Monthly Archives: August 2017

Weka Damu Yako Kwenye Kile Unachoandika, Hapo Ndipo Nguvu Ilipo.

Habari za wakati huu mwandishi mwenzangu?

Karibu kwenye jukwaa hili ambalo nimekuwa natumia kukushirikisha maarifa na mbinu sahihi za uandishi na kutengeneza kipato kwa kutumia mtandao wa intaneti.

Watu wengi ambao bado hawajaingia kwenye uandishi, au ndiyo wanaingia, wamekuwa wanaona ni changamoto kubwa sana kuweza kusikika. Hii ni kutokana na wingi wa watu wanaoandika. Na kwa vile nimekuwa nasisitiza sana kila mtu awe na blog, wapo ambao wamekuwa wananiuliza kila mtu akiwa na blog nani atasoma ya wenzake.

Hapa ndipo nimekuwa nawaambia kosa ambalo wengi wanafanya, ni kuandika kile ambacho kinaandikwa na kila mtu. Na hapo unajihakikishia hupati wasomaji kabisa, kwa sababu kama mtu anaweza kusoma kitu kimoja kwenye blogu 10, kwa nini aje na kwenye blogu yako pia?

Nimekuwa nashauri sana waandishi kujitofautisha, na kujitofautisha simaanishi tu uandike vitu vya tofauti bali uweke utofauti kwenye kile unachoandika.

Kwa msisitizo zaidi nasema weka damu yako kwenye kile unachoandika, weka utu kwenye kile unachoandika. Usiandike ili tu kuonekana umeandika, bali weka uhai kwenye kile unachoandika.

Kumbuka unamwandikia mtu ambaye ana maisha yake, ana changamoto zake na matarajio yake. Anapokuja kusoma makala yako, anahitaji kupata ile hadhi ya utu katika kusoma.

Ni muhimu sana uandike kitu ambacho kitamfanya mtu aseme ndiyo, hichi kinanihusu mimi na siyo mtu mwingine. Kitu ambacho kinampa hatua ya kuchukua ili kuweza kupata kile ambacho anataka.

SOMA;Je Unawezaje Kuandika Kuhusu Mafanikio Iwapo Wewe Hujafanikiwa?

Hii ndiyo njia ya kusimama na kuweza kujitofautisha na waandishi wengine wote. Kwa njia hii, hata kama zitakuwepo blogu nyingi zinazoandika yanayofanana na unayoandika wewe, bado watu watakuja kusoma blog yako, kwa sababu kuna kitu cha ziada wanakipata pale, kuna upekee wanaupata kwako.

Kuweza kufanikisha hili, anza na kujali. Andika kwa kujali, kumjali yule ambaye anakwenda kusoma kile unachoandika, kwa kumshirikisha vitu ambavyo vitakuwa na msaada kwake.

Kwa njia hii, lazima uwe una wasomaji ambao unawalenga. Kama unachotaka ni makala imfae kila mtu, haitamfaa yeyote na utakuwa umekazana kuwa kama waandishi wengine, kitu ambacho hakikusimamishi kwa upekee kwenye kundi la wengi wanaopiga kelele.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Hata Kama Kila Kitu Kimeshaandikwa, Dunia Bado Haijasikia Sauti Yako.

Kusudi langu kubwa kupitia mtandao wa MTAALAMU NETWORK ni kumpa kila mtu fursa ya kuweza kuifikisha sauti yake ya kipekee kwenye dunia.

Watu wengi wamekuwa wanakwama kwenye hilo kwa kuona kwamba kila wanachotaka kusema tayari kimeshasemwa. Kila wanachotaka kuandika, tayari kimeshaandikwa. Na hapo hujizuia kuchukua hatua ya kuipa dunia kile ambacho kipo ndani yao.

Hapa wanafanya makosa mawili makubwa,

Kosa la kwanza ni kuinyima dunia kile ambacho kipo ndani yao. Hakuna mtu ambaye amekuja hapa duniani kupita tu. Kwamba amekuja hapa aamke asubuhi kila siku kuwahi kazini, afanye kazi, apate mshahara au faida, atumie na maisha yajirudie tena. Kuna mambo makubwa ndani ya maisha ya kila mtu zaidi ya kufanya tu kazi ili kuendesha maisha.

