Category Archives: TENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO

Unachojua Wewe, Wapo Wengi Hawakijui, Washirikishe Utengeneze Kipato.

Watu wengi wanapofikiria kuanzisha blog kwa ajili ya kuandika makala na kutoa maarifa kwa wengine, huona kama bado hawajawa na maarifa au utaalamu wa kuwatosha kufanya hivyo. Wengi hufikiria utaalamu au uzoefu walionao ni mdogo na hivyo hawathubutu kuutoa kwa wengine kwa sababu labda wataonekana hawajui au kukosolewa na wanaojua.

Mimi nimekuwa nakuambia wewe rafiki yangu kitu kimoja, unachojua wewe, wapo watu wengi sana ambao hawajui na hivyo unaweza kuwafundisha kupitia blog yako na baadaye ukaweza kutengeneza kipato baadaye.

Na pia napenda kukukumbusha kwamba blog ni yako na humlazimishi mtu kusoma, hivyo usione kama kuna watu watakukosoa kwa kuandika unachojua wewe. Kama hawapendi wataacha kusoma, ila wale ambao unawasaidia, wataendelea kusoma kila unapoweka maarifa.

Na muhimu zaidi ni kwamba, blogu yako siyo kitabu cha rejea mashuleni au vyuoni kwamba lazima idhibitishwe, wewe shirikisha kile ambacho unakijua, halafu wale wenye uhitaji watakufuatilia, watakuwa wasomaji wako, mashabiki wako, na baadaye watanunua kutoka kwako.

Kama bado hujashawishika kwamba una kitu cha kuweza kuandika kwenye blog, hebu niambie kama huna chochote cha aina hii;

 1. Kama umewahi kusoma shuleni au chuoni na ukafaulu vizuri, wapo watu ambao kila siku wanakazana na hawafaulu. Unaweza kuwashirikisha mbinu zako.
 2. Kama umewahi kulea mtoto mchanga mpaka akakua na akawa na afya njema, wapo wazazi wageni kila siku wanakazana na watoto wao, hawajui wafanye nini na kwa wakati gani, watafurahia sana iwapo utatoa maarifa ya aina hiyo.
 3. Kama umewahi kuwa na afya mgogoro siku za nyuma na sasa afya yako ni imara, wapo watu ambao wanahangaika na afya ambao wangenufaika sana na maarifa unayoweza kuwapa.
 4. Kama umewahi kuwa na uzito uliopitiliza, na kuweza kuupunguza bila ya kurudi tena, wapo wengi ambao wangefurahi sana kama ungewapa maarifa hayo.
 5. Kama umewahi kuwa mwalimu ambaye unafundisha vizuri wanafunzi wako na wanafaulu, wapo walimu na wanafunzi ambao wangenufaika sana na mafunzo ambayo ungewapatia.
 6. Kama umewahi kuwa mpishi wa chakula na watu wakawa wanakusifia, wapo watu ambao wangejifunza sana kupitia uzoefu wako.
 7. Kama umewahi kuwa mchezaji wa mchezo wowote, na ukawa unaujua vizuri kiasi cha watu kuwa wanakuomba uwasaidie, unaweza kuwafikia wengi zaidi na kuwasaidia.
 8. Kama umewahi kufanya kilimo cha aina yoyote ile, na ukaweza kuvuna vizuri, wapo watu ambao watanufaika sana na maarifa utakayowashirikisha.
 9. Kama umewahi kufanya biashara ya aina yoyote ile, kwa kuanzia chini kabisa na ukaweza kuikuza, wapo watu wengi ambao wangependa kuanza biashara lakini hawajui pa kuanzia, wangefurahi sana kujifunza kutoka kwako.
 10. Kama unapenda kusoma vitabu, na unanufaika navyo, wapo watu wanapenda kusoma vitabu ila hawana muda wa kutosha, au hawajui wavisomeje. Kwa kuwashirikisha mbinu zako na yale unayojifunza, watanufaika na kuwa wasomaji wako.

Pamoja na hayo yote, kama umewahi kuanzisha chochote na ukashindwa, wapo watu ambao unaweza kuwasaidia ili nao wasishindwe, kwa kuwapa njia za kuepuka, ambazo wewe hukujua na zilikuangusha.

SOMA;Zingatia Misingi Hii Mitatu(03) Ya Kutengeneza Kipato Kwenye Mtandao Wa Intaneti.

Kwa vyovyote vile rafiki, kama unapenda kuwashauri watu, kama unapenda kuwashirikisha watu kile unachojua na kama unapenda kutengeneza kipato kupitia kile unachojua, anzisha blogu yako leo na anza kuwashirikisha watu kile unachojua, ulichosomea, ulichozoea au unachopenda kujifunza.

Chochote kile, siyo hivyo nilivyotaja hapo juu pekee, unachojua, unaweza kuwashirikisha wengine na baadaye ukaweza kutengeneza kipato. Unasubiri nini usichukue hatua leo hii? Kama bado huna blog, niandikie kwenye wasap 0717396253 nikupe maelezo mazuri ya kuwa na blog.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Kwenye mtandao usiangalie MACHO angalia VITENDO kujua watu wa kuwauzia.

Kama unaendesha blog, utakuwa unajua sehemu ya kuangalia iwapo watu wanakubali kazi zako. Sehemu hiyo ni ya takwimu yaani statistics, ambapo inaonesha watu wangapi wametembelea blog kwa siku, wamesoma makala na mengine.

Kwa lugha ya mtandao hii tunaita EYEBALLS au MACHO, yaani ni macho mangapi yameona kila ambacho umeweka au kuandika. Unapotaka kuwakaribisha watu watangaze kupitia blog yako, lazima uwape ushahidi wa macho mangapi yataona kile wanachotangaza.

