Jinsi Unavyoweza Kupata Mawazo Ya Kuandika Makala Kila Siku Kwenye Blog Yako.

Kwa mtu yeyote ambaye anataka kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti, kitu cha kwanza kabisa anachopaswa kufanya ni kuwa na blog. Blog ndiyo nyumbani kwako kwenye mtandao wa intaneti. Hapa ndipo unapoweka kila kitu kinachokuhusu wewe. Mitandao ya kijamii ni sehemu muhimu, ila haiwezi kukusaidia sana iwapo huna blog yako mwenyewe.

Kuwa na blog pekee haitoshi, kwa sababu watu hawataijua blog yako kwa sababu ipo. Bali wataijua blog yako kutokana na kazi unazoweka kwenye blog yako. Unahitaji kuwa na makala nyingi kwenye blog yako, makala zinazowasaidia watu kutatua matatizo yao na kuwapa maarifa ya kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi.

Njia ya uhakika ya kuifanya blog yako kuwa na makala nyingi, na kuwa karibu na watu ni kuandika kila siku. Unapoandika kila siku inakuwa rahisi kwako kuikuza blog, na pia makala zinakuwa mpya kila siku. Tofauti na kuandika makala nyingi siku moja kwa wiki au mwezi, ambapo muda unaweza usiwe rafiki kwako, na makala zikawa hazina utofauti mzuri.

Changamoto ya kuandika kila siku ni hii; kuna wakati mwandishi unakosa cha kuandika. Unapanga muda wa kuandika, lakini muda unapofika unaona huna cha kuandika. Unakazana kufikiria lakini ndiyo kabisa unakosa cha kuandika.

Hapa nakupa njia za kukuwezesha kupata mawazo ya kuandika kila siku, na kamwe hutakosa kitu cha kuandika.

  1. Soma sana vitabu vinavyoendana na yale mambo unayoandika.

Hakikisha kila siku kuna kitabu unachosoma kinachohusiana na mambo unayoandikia. Vitabu vipo vingi sana kama utatafuta na kutenga muda wa kusoma kila siku. Kupitia vitabu unaweza kupata mawazo ya kuandikia. Na kizuri zaidi, unaweza kuchambua kitabu unachosoma. Hivyo kitabu kimoja kinaweza kukupa makala nyingi uwezavyo.

Hivyo kama utapanga kusoma angalau kitabu kimoja kila wiki, hutakosa mawazo matatu ya kuandikia na pia kuandika makala ya uchambuzi wa kitabu hicho.

Usiniambie huna muda wa kusoma, mwandishi ambaye hasomi hajui kile anachoandika.

  1. Angalia matatizo yako binafsi, na yale unataka kujifunza.

Kila siku jiulize ni tatizo gani unalo ambalo ungependa kulitatua? Au ni kitu gani ambacho ungependa kujifunza zaidi? Tatua tatizo lako, au jifunze kile unachotaka kujifunza, kisha washirikishe wasomaji wako kwa kuwaandalia makala zinazoendana na kitu kile. Hii ni njia nzuri sana kwa sababu chochote unachotaka kujifunza, wapo wengine kama wewe ambao wanataka kujifunza pia. Wakijua unajifunza, watakuwa wafuatiliaji wako wa karibu.

  1. Angalia matatizo ya wengine.

Kwenye lile eneo unaloandikia, angalia matatizo ya wengine, angalia watu wanasumbuka na nini zaidi. Angalia makosa watu wanafanya, angalia changamoto watu wanakutana nazo. Na wewe zifanyie kazi, jifunze namna ya kutatua na washirikishe kwenye makala. Hakikisha kila changamoto watu wanaipitia unaitafutia suluhisho na kuwashirikisha wasomaji wako.

Habari njema ni kwamba, matatizo ya watu hawaishi, changamoto hazitakuja kukoma duniani, hivyo kila wakati utakuwa na mambo mengi ya kuandikia.

SOMA; Changamoto Mbili Zinazowakwamisha Waandishi Wa Makala Na Jinsi Ya Kuzishinda.

  1. Wafundishe watu kitu ambacho hawajui.

Kuna mambo mengi sana ambayo watu hawajui juu ya eneo unaloandikia. Yajue mambo hayo na wafahamishe watu. Waandishi wengi wamekuwa wanafikiri kwamba kile wanachojua wao basi kila mtu anajua. Utashangaa sana ukiwauliza watu, utagundua uelewa wao ni mdogo sana kuliko ulivyofikiri. Na wakati mwingine hata kama wanajua, taarifa nyingi walizonazo siyo sahihi. Hivyo kila wakati wape watu maarifa sahihi kwa maeneo muhimu ambayo kila mtu anapaswa kuyajua.

  1. Angalia kile ambacho kila mtu anakubaliana nacho, halafu pingana nacho.

Wakati mwingine unaweza kuamua kuwa tofauti na wengine. Mara nyingi kitu kikiwa kinashabikiwa na kukubaliwa na wengi, huwa kuna matatizo watu huwa hawayaoni. Mapenzi yao yanawapa upofu na hivyo kujikuta kwenye changamoto. Wewe kaa chini na angalia kwa kina, kisha andika makala ya kuwaonesha watu kile ambacho hawaoni.

Unapochagua hili kuwa makini, kuna watu watakupinga na hata kukuchukia, hivyo hakikisha chochote unachopinga, una udhibitisho wa kufanya hivyo. Usiandike tu kujitafutia umaarufu.

  1. Soma tafiti mbalimbali zinazohusiana na unachoandika.

Kuna tafiti nyingi huwa zinafanywa kwenye kila eneo la maisha yetu. Tafiti hizi mara nyingi huwa ni kwa sababu za kitaaluma na hivyo wanataaluma ndiyo wanazifaidi. Wananchi wa kawaida huwa hawazielewi tafiti hizo. Unaweza kutumia fursa hii kuzisoma tafiti na kujaribu kuzielezea kwa lugha ambayo mwananchi wa kawaida anaweza kuielewa.

Kwa njia hii utapata makala nzuri za kuandika na watu watanufaika na tafiti zinazofanywa kila siku.

Haya ni maeneo sita unayoweza kuyatumia kila mara na ukawa na makala za kuandika kila siku. Muhimu ni wewe kuwa na mpangilio mzuri ili kuweza kuwa na makala nzuri na zenye msaada kwa wasomaji wako.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

5 thoughts on “Jinsi Unavyoweza Kupata Mawazo Ya Kuandika Makala Kila Siku Kwenye Blog Yako.

  1. Pingback: Anza Kumwandikia Mtu Huyu Mmoja, Na Itakuwa Rahisi Kuwafikia Watu 1000. | MTAALAMU Network

  2. Pingback: Kama Unasema Huna Muda Wa Kuandika, Nihakikishie Kwanza Hufanyi Vitu Hivi Vitano, Nitakuelewa. | MTAALAMU Network

  3. Pingback: Naweza Kumsaidia Nani? Naweza Kumsaidia Nini? Njia Ya Kupata Mawazo Ya Kuandika. | MTAALAMU Network

  4. Pingback: Sema Kitu Kimoja Kwa Wakati, Kusema Mengi Kunawachanganya Watu. | MTAALAMU Network

Leave a Reply