Kosa la pili ni kupoteza fursa ya kutengeneza kipato kupitia upekee ambao upo ndani ya mtu. Nilishakushirikisha hili siku za nyuma, kwamba hakuna mtu yeyote anayefanana na wewe kwa kila kitu. Wewe una upekee fulani, kwa vipaji vyako, elimu yako, malezi yako, uzoefu wako, hofu zako, mapenzi yako, ukichanganya hivyo kwa pamoja, unapata kitu ambacho dunia haijawahi kupata. Hivyo ukiweza kuishirikisha dunia kitu hicho, utawasaidia wengine, na wao watakuwa tayari kukusaidia pia.

Ni katika kuwasaidia watu kuacha kufanya makosa hayo mawili nimekuwa nasema wazi wazi kabisa kila mtu anapaswa kuwa na blog. Kwa sababu blog ni njia rahisi ya kuweza kuifikisha sauti yako kwenye dunia. Kupitia blog yako unaweza kuishirikisha dunia kile unachojua, ulichozoea au hata ulichosomea. Unaweza kuwashirikisha watu safari yako ya maisha, ukawasaidia kutatua changamoto zao na hata kuwa na maisha bora.

SOMA;Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuuza Maarifa Yanayopatikana Bure Kabisa Kwenye Mtandao.

Lakini wengi wamekuwa wakijikwamisha wakifikiri wanahitaji kuwa na elimu kubwa ili kuwa na blog, au wanahitaji kutenga kiasi kikubwa cha fedha ili kuweza kuwa na blog.

Hapa ndipo nilipoamua kuanzisha mtandao huu wa MTAALAMU NETWORK, ili kuhakikisha kila mtu anaweza kuwa na blog na kuitumia vizuri kuwafikia wnegine wengi. Hivyo nimekuwa natoa huduma ya MTAALAMU BLOG, ambapo unalipia tsh 30,000/= kupata blog iliyokamilika na unayoweza kuitumia vyovyote utakavyo, na kila mwezi unalipia tsh 5,000/= kwa ajili ya kuiwezesha blog hiyo kuwa hewani na hata kupata fursa ya kuwa karibu zaidi na mimi kwa upande wa kuendesha blog yako.

Hivyo kama bado hujawa na blog, huna tena sababu ya kusubiri, kwa sababu blog nitakayokuandalia ni rahisi kutumia, kama umeweza kusoma hapa, basi utaweza kuitumia. Na huhitaji kuweka gharama kubwa, kila kitu nafanya kwa ajili yako, wewe utaweka nguvu zako kwenye kuandaa maarifa mazuri kwa watu na kuwashirikisha.

Kama unahitaji blog hii ya mtaalamu, basi niandikie ujumbe kwa njia ya wasap kwenda namba 0717 396 253, ujumbe uwe na maneno NAHITAJI MTAALAMU BLOG.

Karibu sana tufanye kazi pamoja, nikusaidie kuweza kuifikisha sauti yako kwenye dunia, usiondoke na kile kilichopo ndani yako na pia usipitwe na fursa ya kuweza kutengeneza kipato kupitia hicho unachojua sasa hivi.

Rafiki yako,

Kocha Makirita Amani.

www.mtaalamu.net

Pamoja Na Kuandika Kile Unachopenda, Angalia Pia Idadi Ya Wanaokipenda Pia.

Ushauri mkubwa ambao umekuwa unatolewa kwa wengi kuhusu kazi na biashara umekuwa ni ule kwamba ukifanya unachopenda, basi hutakuja kuwa na shida ya fedha kwenye maisha yako. Kwa kiingereza wanasema follow your passion.

Ushauri huu ni mzuri, na unafanya kazi, lakini pia una ukomo. Kuna baadhi ya hali ambazo ushauri huu haufanyi kazi, na unakuwa mzigo kwa wengi.

Inapokuja kwenye kuandika, hakuna sehemu nzuri ya kuandika kama kwenye vile vitu ambavyo tayari unavipenda. Hii inakupa wewe nafasi kubwa ya kufanikiwa, kwa sababu tayari unakuwa na msukumo mkubwa ndani yako.

