Tenga Muda Wa Kutosha Kutangaza Kazi Yako Ya Uandishi, Hakuna Atakayekufanyia Hilo.

Wapo watu ambao wanaandika vizuri sana, wanaandika makala ambazo wengine wakizipata zitaboresha maisha yao. Wanaandika vitabu ambavyo vina maarifa ya kumwezesha mtu kuwa na maisha bora sana.

Lakini cha kushangaza, watu hao wanaficha kazi zao hizo nzuri. Wanakaa na kazi hizo bila ya kuionesha dunia kazi hizo. Wengi wamekuwa hawapo tayari kutangaza kazi zao kwa nguvu. Wanaona aibu, na kuona labda wakitangaza kazi zao wataonekana wana tamaa.

Pia si unakumbuka usemi kwamba kizuri chajiuza na kibaya chajitembeza? Hilo linawafanya waandishi kuamini kama kazi zao ni nzuri basi watu watazijua tu, hakuna haja ya kujitangaza. Wanachosahau ni kwamba, dunia ya sasa ina kelele nyingi mno. Mtu anapotezwa na kelele hizo kabla hata hajajua kama na wewe upo.

Hivyo basi, kwa zama hizi, lazima utenge muda na hata fedha ya kujitangaza, ni lazima kama kweli unataka kazi yako iwafikie watu wengi. Na hata kama hakuna unachouza, bado unahitaji kutangaza na kusambaza kazi zako ziwafikie watu wengi zaidi.

SOMA;Kuwa Halisi, Simamia Kile Unachojua Na Kuamini Kupitia Uandishi Wako.

Hebu jiulize, kuna faida gani kutumia muda wako mwingi, kuandika makala nzuri kabisa, halafu ikaishia kusomwa na watu 10? Au 20 na hata 50? Wakati huo huo kuna watu zaidi ya 500 ambao wana shida ya kile umeandika, lakini hawajui wanaweza kupata wapi suluhisho la shida zao.

Hii ndiyo inaleta umuhimu wa kutangaza na kusambaza kazi zako. Na njia za kufanya hivyo ni rahisi kabisa. Anza kwa kutumia mitandao ya kijamii unayotumia, hakikisha unasambaza kazi zako kupitia mitandao hiyo.

Unaweza kusambaza kazi zako wewe mwenyewe, moja kwa moja kwa kutuma kwenye mitandao unayotumia. Lakini pia unaweza kuwekeza fedha kidogo na ukatangaza kupitia mitandao ya kijamii kama facebook na instagram.

Ukichagua njia ya kutangaza mwenyewe moja kwa moja, unahitaji kurudia mara nyingi kila siku. Hata kama ni makala moja, unahitaji kuisambaza zaidi ya mara kumi kwa siku moja pekee na katika masaa tofauti. Hii ni kwa sababu mitandao ya kijamii inakuwa na vitu vingi kwa wakati mmoja, kila mtu anaweka ujumbe wake. Hivyo ujumbe unaoweka wewe, unapotea haraka sana kutokana na ujumbe unaowekwa na wengine wengi.

Ndiyo maana nakuambia lazima utenge muda kwa siku wa kuhakikisha unasambaza kazi zako, kwa kurudia rudia mara nyingi.

Sambaza kazi zao kama kiungo (link), sambaza kama ujumbe mfupi, sambaza kama picha, sambaza kama video na pia sambaza kama sauti. Chochote unachoweza kufanya kuwafikia watu na wakajua kazi zako, basi kifanye.

Usione aibu kwamba watu watakuchukuliaje, wale wanaojali watafurahia sana kupata kazi zako kupitia mitandao wanayotumia.

Usiogope kwamba watu wataona unawasumbua, kama yupo atakayeona unamsumbua, huyo siyo unayemlenga. Wale unaowalenga na kuwasaidia, watajali na kuendelea kuwa na wewe.

Angalizo; tangaza kazi yako kwa nguvu ikiwa ni kazi bora, inayoweza kumsaidia mtu kuchukua hatua na kuboresha maisha yake. Usitumie nguvu kubwa kutangaza kazi mbovu, utawapoteza kabisa wale unaowalenga na kukuona wewe kama msumbufu.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

1 thought on “Tenga Muda Wa Kutosha Kutangaza Kazi Yako Ya Uandishi, Hakuna Atakayekufanyia Hilo.

  1. Pingback: Muda Wa Kuandika Upo Wa Kutosha, Ni Wewe Kusema NDIYO Na HAPANA. | MTAALAMU Network

Leave a Reply