwa hilo na usitetereke.

Jua unaposimamia jambo lolote, wapo watu wanaokubaliana na wewe na wanakufuatilia, hata kama hawakuambii chochote. Hivyo usikate tamaa unapokutana na changamoto yoyote kwenye lile unalosimamia.

Huwezi kusimamia kila kitu, huwezi kukubali kila kitu. Chagua jambo moja au machache ambayo unayaamini kweli, kisha yasimamie kwa uhakika. Kila ujumbe unaotoa, uwe unaunga mkono kile ambacho unasimamia. Jiandae kwa kupingwa ila usikubali mtu akusababishe uache kile unachosimamia.

SOMA;Sheria Muhimu Ya Kwenye Mtandao, Kwanza Kuwa Mtu Halisi.

Unaposimamia kitu hasa, jina lako linahusishwa na kitu kile. Hivyo mtu anapokuwa na jambo lolote linalohusiana na kitu kile, moja kwa moja anaambiwa aje kwako. Hata wanaokupinga, watakuongezea watu kwa sababu lazima wakutumie wewe kama mfano wa watu wenye msimamo ambao wao hawakubaliani nao.

Muhimu sana; unachosimamia kiwe kitu sahihi na chenye manufaa kwako na wanaokuzunguka pia. Usisimamie kitu ambacho unakipenda lakini kina madhara kwako au kwa wengine.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Jinsi Ya Kuendelea Kuwa Na Makala Zinazoenda Hewani Kila Siku Hata Kama Huna Mtandao Kila Siku.

Moja ya hitaji muhimu la kuweza kukuza blog yako kupata wasomaji wanaokuamini na kukufuatilia, ni kuwa na makala mpya kila siku. Msomaji anajijengea mazoea kwamba kila siku akija kwenye blog yako, kipo kitu kipya ambacho anajifunza. Lakini msomaji anapokuja na kukuta hakuna makala mpya, akirudi tena na hali ikawa hivyo, anaacha kuitegemea blog yako, kwa sababu hana uhakika ni wakati gani kutakuwa na makala mpya.

Pamoja na umuhimu huo wa kuwa na makala kila siku kwenye blog, maisha hayajanyooka kama mstari. Siyo kila wakati unakuwa kwenye maeneo rafiki kwako kuweza kuhakikisha makala inaenda hewani kila siku.

Wakati mwingine unaweza kuwa umesafiri eneo ambalo hakuna mtandao wa intaneti na hivyo kushindwa kupost makala, hata kama unaweza kuandika. Wakati mwingine unaweza kusafiri eneo ambalo huwezi kuandika kila siku, labda ni umeme hakuna, au mazingira hayakupi nafasi ya kuweza kuandika kila siku.

Je unafanya nini kwenye nyakati kama hizo ili kuhakikisha wasomaji wako wanaendelea kupata makala mpya kila siku?

Shukrani ziende kwenye huduma zote za blogu, iwe ni BLOGGER au WORDPRESS, kuna kitu kinaitwa SCHEDULE. Hapo unaweza kupanga makala ziende hewani muda ambao wewe mwenyewe hutakuwa hewani. Unachofanya ni kuandika makala, kuiweka kwenye blog, lakini badala ya ku PUBLISH moja kwa moja unaenda kwenye ku SCHEDULE. Hapo unachagua makala iende hewani siku gani (tarehe) ana saa ngapi. Hapo unaweza kuchagua siku, mwezi, mwaka na saa na dakika ambayo unataka makala hiyo iende hewani. Ukishakamilisha hilo, wewe unaendelea na mambo yako, hivyo muda ukifikia, makala itaenda hewani, hata kama wewe haupo hewani.

Hivyo kama unasafiri kwa wiki moja, na unaona hutaweza kuandika kipindi hicho, jipange kabla ya safari uandike makala zote za wiki, uziweke kwenye blog kwa kuschedule kwa wiki nzima. Makala zitaendelea kwenda hewani na wasomaji kuendelea kupata maarifa.

Kama unasafiri eneo ambalo halina umeme, unaweza pia kuandika makala zako kabla ya safari na kuziweka kwenye blog kwa kuschedule. Kama unasafiri kwa muda mrefu kwenye eneo ambalo halina umeme, unaweza kujipa utaratibu kwa kutafuta eneo lenye umeme kila wiki na kuandika na kupost makala zako za wiki nzima kwa kuschedule.