Lakini hili pia lina ukomo, hasa pale ambapo unachopenda wewe hakipendwi na wengi.

Kama kile unachopenda kuandika wewe hakuna watu wengi wanaopenda kukifuatilia na kujifunza, utakuwa na wakati mgumu kukuza uandishi wako na hata kuweza kutengeneza kipato.

Kwa sababu kwa chochote unachoandika, lengo lako la baadaye ni kuweza kuwafikia watu wengi zaidi, kuwasaidia na kisha wao kuwa tayari kununua kwako.

Sasa kama watu wanaofuatilia kile unachoandika ni wachache, itakuwa changamoto kubwa kwako kukuza uandishi wako na hata kuweza kutengeneza kipato.

SOMA;Je Unawezaje Kuandika Kuhusu Mafanikio Iwapo Wewe Hujafanikiwa?

Utakazana kufanya kazi kubwa, ambayo wala haitawafikia watu wengi, hilo litakukatisha tamaa zaidi.

Hivyo kabla hujakimbilia kuandika kile unachotaka kuandikia, fanya kwanza utafiti kujua ni watu wengi kiasi gani wanafuatilia hilo. Iwapo wapo watu wanaofuatilia, kutokana na changamoto zao na hata mahitaji yao, unakuwa kwenye nafasi nzuri ya kutoa msaada na kuweza kuuza pia baadaye.

Lakini kama ni wati wachache mno ambao wanafuatilia kile unachoandika, utakwama.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Hivi Ndivyo Unavyoweza Kuuza Maarifa Yanayopatikana Bure Kabisa Kwenye Mtandao.

Sasa hivi karibu kila maarifa yanapatikana bure kabisa kwenye mtandao wa intaneti. Na hivyo watu wengi wamekuwa wakinufaika na maarifa hayo yanayopatikana bure, kuanzia vitabu, makala, video, sauti na kadhalika.

Ukiingia kwenye mtandao wa google na kutafuta kitu chochote, chini ya sekunde moja, utaletewa maelfu ya matokeo yanayoendana na kile unachotafuta.

Kwa kifupi yapo maarifa na taarifa nyingi kiasi kwamba ukitaka uzisome zote, basi itabidi uishi maisha yako yote yaliyobakia kuzisoma tu, na hapo hulipi hata senti moja.

Sasa hapa ndipo waandishi wengi, hasa wachanga hujiuliza wanawezaje kuuza maarifa wakati yanapatikana kwa wingi na bure kabisa kwenye mtandao?

Na hata unapojaribu kuuza, kuna baadhi ya wasomaji wako wanaweza kukuambia mbona unachouza tunakipata bure tu?

Hapo wengi hukata tamaa na kuona hawawezi kutengeneza kipato kwenye mtandao kwa kuuza maarifa. Lakini ukweli ni kwamba, hilo linawezekana, na wengi wanafanya hivyo.

Nimekuwa nawashauri watu wanaoniomba ushauri kuhusu kuandika vitabu, na swali langu kwao huwa ni moja, unataka kuandika kitabu, je una blog? Wengi jibu huwa ni hapana. Na huwa nawaambia kitu kimoja, anza na blog kwanza, kabla hujakimbilia kwenye kitabu.

Uandishi wa zama hizi, au biashara yoyote ya kuuza maarifa, kitu cha kwanza kinachomsukuma mtu kununua kwako, ni kama anakujua kwa muda mrefu. Kama ameshafuatilia kazi zako kwa muda mrefu na hivyo kuwa mfuasi na shabiki wako. Mtu huyu ndiye atakayekuwa wa kwanza kununua kwako, bila ya kujiuliza kama maarifa hayo yanapatikana bure mtandaoni au la.

SOMA;Kama Wewe Una Taaluma Au Uzoefu Wowote Ambao Watu Wanauhitaji, Unafanya Kosa Kubwa Sana Kama Huna Blog.

Hivyo basi, ili kuuza maarifa yanayopatikana bure mtandaoni, unahitaji kuwa na watu wanaokukubali na kukufuatilia kwa muda mrefu. Watu ambao umekuwa unawaandikia na kuwashirikisha maarifa yako kwa muda mrefu, wakanufaika nayo sana.