Hii ni njia rahisi ya kuangalia kukubalika kwa kile unafanya, ila siyo njia halisi na ya uhakika. Kwa sababu wakati mwingine mtu anaweza kuona kichwa, kikamvutia, akafungua lakini asisome. Au mwingine akafungua, akaona ndefu akasema atasoma baadaye. Na nikudokeze jambo moja kuhusu kusoma baadaye, huwa haitokei, wanasahau, wanatingwa na mengine.

Njia bora kwako wewe kutumia siyo macho, bali vitendo. Je msomaji anachukua hatua gani baada ya kusoma? Na hapa ni muhimu umpe msomaji hatua za kuchukua, ili uweze kupima na kufuatilia.

Labda unamwambia atoe maoni, au kuuliza swali, au kuweka mawasiliano yake. Inawezekana kumwambia awashirikishe wengine au afungue makala nyingine na kusoma.

Kwa njia hizi utaweza kuona ni watu wangapi wapo pamoja na wewe kwenye kile unachofanya, wanafuatilia kazi zako kwa karibu. Na hawa ndiyo watu ambao wapo tayari kununua chochote unachouza.

SOMA;Hichi Ndiyo Kitu Kinachowavutia Watu Kwenye Mitandao Ya Kijamii, Na Jinsi Ya Kukitumia Kutengeneza Kipato.

Hii pia unapaswa kuitumia kwenye email list yako, unapowatumia wasomaji wako chochote, utaoneshwa idadi ya waliofungua, ila pia unahitaji kuwapa kitu cha kufanya, ambacho kitakuonesha ni wangapi ambao kweli wanakufuatilia kwa karibu.

Kumbuka lengo letu siyo wasomaji wa kuja na kupita, lengo letu ni kuwa na wasomaji ambao ni mashabiki wa ukweli, ambao wanakubali kile tunachofanya na wapo tayari kutuunga mkono kwa kile tunachofanya.

Nguvu zako nyingi zipeleke kutengeneza wasomaji wa aina hii.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Eneo Moja Muhimu La Kufanyia Kazi Kila Siku Ili Kutengeneza Kipato Kwenye Intaneti.

Unapotaka kutengeneza kipato kwenye intaneti, kipato cha uhakika na cha kudumu muda mrefu, kuna eneo moja muhimu ambalo unapaswa kulifanyia kazi kila siku. Eneo hili ndiyo linajenga mhimili wako wa biashara ya intaneti, ndiyo linawasukuma watu kununua kile unachouza au hata kutangaza na wewe.

Kabla hatujaangalia eneo hilo muhimu, kwanza nikukumbushe kwamba njia bora, ya uhakika na ya kudumu ya kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti ni kuuza huduma au bidhaa zako mwenyewe. Zipo njia za matangazo na hata kuuza bidhaa za wengine, lakini njia hizi hazina udhibiti wako wa moja kwa moja. Hivyo ni vigumu kumhakikishia msomaji au mfuatiliaji wako kuhusu vitu hivyo, maana hujahusika navyo wewe moja kwa moja.

Ila kama unawauzia kitu ambacho umeandaa au kutengeneza mwenyewe, maana unaweza kuwapa uhakika wa asilimia 100 kwamba kitawasaidia, na kama hawataridhika basi wanaweza kurejesha na ukawapa kilicho bora zaidi.

Na kingine muhimu, unapouza bidhaa za wengine au kutangaza, kipato kina ukomo, lakini ukiuza zako mwenyewe, kipato ni kadiri utakavyo wewe mwenyewe.

Hivyo njia yako kuu iwe kuuza bidhaa na huduma zako, japo pia unaweza kutumia njia nyingine ili kuongeza kipato chako. Lakini kuu iwe huduma na bidhaa zako mwenyewe.

Sasa katika kuuza bidhaa na huduma zako mwenyewe, lazima kwanza uwe umejijengea jukwaa, uwe na wafuatiliaji wanaokukubali, uwe na mashabiki wa ukweli elfu moja.

Njia ya kukuwezesha kufikia hilo ni moja, kuandika vizuri.

Lazima uweze kuandika vizuri, kitu ambacho kinawavutia watu kwanza, halafu kinawaelimisha au kuwapa maarifa.

SOMA;Zingatia Misingi Hii Mitatu(03) Ya Kutengeneza Kipato Kwenye Mtandao Wa Intaneti.

Wapo watu ambao wana ujumbe mzuri sana, wanajua vitu vingi sana, lakini hawawezi kuwaeleza watu wakaelewa kwa lugha rahisi na kuweza kuchukua hatua. Hichi ni kikwazo kwao na hawawezi kupiga hatua kubwa kwa kutumia maarifa waliyonayo.

Unapaswa kujifunza namna ya kuandika vizuri, na hili ni zoezi ambalo halina kuhitimu. Huwezi kufika mahali ukasema sasa nimeshakuwa mwandishi bora.

Kila siku unahitaji kulifanyia kazi hilo, kuboresha zaidi uandishi wako.

Unaweza kuboresha uandishi wako kupitia kusoma kazi za waandishi wengine, hasa kwenye vitabu vya zamani ambavyo vimeendelea kukubalika mpaka sasa. Ukisoma vitabu vya aina hiyo, utaona kuna kitu cha tofauti kwa waandishi wao, uandishi wao unawagusa watu moja kwa moja.

Jifunze kumwandikia mtu moja kwa moja. Jifunze kuandika kitu kinachobeba hisia za kujali. Jifunze kuandika kitu kinachomsukuma mtu kuchukua hatua. Na hayo yote unayafanya kwa kuwa na majaribio mengi na kufanya tafiti nyingi.

Kuandika siyo tu kuwa na wazo na kuliweka kwenye maandishi, bali ni kujumuisha vitu vingi kwenye kile unachoandika. Unajumuisha maarifa, unajumuisha hisia, unajumuisha kujali na yote haya yanamfikia mtu anaposoma.