SOMA;Kabla Hujafikiria Kulipwa Kwenye Mtandao, Andika Kwanza Makala 100.

Iwapo kuandika na kuweka makala hizo kwa wakati mmoja ni nyingi, basi punguza idadi ya makala, lakini usiache kabisa kupost. Kama safari yako au kazi yako ni ya muda mrefu, basi unaweza kubadili, badala ya kuweka makala zinazoenda hewani kila siku, ukaweka makala zinazoenda hewani kila baada ya siku moja. Yaani leo ikienda, kesho haiendi, au unaweza kupanga makala ziende hewani jumatatu, jumatano na ijumaa. Kwa njia hii, wasomaji wako hawatakusahau kabisa.

Usikubali changamoto yoyote ikuzuie wewe kuwawekea wasomaji wako makala kila siku. Jipange kulingana na hali unayopitia na hakikisha wasomaji wako wanaendelea kupata maarifa kupitia blog yako. Umeshafanya kazi kubwa kuwapata, usikubali kuwapoteza kirahisi.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Sababu Nyingine Kwa Nini Unapaswa Kuzalisha Kazi Nyingi Na Bora Zaidi.

Mtandao wa intaneti umefanya jambo moja kubwa sana, ambalo halijawahi kutokea tangu kuwepo kwa dunia. Jambo hilo ni kumwezesha kila mtu kuwa na sauti, sasa hivi kila mtu anaweza kutoa maoni yake wakati wowote anapojisikia kufanya hivyo, na popote pale alipo.

Mtandao wa intaneti umeleta usawa mkubwa kwenye mawasiliano na hata biashara. Kila mtu mwenye kitu anaweza kufanya, akiwa popote pale.

Hii ina maana kwamba, watu wanaandika vitu vingi, kuanzia makala, vitabu na hata jumbe fupi fupi zinazowekwa kwenye mtandao.

Kutokana na wingi huu, ni kama kumekuwa na kelele nyingi kwenye mtandao wa intaneti. Ni kama kila anayeshiriki anapiga kelele, nisome na mimi, nipo hapa pia.

Kitu pekee kinachoweza kukusimamisha kwenye kelele hizi na watu wakakuona, ni wingi na ubora wa kazi zako.

Wingi kwa maana kwamba unahitaji kutoa kazi nyingi uwezavyo. Andika mara nyingi mno, kama ni makala ziwe nyingi, kama vitabu viwe vingi pia. Hii ina maana kila siku, lazima watu wakusikie, lazima watu wapate kazi yako. Na hii inawafanya wakukumbuke na kuendelea kuwa na wewe. Lakini kama utakuwa unatoa kazi chache, hata kama zinakuwa bora kiasi gani, watu watakusahau, kwa sababu kelele zinazowasumbua ni nyingi mno.

SOMA;Eneo Moja Muhimu La Kufanyia Kazi Kila Siku Ili Kutengeneza Kipato Kwenye Intaneti.

Ubora wa kazi ni muhimu pia, kwa sababu kama unazalisha kazi nyingi lakini za hovyo, watu watakupuuza, hawatajisumbua kwa sababu wanajua hakuna kizuri unachotoa. Sasa hapa kwenye ubora unapaswa kuwa makini, maana wengi hukosea kwa kufikiri ubora ni mpaka ukubalike na kila mtu, asiwepo hata mmoja wa kukupinga. Ubora tunaouzungumzia hapa ni kuweza kuwasaidia watu ambao wana changamoto au matatizo fulani, na maisha yao yakawa bora.

Kuweza kufikia hilo la wingi na ubora, nimekuwa nakusisitiza mambo mawili muhimu.

Jambo la kwanza, andika kila siku, kila siku andika, iwe ni makala au vitabu. Hivyo ukiandika kila siku, utaweza kutoa makala kila siku. Na wakati huo huo, kila mwezi unaweza ukatoa kitabu pia.

Jambo la pili, chagua kundi la watu ambao utawatatulia matatizo na changamoto walizonazo. Waandalie maarifa na taarifa ambazo zitawawezesha kuwa na maisha bora.

