Makundi Matatu Ya Wasomaji Wa Kazi Zako Ambayo Unapaswa Kuyajua Ili Kufanikiwa Kwenye Uandishi.

Uandishi una changamoto nyingi, na sehemu ya changamoto hizo inatokana na wasomaji wa kazi zako. Usipowajua wasomaji wako vizuri, unaweza kufanya maamuzi makubwa kuhusu uandishi wako kwa msingi ambao siyo sahihi.

Kwa mfano wapo watu wengi ambao wamekata tamaa na kuacha kuandika kwa sababu ya maoni ya wasomaji wao wachache. Wakaacha kabisa wakati kuna watu wengine walikuwa wanawafuatilia vizuri.

Wapo pia waandishi wengine ambao wamejipa vichwa kwa kuona wanakubalika sana, na kufanya maamuzi makubwa ambayo yanawagharimu sana pale wanapogundua hawakuwa wanakubalika kama walivyofikiri awali. Labda mwandishi amechapa vitabu vingi kutokana na maoni ya wasomaji wake kuwa kwamba wanataka kitabu, akishakuwa na kitabu, anashangaa mbona hakinunuliwi kama alivyofikiri.

Wapo wasomaji wa aina tatu kwa kazi zako, unapaswa kuwajua wasomaji hawa ili unapofanya maamuzi yako, uyafanye kwa usahihi.

Kundi la kwanza; wasomaji ambao wanakubaliana na wewe moja kwa moja.

Hili ni kundi la wasomaji ambao wanakukubali wewe kama wewe, hivyo kila unachoandika wanakubaliana nacho, hata kama kina makosa. Watakuelewa zaidi ya hata unavyofikiria wewe mwenyewe. Wasomaji hawa wapo tayari kuchukua hatua kwa lolote unalowafundisha au kuwashauri.

Hili ni kundi ambalo litakupa moyo sana wa wewe kuendelea kufanya kazi yako, kwa sababu utajua wapo watu wanakubaliana na wewe.

SOMA;Kuwa Halisi, Simamia Kile Unachojua Na Kuamini Kupitia Uandishi Wako.

Lakini pia hili ni kundi ambalo linaweza kukudanganya, likakupa matumaini ambayo hayapo na ukafanya maamuzi yatakayokuangusha baadaye. Lazima uwe makini na kundi hili, na ujue ni sehemu tu ya wasomaji wako, siyo wote wanakuchukulia hivyo.

Kundi la pili; wasomaji wasiokukubali kabisa.

Lipo pia kundi la wasomaji ambao hawakubaliani na wewe kabisa. Yaani hawa hawakukubali tu wewe, hivyo chochote unachoandika au kusema, hawakubaliani nacho. Labda hawakubaliani na falsafa ambayo unaisimamia au mtazamo wao ni tofauti na ule ulionao wewe.

Kundi hili linaweza kukukatisha tamaa na hata ukafikia hatua ya kuacha kabisa kuandika. Hili ni kundi unalopaswa kuwa nalo makini kwa sababu linaweza kukupelekea kukata tamaa.

Lakini pia unaweza kulitumia kujifunza, hasa pale wanapokukosoa kwa mambo ambayo unakosea kweli, kundi hili linakufanya uone wapi unakosea au wapi uboreshe zaidi.

Kundi la tatu; wasomaji wasiojali kuhusu wewe.

Hili ni kundi la wasomaji ambao hawakukubali moja kwa moja, na wala hawakukatai moja kwa moja. Hawa wapo tu, ukitoa kazi yako wanaweza kuisoma au wasiisome, wakiisoma wanaweza kuikubali au kuikataa. Hawana muda mwingi wa kufuatilia kuhusu wewe, hivyo wakikutana na wewe sawa, wasipokutana na wewe sawa.

Hili ni kundi ambalo unaweza kulitumia vizuri kuhakikisha unawafikia watu wengi zaidi. Kwa sababu utakapolifikia kundi hili vizuri, kuna ambao watakukubali na kuwa mashabiki wa ukweli, na wengine watakukosoa na kuwa wapinzani kwako.

Hivyo basi, unapoandika chochote na wakajitokeza watu kupinga, jua pia wapo ambao wamekubaliana na hicho, hata kama hawaoneshi waziwazi.

Kadhalika unapoandika kitu na watu wakakusifia sana, jua pia wapo wanaokupinga kwenye hilo, hata kama wapo kimya.

Hivyo wajibu wako ni kufanya kile muhimu, kukazana kuwa sahihi na kuboresha kila wakati. Watu watajipanga wenyewe kadiri wanavyopokea kazi zako, juhudi za kuwafanya wakukubali ni kupitia kazi unayofanya, na siyo njia nyingine.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

3 thoughts on “Makundi Matatu Ya Wasomaji Wa Kazi Zako Ambayo Unapaswa Kuyajua Ili Kufanikiwa Kwenye Uandishi.

  1. Pingback: Chini Kumejaa, Lakini Juu Zipo Nafasi Za Kutosha Sana. | MTAALAMU Network

  2. Pingback: Mambo Muhimu Ya Kuzingatia Kiuandishi Kabla Ya Kuandika Kitabu. | MTAALAMU Network

  3. Pingback: Acha Kukimbizana Na Watu Ambao Siyo Sahihi Kwa Kazi Zako. | MTAALAMU Network

Leave a Reply