Fanyia kazi uandishi wako kila siku, na angalia mwitikio ambao watu wanakuwa nao kwenye kazi zako mbalimbali. Hata siku moja usifike na kusema sasa najua kila kitu, hapo ndiyo utakuwa umeanza kujipoteza wewe mwenyewe.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

 

Zingatia Misingi Hii Mitatu(03) Ya Kutengeneza Kipato Kwenye Mtandao Wa Intaneti.

Kila kitu kwenye maisha kina misingi yake,

Ni wale wanaoijua misingi na kuisimamia ndiyo mara zote wanabaki salama. Wengine ambao wanaipuuza misingi kwa sababu ya vitu vinavyoonekana vya haraka, huwa wanaishia kupotea kabisa.

Nakumbuka wakati naanza safari hii ya kutengeneza kipato kupitia mtandao wa intaneti, nilikuwa sijui wapi pa kuanzia. Hivyo nilikuwa naangalia watu wanafanya nini. Au naingia google na kuandika HOW TO MAKE MONEY ONLINE, yanakuja majibu mengi, mengine hata sikuwa naelewa.

Nikawa naona watu wanatoa maelezo ya kupewa link halafu unabonyeza matangazo na unaona namna dola zinasoma kwenye akaunti yako. Nilijiunga na moja ya aina hiyo, nikabonyeza matangazo kweli, mpaka nikafikisha dola 25, ambacho kilikuwa ndiyo kiwango cha chini kulipwa. Basi nikaanza mchakato wa kutaka nilipwe changu, hapo ndipo nilipojifunza somo kubwa sana, kwamba kutengeneza fedha kwenye mtandao unahitaji misingi. Kwa kifupi sikulipwa, lakini nilipata somo, ambalo nitakwenda kukushirikisha wewe leo ili usipoteze muda wako.

Misingi ya kutengeneza kipato kwenye mtandao ipo mingi, yapo mengi ya kuzingatia, nimeyaandikia mpaka kitabu (unaweza kukisoma hapa), lakini leo nataka nikupe misingi mitatu ambayo ukiifuata, hutakuja kudanganywa na utaijenga biashara yako vizuri sana.

Msingi wa kwanza; fanya utafiti.

Unahitaji kufanya utafiti mzuri sana wa namna gani utatengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti. Nilishasoma kitabu kimeandika njia 1000 za kutengeneza kipato kwenye mtandao! Sasa hebu jiulize hapo unaanzia wapi.

Ni muhimu ufanye utafiti, kwa kuangalia kile ambacho unafanya wewe kwenye mtandao, na kuona watu wanaweza kukulipaje. Angalia njia zote ambapo unaweza kuongeza thamani kwa watu na wao wakakulipa. Na utafiti huu siyo unaufanya kwanza ndiyo unakuwa na blog, badala yake unakuwa na blog huku ukiendelea kuufanya.

Njia ambazo nimekuwa nawashauri watu waanze nazo, baada ya kuwa wamepata wasomaji kiasi kwenye blog zao ni kuandika kitabu, kuendesha semina au kozi fupi, kuwa na makala maalumu kwa waliolipia, kuwa na kundi la wasap au facebook kwa wale wanaolipia, na pia ushauri kwa wanaolipia.

Sasa kwa njia hizi, wewe unahitaji kufanya utafiti kwa wasomaji wako. Kama ni kitabu unafikiria kuandika, je ni kitabu gani? Kinachowasaidia nini? Utakiuza kwa bei kiasi gani? Lazima haya yote uyafanyie utafiti, ili unapokaa chini na kuandika kitabu, uje na kitu ambacho watu wanakihitaji, na kwa bei ambayo wanaweza kuimudu.

Unaweza kuendesha utafiti wako kwa kuwauliza wasomaji maswali, kwa kuangalia mwitikio wao na hata maswali wanayouliza na ushauri wanaoomba mara kwa mara.

Kwa mimi nimejiwekea kasheria kadogo kwamba nikiombwa ushauri na zaidi ya watu 10 kwenye kitu kimoja, basi napaswa kuandika kitabu chenye kutoa mwongozo juu ya jambo hilo. Kwa njia hii yeyote atakayeomba ushauri kwenye jambo hilo, kwanza nitamwelekeza asome kitabu, halafu ndipo tushauriane kwa kuanzia hapo. Nilichogundua wengi wanasaidiwa na kitabu na hata wanakuwa hawana maswali tena.

Utafiti ni muhimu kwenye maisha yako yote ya kibiashara kwenye intaneti. Fanya utafiti kwenye kila jambo, na hakikisha unachukua hatua ili kuboresha zaidi.

Msingi wa pili; jielimishe.

Soma vitabu, soma blog za wengine.

Nimesema mengi kwenye msingi wa kwanza, sitasema mengi hapa. Ninachokusisitiza ni hichi, soma vitabu, tena vingi kadiri uwezavyo. Naweza kusema kiwango cha chini kiwe angalau kitabu kimoja kwa wiki. Na kama huwezi kabisa, umebanwa kabisa, basi soma vitabu viwili kwa mwezi. Kama huwezi kusoma vitabu kabisa, yaani mwezi unaisha hujasoma kitabu chochote, funga bloga yako na kafanye mambo mengine yanayokufaa.

Kwa kusoma vitabu unaongeza maarifa, juu ya mambo mbalimbali. Na pia unajifunza njia bora za uandishi. Ili uwe mwandishi bora, lazima uwasome waandishi wengine. Utaona namna watu wanapangilia mawazo yako na wewe kujifunza na kuboresha zaidi.

SOMA;Kama Unataka Kutengeneza Fedha Kwenye Mtandao, Jukumu Lako Kubwa Ni Hili.

