Zingatia Mambo Haya Matatu Unapoandaa Tangazo La Chochote Unachouza.

Unapoandika au kuongea, au kutengeneza chochote ambacho kinatangaza bidhaa au huduma unayotoa, unahitaji kuwa makini sana kama unataka kupata matokeo bora.

Watu wengi wamekuwa wakifanya hilo vibaya, wakifikiri kuwaeleza watu kuhusu kile wanachouza na sifa za hicho wanachouza kunatosha kabisa. kinachowashangaza ni pale ambapo watu hawaonekani kukazana kununua, na hapo mtu kufikiria labda bidhaa au huduma wanayouza siyo sahihi.

Bidhaa au huduma inaweza kuwa sahihi kabisa na inayoweza kuwasaidia watu, ila unakuwa umeshindwa kuandika au kuandaa kitu kinachoweza kuwashawishi watu kuchukua hatua.

Ili uweze kuwashawishi watu kuchukua hatua ya kununua chochote unachouza mara moja, zingatia mambo haya matatu;

  1. Unauza nini, kinafanya nini na kwa nani.

Watu wengi huishia kusema wanachouza na sifa zake, hilo halimfanyi mtu kuchukua hatua. Unapaswa kueleza unachouza ni nini, na pia kinafanya nini. Yaani kinamsaidiaje mtu kutatua matatizo yake au kinatimiza mahitaji gani. Lazima umweleze mtu ananufaikaje kwa kununua kile ambacho unauza.

Eneo jingine muhimu ni kueleza watu wa aina gani wanaweza kunufaika na kile ambacho unauza. Hakuna kitu cha kila mtu, hivyo sema wazi unachouza kinawafaa watu gani.

SOMA;Usitangaze Biashara Yako Kwenye Blog Za Wengine, Badala Yake Fanya Hivi.

  1. Sababu za kuchukua hatua mapema.

Watu huwa hawachukui hatua mpaka kuwe na sababu ambazo zinawasukuma kweli kuchukua hatua. Kwa sababu watu hawapendi mabadiliko, wanapenda kuendelea kufanya kile ambacho wamezoea kufanya. Katika tangazo lako la kile unachouza, eleza kwa nini mtu anapaswa kuchukua hatua sasa na siyo kusubiri.

Labda kuna manufaa makubwa wanayakosa kwa kutokuwa na kile unachouza, au kuna maumivu wanayoyapata sasa kwa kuwaonesha wazi. Wakati mwingine unaweza kuwa na ofa ambayo ni ya muda mfupi, hivyo mtu asipochukua hatua kwa wakati huo, anakuwa amekosa ofa hiyo.

Kwa vyovyote vile, hakikisha mteja anayo sababu ya kununua sasa na siyo kusubiri. Kwa sababu mteja anaposubiri, huwa anasahau.

  1. Nani mwingine ameshanunua?

Watu huwa wanaogopa kununua kitu ambacho hakuna watu wengine wameshanunua. Watu huwa wanafanya maamuzi kwa kuangalia kama kuna wengine wameshafanya maamuzi kama hayo. Hivyo kwenye mpango wako unaoandaa wa kuuza, hakikisha unaweza kumwonesha mteja watu wengine mabao nao wamenunua.

Hapa ndipo unahitaji ushuhuda wa watu ambao wameshanunua kwako na wamenufaika kwa manunuzi hayo. Ushuhuda huo unawafanya wengine kuamini kwamba wanafanya maamuzi sahihi. Ushuhuda huwa unafanya kazi, hata kama anayenunua hamjui anayeshuhudia. Na haya kama umeandikwa, bado una nguvu kubwa ya kumshawishi mtu kuchukua hatua.

Zingatia mambo haya matatu katika kuandika, kuongea au kuandaa mpango wa kutangaza bidhaa au huduma yoyote unayouza. Inaweza kuwa kitabu, huduma za ushauri, semina, mafunzo na hata bidhaa nyingine za kawaida. Lengo ni kumpa mteja sababu za kununua, na kumpa uhakika kwamba manunuzi yake yatakuwa sahihi na yatamsaidia.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Leave a Reply