Watu hawa ndiyo watakaohamasika sana pale utakapowaambia, nimekuwa nakuandikia makala hizi kwa muda mrefu, umenishirikisha changamoto zako kwa muda mrefu, hapa kuna kitabu ambacho kitakusaidia sana… watanunua hata kama hujawaambia jina la kitabu. Kwa sababu wanakuamini, kwa sababu wana sababu ya kukusikiliza.

Usikimbilie kuuza kwa sababu unataka kuuza, ila tengeneza kwanza sababu ya watu kununua kwako. Sababu hii unaitengeneza kwa kuwapa watu maarifa ambayo yanawasaidia, kiasi kwamba siku ukija na maarifa unayouza, watakuwa tayari kulipia kwa sababu tayari wameshazoea kupata vitu vizuri.

Wape watu sababu ya kununua kwako, na watakuwa tayari kununua muda wowote na chochote unachouza hata kama wanaweza kukipata bure sehemu nyingine.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Chagua Tatizo Unaloweza Kuwasaidia Watu Kutatua Kupitia Maarifa Sahihi.

Jambo moja muhimu sana ambalo waandishi na wafanyabiashara wanapaswa kujua ni kwamba watu wana matatizo, tena mengi, siyo madogo. Watu wana changamoto mbalimbali ambazo zinawazuia wao kufika pale wanapotaka kufika au kuwa na maisha ambayo wanapenda kuwa nayo. Watu wana mahitaji mbalimbali ili kuwa na maisha wanayotaka.

Hili ndiyo eneo muhimu ambalo kila mtu anapaswa kuanzia, kwa kuchagua tatizo au hitaji analoweza kufanyia kazi, na kuwapa watu kile ambacho wanakitaka.

Kwenye uandishi, kitu kikubwa ambacho unakitoa ni maarifa sahihi ya mtu kuchukua ili kuondokana na tatizo alilonalo, au kupata kile ambacho anataka.

Watu wengi sana wamekwama kwa sababu hawajui wafanye nini. Huenda wameshajaribu njia kadhaa lakini hawajapata matokeo waliyokuwa wanategemea.

Cha kushangaza ni kwamba, yapo maarifa ya kuweza kutatua kila tatizo, na hata kama siyo kulitatua kabisa, basi kupunguza makali yake. Lakini watu wengi wanateseka wasijue wanawezaje kupata maarifa hayo, na hata wakiyapata wasijue wayatumieje.

Hapa ndipo wewe unapoweza kuingia na kuwasaidia watu kupata maarifa sahihi na kuweza kuyatumia kuondokana na matatizo yao au kupata kile ambacho wao wanakitaka.

Hili linakuhitaji wewe uwe mdadisi, uwe mtafiti uwe mtu wa kujifunza njia za kutatua tatizo lile, kisha kuwashirikisha watu kile ambacho kinaweza kuwasaidia. Wale wenye tatizo unalotoa maarifa ya kulitatua watakufuatilia na kukuamini, na baadaye watakuwa tayari kununua chochote unachouza.

SOMA;Njia Tano Za Kuanza Kukuza Email List Yako Kupitia Blog Na Mitandao Ya Kijamii.

Uzuri wa hili ni kwamba, unaweza kuanza na matatizo ambayo wewe mwenyewe yanakusumbua. Ukaanza kwa kutafuta maarifa sahihi ya kutatua matatizo hayo, ukayafanyia kazi, ukapata matokeo mazuri halafu ukawashirikisha watu kwa ushuhuda wako mwenyewe. Kwa njia hii utaweza kuwasaidia wengi zaidi na wakapata matokeo bora zaidi.

Angalia tatizo gani linawasumbua wengi, na ambalo unaweza kupata maarifa sahihi ya kulitatua, anza kuwashirikisha watu maarifa hayo kupitia blogu yako. Kama mpaka sasa huna blog, basi unapaswa kuwa nayo, na kama hujui unaipataje, tuwasiliane kwa wasap 0717396253.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Makundi Matatu Ya Wasomaji Wa Kazi Zako Ambayo Unapaswa Kuyajua Ili Kufanikiwa Kwenye Uandishi.