Na kama nilivyoeleza kwenye makala hii ya kupata mawazo ya kuandika, kupitia vitabu unaweza kupata mawazo mazuri ya kuandika, au hata kuchambua kitabu ulichosoma na kuwashirikisha wasomaji wako. Faida ni nyingi za kusoma vitabu.

Soma pia blog za waandishi unaowakubali na unaopenda kujifunza kwao. Hakikisha unatembelea blog zao kila siku kama wanapost kila siku. Hawa watakupa maarifa ya ziada, lakini usiyatumie kama mawazo yako ya kuandika, vinginevyo utajikuta unaiga vitu vyake na wasomaji wakuone wewe siyo halisi.

Usiache kutembelea mtandao huu wa www.mtaalamu.net/pesablog kila siku, yapo mengi ya kujifunza kuhusu kutengeneza fedha kwenye mtandao.

Msingi wa tatu; weka kazi.

Huwa haipiti siku sijapata ombi la ushauri kutoka kwa vijana, ambao wanaangalia fursa ya kutengeneza kipato kwenye mtandao kama njia ya mteremko ya kupata fedha. Huwa najichekea mwenyewe kwa sababu nashindwa kuelewa watu wanatoa wapi dhana hii.

Hadithi ya kweli, wiki hii kuna kijana alikuwa ananipigia simu mara nyingi akiniuliza kuhusu kutengeneza kipato kwenye youtube. Nikamuuliza una video ngapi umeshaweka? Akaniambia sita, nikamwambia una watu wangapi wanaziangalia, akaniambia kama 50. Nikamwambia hebu weka kazi kwanza, hebu fikisha video 100 na waangaliaji zaidi ya 1000 kwenye video halafu uje tuongee. Akaendelea kusisitiza nimpe tu mwanga, nikamwambia anipe link ya chanel yake nione video zake, kwa kweli hakuna alichokuwa anafanya. Kwa nilivyoona video zake ni kama anafika mahali, anachukua simu yake na kurekodi kitu anachoona, halafu anaweza kwenye youtube. Sikuona kitu chochote ambacho anafundisha watu au watu wananufaika, na yeye anafikiria kutengeneza kipato, bila ya kuweka kazi yoyote.

Kufupisha maelezo rafiki ni hivi, weka kazi, weka kazi tena siyo kazi ya kitoto. Nilishaeleza hili kwenye kuandika makala 100, na nimekuwa nalisisitiza mara nyingi. Andika kila siku, sambaza kazi zako kwa watu wengi. Njoo na maarifa bora zaidi, wasaidie watu kutatua matatizo yao. Na endelea kuweka juhudi, hapo ndipo unaweza kuwa na uhakika na kutengeneza kipato.

Kama unafikiria kutengeneza kipato kwenye mtandao lakini hupo tayari kuweka kazi, nakushauri uache kupoteza muda wako kwa jambo hili. Jipange na uweke kazi, au tafuta jambo jingine la kupotezea muda wako.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Hichi Ndiyo Kitu Kinachowavutia Watu Kwenye Mitandao Ya Kijamii, Na Jinsi Ya Kukitumia Kutengeneza Kipato.

Njia bora kabisa ya kuweza kuitumia vizuri mitandao ya kijamii kutengeneza kipato, ni kujifunza kwanza tabia za watu, hasa wanapokuwa kwenye mitandao hiyo. Kwa kujifunza tabia zao, unajua namna gani unaweza kuzitumia tabia hizo kutengeneza kipato.

Hivi ndivyo makampuni makubwa yanavyofanya, ila wao wanatumia kompyuta na mtandao kukufuatilia wewe. Kama umewahi kuona hili, kama kuna kitu umetafuta kwenye mtandao wa google, au kitu unafuatilia sana, utajikuta matangazo mengi unayokutana nayo kwenye intaneti yanaendana na kile unachotafuta au unachofuatilia.

Makampuni makubwa kama google na facebook, yanazo kompyuta kubwa zinazokufuatilia kwa kila unachofanya, na hivyo kukuletea matangazo yanayoendana na yale mambo unayofuatilia. Ni mfumo mzuri ila una udhaifu mmoja, haupo sahihi kwa asilimia 100, kwa sababu siyo mtu anafanya hivyo, bali mashine.

Wewe unaweza kuboresha zaidi mfumo huu na ukaweza kukuza biashara yako na kutengeneza kipato kupitia intaneti na mitandao ya kijamii. Unachopaswa kufanya ni kujua tabia za watu unaowalenga, kisha kwenda nazo vizuri.

Swali muhimu sana la kujiuliza ili kujua tabia za watu kwenye mitandao ya kijamii ni hili; je watu wanaingia kwenye mitandao ya kijamii kwa madhumuni gani? Yaani mtu anapoamka na kitu cha kwanza kukimbilia simu yake na kwenda facebook au instagram, nini kinamsukuma?

Sidhani kama yupo mtu anayeingia kwenye mtandao wa kijamii akisema ngoja nikaone ni nguo gani naweza kununua leo. Au ngoja niangalie kitabu gani cha kununua, hilo hutokea baadaye, lakini siyo msukumo wake wa kwanza. Lakini watu wanatumia nguvu nyingi kuuza vitu hivyo kila wakati kwenye mitandao hii, wakifikiri hiyo ndiyo njia bora kwao.

Kwa kufikiria kuuza tu kwenye mitandao ya kijamii ni kosa moja ambalo wengi wanafanya na linawagharimu. Ndiyo wanaweza kuuza, lakini siyo kwa kiasi kikubwa kama ambavyo wangeweza kufanya iwapo wangetumia vizuri tabia za watu.

Watu wanaingia kwenye mitandao ya kijamii kwa msukumo mkubwa wa kutaka kujua nini kinaendelea duniani. Wanataka kupata habari, taarifa, maarifa, burudani na bila kusahau, kujua wengine wanaendeleaje na maisha yao.