Fanyia kazi hayo mawili kila siku, ukiangalia miaka 10 ijayo mbele, usisumbuliwe na kitu kingine chochote, na utaweza kufanya makubwa.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Jambo Pekee La Kiungwana Unaloweza Kufanya Kwenye Mtandao Wa Intaneti Ni Hili, Na Ukalipwa Pia.

Siku za nyuma, nilikuwa nasema kwamba huku Afrika, tumebaka teknolojia, hasa hii ya mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii. Nilikuwa nasema hivyo kwa sababu watu wengi walikuwa wanatumia mitandao hii bila ya kuwa na uelewa sahihi. Mtu anapata simu yake, anasaidiwa kujiunga na mitandao hii na kuanza kuitumia kama anajua vile. Hakukuwa na elimu yoyote ya matumizi sahihi.

Sasa ambacho kilikuwa kinatokea, ni watu kutukanana, kuzodoana, kukasirishana na hata kuvumishiana mambo yasiyo ya kweli. Hapo bado watu wengi walikuwa wakipoteza muda mwingi kwenye mitandao hii.

Nina hakika mpaka sasa wapo ambao wanaendelea na ubakaji huo wa mtandao, kwa kuutumia kwa hasara kwao na wale wanaowazunguka. Mtandao huu ni kitu kizuri lakini watu wanatumia kwa njia mbaya.

Sasa kwenye upande wa kutengeneza kipato, watu wanaendelea kubaka mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii. Wanakazana kufanya vitu bila ya kujua, na hilo linawapelekea kuchoka na kipato hawatengenezi. Wanakazana kuuza vitu kwenye mitandao, kutangaza sana, lakini hawapati wanunuaji wa kutosha.

Leo nakwenda kukuambia jambo moja la kiungwana ambalo unaweza kufanya kwenye mtandao wa intaneti, na likapelekea wewe kulipwa pia.

Jambo hilo ni kuwapa watu suluhisho la matatizo wanayopitia. Hili ni jambo la kiungwana sana, ambalo litawanufaisha watu, na kukunufaisha wewe pia.

Iko hivi, watu wana matatizo na changamoto wanazopitia kwenye maisha yao. Na wewe huenda ulishapitia matatizo kama hayo na ukaweza kutatua. Au una utaalamu unaoweza kuwasaidia watu hao. Au una uzoefu, kupitia wengine kwenye matatizo na changamoto hizo. Hivyo unachofanya ni wewe kuwashirikisha kile ambacho kinaweza kuwasaidia kutoka pale walipo.

Huhitaji elimu kubwa, huhitaji kuwa na fedha na wala huhitaji uwe na muda mwingi, ni wewe kuchagua kitu gani unaweza kuwasaidia watu kupata suluhisho, na kufanya hivyo.

SOMA;Sababu Moja Kwa Nini Wewe Unapaswa Kuwa Na Blog, Hata Kama Hutaki Kipato Mtandaoni (NA ZAWADI YA KITABU BURE.)

Unajuaje watu gani unaweza kuwasaidia?

Kama nilivyoeleza hapo juu, angalia mambo ambayo yanawasumbua wengine, lakini kwako ni rahisi. Angalia vitu ambavyo unajua wewe, lakini wengine hawajui. Halafu anza kuwasaidia watu kujua kile unachojua, kuwashirikisha njia bora za kuwatoa pale walipo.

Unawasaidia kwa njia gani?

Kwa kutumia akaunti zako za mitandao ya kijamii unayotumia, facebook, instagram, twitter, wasap na kadhalika.

Kwa kuwa na blog ambayo watu wanafika kujifunza zaidi, ambapo unaweka makala nzuri zaidi na huduma zako nyingine.

Na kwa kuwa na mfumo wa barua pepe (email list) ambapo unawasiliana na wasomaji wako na kuwapa zaidi lile suluhisho unalowaandalia.

Vitu hivyo vitatu lazima uwe navyo vyote, siyo kimoja, lazima vyote vitatu.

Kumbuka, kwenye mtandao wa intaneti, jambo la kiungwana kabisa kufanya, ni kuwasaidia watu kutatua changamoto wanazopitia.

Halafu sasa unaweza kuwauzia huduma zako zaidi, kama vitabu, ushauri, semina na kadhalika.

Kama unahitaji ushauri zaidi kwenye hili, tuwasiliane sasa kwa njia ya wasap 0717396253.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.