Uandishi una changamoto nyingi, na sehemu ya changamoto hizo inatokana na wasomaji wa kazi zako. Usipowajua wasomaji wako vizuri, unaweza kufanya maamuzi makubwa kuhusu uandishi wako kwa msingi ambao siyo sahihi.

Kwa mfano wapo watu wengi ambao wamekata tamaa na kuacha kuandika kwa sababu ya maoni ya wasomaji wao wachache. Wakaacha kabisa wakati kuna watu wengine walikuwa wanawafuatilia vizuri.

Wapo pia waandishi wengine ambao wamejipa vichwa kwa kuona wanakubalika sana, na kufanya maamuzi makubwa ambayo yanawagharimu sana pale wanapogundua hawakuwa wanakubalika kama walivyofikiri awali. Labda mwandishi amechapa vitabu vingi kutokana na maoni ya wasomaji wake kuwa kwamba wanataka kitabu, akishakuwa na kitabu, anashangaa mbona hakinunuliwi kama alivyofikiri.

Wapo wasomaji wa aina tatu kwa kazi zako, unapaswa kuwajua wasomaji hawa ili unapofanya maamuzi yako, uyafanye kwa usahihi.

Kundi la kwanza; wasomaji ambao wanakubaliana na wewe moja kwa moja.

Hili ni kundi la wasomaji ambao wanakukubali wewe kama wewe, hivyo kila unachoandika wanakubaliana nacho, hata kama kina makosa. Watakuelewa zaidi ya hata unavyofikiria wewe mwenyewe. Wasomaji hawa wapo tayari kuchukua hatua kwa lolote unalowafundisha au kuwashauri.

Hili ni kundi ambalo litakupa moyo sana wa wewe kuendelea kufanya kazi yako, kwa sababu utajua wapo watu wanakubaliana na wewe.

SOMA;Kuwa Halisi, Simamia Kile Unachojua Na Kuamini Kupitia Uandishi Wako.

Lakini pia hili ni kundi ambalo linaweza kukudanganya, likakupa matumaini ambayo hayapo na ukafanya maamuzi yatakayokuangusha baadaye. Lazima uwe makini na kundi hili, na ujue ni sehemu tu ya wasomaji wako, siyo wote wanakuchukulia hivyo.

Kundi la pili; wasomaji wasiokukubali kabisa.

Lipo pia kundi la wasomaji ambao hawakubaliani na wewe kabisa. Yaani hawa hawakukubali tu wewe, hivyo chochote unachoandika au kusema, hawakubaliani nacho. Labda hawakubaliani na falsafa ambayo unaisimamia au mtazamo wao ni tofauti na ule ulionao wewe.

Kundi hili linaweza kukukatisha tamaa na hata ukafikia hatua ya kuacha kabisa kuandika. Hili ni kundi unalopaswa kuwa nalo makini kwa sababu linaweza kukupelekea kukata tamaa.

Lakini pia unaweza kulitumia kujifunza, hasa pale wanapokukosoa kwa mambo ambayo unakosea kweli, kundi hili linakufanya uone wapi unakosea au wapi uboreshe zaidi.

Kundi la tatu; wasomaji wasiojali kuhusu wewe.

Hili ni kundi la wasomaji ambao hawakukubali moja kwa moja, na wala hawakukatai moja kwa moja. Hawa wapo tu, ukitoa kazi yako wanaweza kuisoma au wasiisome, wakiisoma wanaweza kuikubali au kuikataa. Hawana muda mwingi wa kufuatilia kuhusu wewe, hivyo wakikutana na wewe sawa, wasipokutana na wewe sawa.

Hili ni kundi ambalo unaweza kulitumia vizuri kuhakikisha unawafikia watu wengi zaidi. Kwa sababu utakapolifikia kundi hili vizuri, kuna ambao watakukubali na kuwa mashabiki wa ukweli, na wengine watakukosoa na kuwa wapinzani kwako.

Hivyo basi, unapoandika chochote na wakajitokeza watu kupinga, jua pia wapo ambao wamekubaliana na hicho, hata kama hawaoneshi waziwazi.