SOMA;Sheria Muhimu Ya Kwenye Mtandao, Kwanza Kuwa Mtu Halisi.

Kwa maana hiyo basi, kwanza kabisa, unapokuwa kwenye mitandao ya kijamii, lazima kwanza uwe mtu, ndiyo watu wakufuate wewe kama mtu, wakitaka kujua nini kinaendelea kwenye maisha yako. Baada ya hapo wape watu taarifa na maarifa muhimu sana kwenye maisha yao, yanayohusiana na kazi au biashara unayofanya, ambayo unataka kupata wateja kupitia mitandao ya kijamii. Na hapo sasa ndiyo unaweza kuwapa huduma na bidhaa zako nyingine.

Usikazane kuuza muda wote, badala yake changanya utu wako, weka burudani kidogo, toa taarifa na maarifa muhimu. Hivi ndivyo vitu vinajenga urafiki na mahusiano mazuri kwenye mitandao ya kijamii na hatimaye sasa watu wanakuamini na kuwa tayari kununua chochote unachouza.

Na ili kufanikiwa kwenye hili, ni muhimu sana uwe na blog yako ambapo utawakaribisha watu kujifunza zaidi. Wale wanaokujua na mnaokutana kwenye mitandao ya kijamii, wanaweza kutembelea blog yako na kujifunza zaidi.

Pia unahitaji kuwa na mfumo wa kukusanya taarifa na mawasiliano ya wasomaji wako ili kuwapa maarifa zaidi na hatimaye kuwapa huduma na bidhaa zako. Hapo unahitaji kuwa na email list ambapo utakusanya mawasiliano ya wasomaji wako, na kuendelea kuwatumia email zinazowapa maarifa zaidi. Kupitia email hizo pia unaweza kuwauzia kwa urahisi zaidi kuliko kuuza moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Hivi Ndivyo Unavyojizuia Kunufaika Na Mtandao Wa Intaneti.

Mtandao wa intaneti, ni fursa bora sana kwa zama zetu. Ni kitu ambacho kimempa nguvu kila mtu ya kufanya kile ambacho, miaka michache iliyopita, kilifanywa na wachache pekee, ambao walichaguliwa au walipendelewa.

Siku za nyuma ili uweze kuandika kitabu, kutengeneza kipindi cha tv au redio, kuandika makala, ilikuw ampaka ukubalike na vyombo vinavyozalisha vitu hivyo. Kama hukuchaguliwa au kukubalika basi ndiyo umekosa fursa.

Lakini sasa hivi, kama unataka kuandika kitabu ni wewe tu unajizuia, kwa sababu unaweza kukiandika mwenyewe na hata kukiuza mwenyewe kwenye mtandao wa intaneti, wala hata huhitaji kukichapa. Kama unataka kutengeneza kipindi cha tv, ni wewe tu uchukue simu yako, urekodi video yako na kuiweka kwenye mtandao. Hakuna wa kukuzuia au wa kukuambia usubiri mpaka akuchague.

Pamoja na fursa hii kubwa, bado watu wanajizuia kuchukua hatua.

Bado watu wanapenda kuandika, lakini wanasubiri, hawaandiki na wanasubiri wasijue wanachosubiri ni nini.

Bado watu wana mawazo mazuri ya kutengeneza vipindi vizuri vya tv au redio, lakini hawazalishi, wanasubiri mpaka mtu aje kuwaambia wanaweza.

Ninachotaka kukuambia leo ni hichi, wazo ulilonalo, hakuna wakati bora wa kulifanyia kazi kama sasa.

Kama ni wazo la kuandika, anza na blog, andika kile ambacho ungependa wengine wajifunze. Andika kile ambacho wewe mwenyewe unapenda kujifunza.

Una wazo la kipindi cha tv au redio? Unasubiri nini? Chukua simu yako, rekodi sauti au video yako na washirikishe watu kwenye mtandao wa intaneti. Mitandao karibu yote ya kijamii inaruhusu kuweka video, mtandao wa youtube ni mahususi kwa ajili ya video, kama unasubiri, umeamua kujichelewesha wewe mwenyewe.

SOMA;Sheria Muhimu Ya Kwenye Mtandao, Kwanza Kuwa Mtu Halisi.

Huu siyo wakati wa kusubiri rafiki, huu ni wakati wa kuinuka na kuingia kwenye mchezo. Mtandao wa intaneti umeleta usawa kwenye kila aina ya mchezo, kila aina ya biashara. Kinachokuzuia sasa, ni wewe mwenyewe, hakuna mwingine yeyote.

Unaposubiri mpaka watu wakuambie unaweza, au unaruhusiwa kufanya, ndiyo unajizuia wewe mwenyewe kunufaika. Ni vyema ukachukua hatua sasa kwa sababu unakosa mengi kwa kutochukua hatua.

Chochote ambacho unafikiria kufanya, ambacho kitawanufaisha wengine, anza kufanya sasa. Anza kwa kuandika kwenye mitandao ya kijamii, andika kwenye blog yako na rekodi sauti na video kisha weka kwenye intaneti. Endelea kuboresha kile unachofanya na baada ya kuwa utakuwa umetengeneza jukwaa utakalotumia kuwafikia wengi zaidi na hata kunufaika kwa kipato pia.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Jinsi Unavyoweza Kupata Wasomaji Wa Kudumu Kwenye Blogu Yako.

Tofauti kati ya blogu za kuhabarisha na blogu za kufundisha au kutoa maarifa, ni hatua mtu anayochukua baada ya kusoma kile kilichoandikwa.

Nikupe mifano miwili kabla hatujaendelea;

Mfano wa kwanza kwenye blogu ya habari; Huyu ni mtu aliyefanya mauaji ya kutisha.

Mfano wa pili kwenye blogu ya mafunzo; hatua tatu za kuboresha wazo lako la biashara.

Katika makala hizo mbili, kwanza itakayofunguliwa sana ni ile ya mauaji ya kutisha. Kwa sababu gani? Kwa sababu inashika eneo muhimu la watu ambalo ni hofu. Lakini sasa twende, kama wameifungua watu 1000, unafikiri wanachofanya ni nini baada ya kusoma habari hiyo? Hakuna kikubwa, watakuwa na hofu na kuendelea na maisha yao. Hawatajali hata ni nani ameandika habari hiyo. Wao wameshajua mwenye kufanya mauaji, na wanaendelea na maisha.

Kwenye habari ya pili, ya hatua tatu za kuboresha wazo lako la biashara, tuseme imefunguliwa na watu 50. Kati ya hao 50, huenda 10 wanakazana kupata wazo bora la biashara. Hawa moja kwa moja watachukua hatua, watafanyia kazi zile hatua tatu, watataka kumjua mwandishi zaidi na hivyo kusoma makala zake nyingine, na ataendelea kumfuatilia kuanzia hapo. Anaweza asimtafute wakati huo, lakini kadiri siku zinavyokwenda ataendelea kujifunza zaidi. Na iwapo mwandishi ataendelea kutoa makala zinazomsaidia, anakuwa mshabiki wake na kuwa tayari kununua chochote kutoaka kwake.

Kama ulivyoona hapo, kinachomfanya mtu kuwa msomaji wa kudumu wa blogu yako, siyo kuvutiwa na kile unachoandika, bali kitu gani anaondoka nacho cha kuweza kufanyia kazi. Hivyo ni muhimu sana unapoandika makala zako, hakikisha unampa mtu kitu cha kufanyia kazi, hakikisha kuna hatua ya yeye kuchukua ili kuweza kuboresha maisha yake zaidi.

Usiumizwe na namba, hasa mwanzoni. Maana watu wengi wamekuwa wanaangalia idadi ya wasomaji, wanavyoona ndogo wanakata tamaa na kuacha. Hata kama unao wasomaji 50, hao ni wazuri sana kuanza nao. Waandikie hao, wape hatua za kuchukua na mtaendelea kuwa pamoja.

Hivi ndivyo unavyojenga wasomaji wanaokufuatilia kupitia kazi zako. Siyo kwa kutaka kuwavutia wengi, ambao hawana wanachofanyia kazi. Bali kwa kuwavutia wachache ambao watachukua hatua na kuendelea kuwa pamoja.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Jinsi Ya Kuandika Kitabu Ndani Ya Siku 10 Na Kuweza Kukiuza Kwa Urahisi.

Kitu kimoja ambacho nimekuwa naamini ni hichi; kila mtu ni kitabu ambacho kinatembea. Maisha yako ni kitabu, ambacho watu hawajakijua kwa sababu hawawezi kuyasoma moja kwa moja.

Wewe ni wa kipekee sana hapa duniani, hakuna mtu kama wewe na wala hatakuja kutokea mtu kama wewe. Una historia, uzoefu, elimu na makuzi ambavyo ukivichanganya kwa pamoja, unapata kitu ambacho hakiwezi kupatikana kwa wengine.

Mengi ambayo unayajua yanaweza kuwasaidia wengi kama yakiwa kwenye mfumo mzuri. Na mfumo mzuri wa kuweza kuwasaidia wengine, hata kwa kidogo unachojua, ni kuandika kitabu.

Unaweza kuandika kitabu kuhusu jambo lolote ambalo ungependa wengine walijue. Au jambo lolote unalopenda kujifunza au kufuatilia. Kwa njia hii ukawawezesha wengine kujifunza ziadi.

kuandika kitabu

Muhimu zaidi, ni kupitia maandishi ndiyo unaweza kuacha alama ya kudumu hapa duniani. Yote tunayojifunza kwenye falsafa na dini sasa hivi, ni kupitia maandiko waliyofanywa na watu walioishi kipindi cha nyuma. Kama yasingekuwepo maandiko, leo tusingejua kuhusu Yesu, Mohammad, Budha, Mfalme Selemani na wengine wengi.

Hivyo ni muhimu sana wewe uandike kitabu kwenye maisha yako, hata kama hutakichapa wala kukiuza, kinaweza kuwasaidia watoto wako na vizazi vijavyo pia.

Lakini wengi wamekuwa wanashindwa kuandika vitabu vilivyopo ndani yao, kwa sababu wanaona kukaa chini na kuandika kitabu ni kazi hasa. Kwa sababu kitabu cha kawaida, chenye kurasa zaidi ya 200, kinapaswa kuwa na maneno elfu 60. Na vitabu vidogo, ambavyo vina kurasa zaidi ya 100 vinapaswa kuwa na maneno yasiyopungua elfu 20. Sasa kukaa chini na kuandika maneno elfu 20 mpaka yaishe siyo kazi ndogo.

Hapa nakupa njia ya kuandika kitabu ndani ya siku kumi na uwe umemaliza.

Nimekuwa nawakochi watu kuandika vitabu, ambao wamekuwa wanakazana lakini hawamalizi. Lakini ndani ya muda mfupi, usiozidi mwezi, wanakuwa wamekamilisha vitabu vyao.

Ili uweze kuandika kitabu ndani ya siku kumi, unahitaji kupitia hatua hizi sita;

Hatua ya kwanza; fikiria jina la kitabu.

Hapa unakaa chini na kufikiria jina ambalo utakipa kitabu chako. Unaweza kufikiria jina kulingana na kile unachoandika. Jina linapaswa liwe la kuvutia watu kutaka kusoma kitabu. Lakini pia jina lisiwe refu sana. Kwenye makala zijazo nitajadili kwa kina kuhusu njia bora ya kupata jina zuri la kitabu.