Kadhalika unapoandika kitu na watu wakakusifia sana, jua pia wapo wanaokupinga kwenye hilo, hata kama wapo kimya.

Hivyo wajibu wako ni kufanya kile muhimu, kukazana kuwa sahihi na kuboresha kila wakati. Watu watajipanga wenyewe kadiri wanavyopokea kazi zako, juhudi za kuwafanya wakukubali ni kupitia kazi unayofanya, na siyo njia nyingine.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Siri Moja Ya Kubobea Kwenye Jambo Lolote Unaloandikia.

Japokuwa hakuna cheti chochote unapaswa kuwa nacho ndiyo uruhusiwe kuandika, ukiondoa yale maeneo ya kitaalamu, watu wengi bado wamekuwa wanajizuia kuandika, kwa sababu wanaona hawana ubobezi wa kutosha kwenye kile wanachotaka kuandika.

Mimi sipendi mtu yeyote ambaye anapenda kuandika, ndani yake ana msukumo wa kuandika azuiwe na kitu chochote. Ndiyo maana kila siku kupitia mtandao huu wa MTAALAMU, nimekuwa nakupa mbinu za kukuwezesha kuvuka kila changamoto.

Kwa wale ambao wanakwama kutokana na kuona bado hawajabobea, leo nakwenda kuwapa siri moja ambayo wanaweza kuifanyia kazi popote walipo.

Iko hivi, ili uwe umebobea kwenye jambo lolote, kiasi cha wewe kuweza kuandika na kushauri wengine juu ya jambo hilo, unahitaji kujua vitu zaidi ya wengine wanavyojua. Unahitaji kujua misingi ya kitu kile, unahitaji kujua mambo yote muhimu.

Pia elewa kwa kawaida, watu hawapendi sana kusoma na kujifunza mambo kwa undani. Hivyo ina maana ukitenga muda wa kujifunza na kwenda ndani zaidi, utajua mengi zaidi ya wengine na hivyo kuwa na cha kuwashirikisha.

Zaidi ya nusu ya watu, hawasomi kitabu chochote wakamaliza kwenye maisha yao, hivyo ukisoma kitabu kimoja na ukakimaliza, utakuwa unajua vitu vingi zaidi ya nusu ya watu wanaokuzunguka.

Ukisoma vitabu viwili, utakuwa unajua vitu zaidi ya asilimia 80 ya watu wanaokuzunguka.

SOMA;Andika Hichi Pale Ambapo Huna Kabisa Kitu Cha Kuandika.

Ukisoma vitabu vitatu, utakuwa umejua vitu zaidi ya asilimia 90 ya wanaokuzunguka.

Na ukisoma vitabu vitano, utakuwa unajua vitu vingi zaidi ya asilimia 99 ya watu wanaokuzunguka.

Hivyo siri ipo hapo rafiki, soma vitabu vitano.

Eneo lolote unaloandika, ambalo kwa sasa unajiona hujawa mbobezi, chagua vitabu vitano bora kabisa ambavyo vimewahi kuandika kuhusiana na eneo hili. Soma vitabu hivyo, mwanzo mpaka mwisho.

Kupitia vitabu hivi utapata maarifa mengi, ambayo wengi hawana. Hivyo ukianza kuwashirikisha maarifa yale, watakushangaa kweli na kuona unajua vitu vingi. Kumbe ni vitu ambavyo vipo na kama wangependa kujifunza, wangeweza kuvipata pia.

Hivyo hili ni eneo zuri sana la kuanzia, kupitia kusoma vitabu vitano, utaelewa misingi ya kile unachoandika, utaelewa mambo muhimu sana yanayohusiana na kile unachoandika. Na kuanzia hapo, utajua maeneo yapi muhimu ya kuzingatia zaidi.

Nimalize kwa kusema, ukiondoa maeneo ambayo ushauri wa kitaalamu unahusika, kama afya, sheria na sayansi nyingine muhimu, unaweza kubobea kwenye jambo lolote unalopenda kuandikia kwa kusoma vitabu vitano. Chagua sasa vitabu vitano bora kabisa kuhusiana na eneo unaloandikia, visome mwanzo mwisho, utapata msingi muhimu sana utakaoweza kuutumia kuandika.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.