Hatua ya pili; fikiria sura kumi za kitabu chako.

Kwenye hatua ya pili, unafikiria mambo makuu kumi ambayo ungetaka mtu aondoke nayo kwenye kusoma kitabu chako. Mambo haya kumi yafanye kuwa sura za kitabu chako. Unaweza kuwa na pungufu ya hapo au zaidi ya hapo, hapa nimekuambia kumi ili twende vizuri na siku zetu kumi.

Hatua ya tatu; kwenye kila sura weka ambo mawili muhimu.

Baada ya kuwa na sura 10 za kitabu chako au idadi nyingine kama ulivyopanga wewe, unahitaji kuchagua mambo mawili muhimu unayotaka mtu aondoke nayo kwenye kila husika. Hapa pia unaweza kuwa na pungufu au zaidi, ni wewe tu utakavyo.

Hatua ya nne; kila siku andika maneno yasiyopungua elfu 2.

Baada ya kuwa na vichwa viwili kwenye kila sura, sasa unaanza kazi ya kuandika. Kila siku kamilisha kuandika sura moja na hakikisha unaandika siyo chini ya maneno elfu 2. Kwa kwenda hivi, siku 10 utakuwa umemaliza sura zako kumi.

Hatua ya tano; hitimisha kitabu chako.

Hapa unaweka maelezo ya kuhitimisha, unaweka maelezo ya utangulizi, unaweka maneno ya shukrani na hitimisho la kitabu chako.

Hatua ya sita; chapa kitabu au kisambaze kama nakala tete.

Ukishakamilisha kitabu, unaweza kukichapa kama nakala ngumu kwa kuwasiliana na wachapaji mbalimbali na kuchagua. Hapo watakusaidia kukipangilia vizuri na kutengeneza ganda la nje lenye mvuto.

Kama huna uwezo wa kukichapa kwa kuanzia, unaweza kukisambaza kama nakala tete, kwa kuwatumia watu kwenye email au mitandao kama wasap.

Hapo kuna vitu muhimu ya kuzingatia kama bei ya kitabu na njia ya kusambazao.

Kwa upande wa bei, kama utachapa utaangalia gharama za uchapaji na usambazaji kisha utaweka bei ambayo watu wanaweza kuimudu na wewe kupata faida.

Kama utasambaza kama nakala tete, utapanga bei kulingana na uwezo wa soko unalolenga na faida unayotaka kupata.

Hivyo ndivyo unavyoweza kuwa na kitabu chako ndani ya siku kumi. Kama kuandika maneno elfu 2 kwa siku ni mengi, basi andika maneno elfu 1 kila siku na itakuchukua siku 20 mpaka mwezi. Au andika maneno mia tano kila siku na ndani ya miezi miwili una kitabu chako. Vyovyote utakavyochagua, muhimu ni kuwa na ramani ya kitabu chako na kuandika kila siku.

 

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Kama Una ‘Smartphone’ Na Unalia Huna Biashara Au Kazi, Umejitakia Mwenyewe.

Robert Kiyosaki, mwandishi maarufu wa kitabu RICH DAD POOR DAD anasema kwamba, KAMA UNA SMARTPHONE NA BADO NI MASIKINI, BASI UNA TATIZO KUBWA.

Tunaishi kwenye zama bora sana kuwahi kutokea hapa duniani. Katika zama hizi, unaweza kutengeneza kipato popote ulipo na bila hata ya kuajiriwa au kufungua eneo la biashara.

Simu yako ya mkononi yenye mtandao wa intaneti, ni biashara tosha inayoweza kukutoa kwenye umasikini mpaka utajiri.

Angalia somo hili la leo ili kujifunza JINSI UNAVYOWEZA KUTENGENEZA KIPATO KWENYE MTANDAO WA INTANETI.

Kuangalia somo hili bonyeza maandishi haya kama hujaliona hapo juu.

Unaweza pia kujifunza zaidi kwa kutembelea www.mtaalamu.net hapo utajifunza kila kitu kuhusu kutengeneza fedha kwenye mtandao.

Pia nimeandika kitabu kinaitwa JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, kitabu ni softcopy (pdf) na kinatumwa kwa email.

Kupata kitabu hichi, tuma fedha tsh 10,000/= kwenye namba 0717 396 253 au 0755 953 887 kisha tuma email yako kwenye moja ya namba hizo na utatumiwa kitabu.

Karibu sana ujifunze namna ya kuigeuza simu yako kuwa ofisi yako. Usilie tena umasikini kwenye zama hizi ambazo unaweza kutembea na biashara popote pale ulipo.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK.

Makirita Amani,

Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Karibu sana kwenye MTAALAMU NETWORK uweze kutengeneza kipato kupitia mtandao wa intaneti.

Kujua huduma za blog tunazotoa BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kusoma makala zetu za mbinu na maarifa ya kutengeneza kipato kupitia mtandao wa intaneti BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Njia Kumi (10) Za Kutengeneza Fedha Kwenye Mtandao Wa Intaneti Kwa Wenye Taaluma Ya Ualimu.

Ualimu ni moja ya taaluma muhimu sana kwenye jamii yoyote. Walimu ndiyo wanaoijenga jamii kutokana na malezi wanayotoa kwa watoto ambao ni kizazi kinachokuja.

Pamoja na umuhimu huu mkubwa wa taaluma ya ualimu, maslahi yamekuwa siyo mazuri. Walimu wamekuwa ndiyo watu wa kulalamika kila siku kuhusu mishahara midogo na kutokuendana na gharama za maisha. Hapo bado hujaangalia wale ambao wamehitimu taaluma hii lakini hawakupata kazi.

Kauli za viongozi wengi zimekuwa ni kwamba kama umekosa kazi au kama kipato hakikutoshi basi jiajiri. Lakini walimu wengi wamekuwa wakilalamika kwamba wao wanawezaje kujiajiri kwa taaluma yao? Mtu atawezaje kwenda kuanzisha shule yake binafsi wakati hana kazi kabisa, au mshahara wake haumtoshi?

Njia rahisi ya kujiajiri au kujiongezea kipato iliyokuwa imezoeleka na walimu ilikuwa kutoa masomo ya ziada kwa wanafunzi maarufu kama tuition, lakini hii pia imepigwa marufuku maeneo ya shuleni.

FEDHA KWA BLOG

Hali kama hizi zinawafanya walimu wajione hawawezi kuondoka kwenye matatizo waliyopo. Lakini leo nataka kuzungumza na kila mwalimu ya kwamba ipo njia rahisi ya wewe kujiajiri, itakayokuwezesha kutengeneza kipato cha ziada, bila ya kuacha kile unachofanya sasa.

Njia hii ni kujiajiri na kutoa huduma kupitia mtandao wa intaneti.

Sasa hivi karibu kila mtu mwenye simu anatumia mtandao wa intaneti, na namba inazidi kuongezeka kila mwaka. Hivyo walimu wanaweza kutumia mtandao huu wa intaneti kuweza kutoa huduma kwa wale wenye uhitaji, na baadaye wakaweza kutengeneza kipato.

Kwenye mtandao wa intaneti, unatoa maarifa na taarifa zinazowasaidia watu kufanya maamuzi bora kabisa ya maisha yao.

Kabla ya kuangalia mwalimu anawezaje kutengeneza fedha kwenye mtandao wa intaneti, kwanza soma vitu vitatu muhimu unavyohitaji kuwa navyo ili kutengeneza fedha kwenye intaneti. Visome kwa kubonyeza maandishi haya.

Zifuatazo ni njia kumi(10) anazoweza kutumia mwalimu kutengeneza fedha kwenye mtandao wa intaneti.

 1. Kuandika makala zinazohusu elimu kwa ujumla. Hapa itakuwezesha kujijenga kama mtaalamu wa elimu na hivyo kupata fursa zaidi za kushauri na kufundisha kuhusu elimu.
 2. Kuuza vifaa vya ufundishaji ambavyo umetengeneza au kuandaa mwenyewe. Kama mwalimu unaweza kuwa na notes nzuri ulizoandaa, maswali mazuri na vitu vingine vinavyoweza kutumika kufundisha. Unaweza kuzitengeneza vizuri na kuziuza kupitia mtandao wa intaneti.
 3. Kuandika kuhusu malezi ya watoto. Moja ya vitu ambavyo walimu wanajifunza ni malezi, kitu ambacho wazazi wengi hawajajifunza. Hivyo mwalimu anaweza kuwa anatoa mafunzo ya aina hii na baadaye kuwa mshauri au kutoa mafunzo ya kulipia juu ya malezi bora ya watoto.
 4. Kupata fursa ya kufundisha watoto masomo ya ziada majumbani kwao. Kwa kuwa tuition mashuleni zimekatazwa, mwalimu anaweza kutoa masomo ya ziada kwa kuwafuata wanafunzi kule walipo. Kwa kutumia mtandao wa intaneti, mwalimu anaweza kuwafikia wateja wake wa huduma ya masomo ya ziada.
 5. Kuandaa kozi utakayoitoa kwa njia ya mtandao. Kupitia mtandao wa intaneti, mwalimu anaweza kuandaa na kutoa kozi ambayo watu watajiandikisha na kulipia. Kozi hii inaweza kuhusu mambo mbalimbali yanayoweza kuwasaidia watu.
 6. Kuandika kitabu na kukiuza kwa njia ya mtandao. Kitabu hiki unaweza kukichapa au kukiuza kama nakala tete.
 7. Kutoa ushauri na mafunzo kwa walimu waliopo vyuoni bado, namna bora ya kusoma na kufaulu mitihani, mambo muhimu ya kuzingatia wanapoanza kazi na hata namna ya kuendeleza na kukuza taaluma zao.
 8. Kuandaa mtaala unaoweza kutumiwa na watu wanaolenga kutoa mafunzo fulani. Kama mwalimu una uzoefu juu ya mitaala, unaweza kutumia uzoefu huo kusaidia wengine wanaoanza kutoa mafunzo mbalimbali.
 9. Kutumia vipaji na uwezo ulionao kutengeneza fedha kwenye mtandao. Hapa unaweza kuandika au kufundisha juu ya vitu vingine unavyojua, ulivyozoea au unavyopenda nje ya ualimu.
 10. Kutumia mtandao wa intaneti kutangaza na kukuza biashara zako nyingine ulizonazo tayari. Kama tayari umeshaanza biashara nyingine, unaweza kutumia mtandao wa intaneti kuzikuza zaidi.

Wakati wa kulalamika kwamba wewe kama mwalimu huna njia za kuongeza kipato zimepitwa na wakati. Una taaluma muhimu sana na zipo njia za bure kabisa kwako kuzitumia kuweza kutengeneza fedha kwa taaluma uliyonayo. Anza kufanyia kazi hayo niliyokushirikisha, na kama utapenda ushauri wangu wa karibu zaidi na hata kukuongoza kwenye hilo, nitafurahi sana kufanya kazi na wewe. Tuwasiliane kwa njia ya wasap namba 0717396253. Karibu sana.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK.

Makirita Amani,

Kocha wa mafanikio, Mwandishi na Mjasiriamali.

Karibu sana kwenye MTAALAMU NETWORK uweze kutengeneza kipato kupitia mtandao wa intaneti.

Kujua huduma za blog tunazotoa BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kusoma makala zetu za mbinu na maarifa ya kutengeneza kipato kupitia mtandao wa intaneti BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.