Hichi Ndiyo Kitu Kinachowavutia Watu Kwenye Mitandao Ya Kijamii, Na Jinsi Ya Kukitumia Kutengeneza Kipato.

Njia bora kabisa ya kuweza kuitumia vizuri mitandao ya kijamii kutengeneza kipato, ni kujifunza kwanza tabia za watu, hasa wanapokuwa kwenye mitandao hiyo. Kwa kujifunza tabia zao, unajua namna gani unaweza kuzitumia tabia hizo kutengeneza kipato.

Hivi ndivyo makampuni makubwa yanavyofanya, ila wao wanatumia kompyuta na mtandao kukufuatilia wewe. Kama umewahi kuona hili, kama kuna kitu umetafuta kwenye mtandao wa google, au kitu unafuatilia sana, utajikuta matangazo mengi unayokutana nayo kwenye intaneti yanaendana na kile unachotafuta au unachofuatilia.

Makampuni makubwa kama google na facebook, yanazo kompyuta kubwa zinazokufuatilia kwa kila unachofanya, na hivyo kukuletea matangazo yanayoendana na yale mambo unayofuatilia. Ni mfumo mzuri ila una udhaifu mmoja, haupo sahihi kwa asilimia 100, kwa sababu siyo mtu anafanya hivyo, bali mashine.

Wewe unaweza kuboresha zaidi mfumo huu na ukaweza kukuza biashara yako na kutengeneza kipato kupitia intaneti na mitandao ya kijamii. Unachopaswa kufanya ni kujua tabia za watu unaowalenga, kisha kwenda nazo vizuri.

Swali muhimu sana la kujiuliza ili kujua tabia za watu kwenye mitandao ya kijamii ni hili; je watu wanaingia kwenye mitandao ya kijamii kwa madhumuni gani? Yaani mtu anapoamka na kitu cha kwanza kukimbilia simu yake na kwenda facebook au instagram, nini kinamsukuma?

Sidhani kama yupo mtu anayeingia kwenye mtandao wa kijamii akisema ngoja nikaone ni nguo gani naweza kununua leo. Au ngoja niangalie kitabu gani cha kununua, hilo hutokea baadaye, lakini siyo msukumo wake wa kwanza. Lakini watu wanatumia nguvu nyingi kuuza vitu hivyo kila wakati kwenye mitandao hii, wakifikiri hiyo ndiyo njia bora kwao.

Kwa kufikiria kuuza tu kwenye mitandao ya kijamii ni kosa moja ambalo wengi wanafanya na linawagharimu. Ndiyo wanaweza kuuza, lakini siyo kwa kiasi kikubwa kama ambavyo wangeweza kufanya iwapo wangetumia vizuri tabia za watu.

Watu wanaingia kwenye mitandao ya kijamii kwa msukumo mkubwa wa kutaka kujua nini kinaendelea duniani. Wanataka kupata habari, taarifa, maarifa, burudani na bila kusahau, kujua wengine wanaendeleaje na maisha yao.

SOMA;Sheria Muhimu Ya Kwenye Mtandao, Kwanza Kuwa Mtu Halisi.

Kwa maana hiyo basi, kwanza kabisa, unapokuwa kwenye mitandao ya kijamii, lazima kwanza uwe mtu, ndiyo watu wakufuate wewe kama mtu, wakitaka kujua nini kinaendelea kwenye maisha yako. Baada ya hapo wape watu taarifa na maarifa muhimu sana kwenye maisha yao, yanayohusiana na kazi au biashara unayofanya, ambayo unataka kupata wateja kupitia mitandao ya kijamii. Na hapo sasa ndiyo unaweza kuwapa huduma na bidhaa zako nyingine.

Usikazane kuuza muda wote, badala yake changanya utu wako, weka burudani kidogo, toa taarifa na maarifa muhimu. Hivi ndivyo vitu vinajenga urafiki na mahusiano mazuri kwenye mitandao ya kijamii na hatimaye sasa watu wanakuamini na kuwa tayari kununua chochote unachouza.

Na ili kufanikiwa kwenye hili, ni muhimu sana uwe na blog yako ambapo utawakaribisha watu kujifunza zaidi. Wale wanaokujua na mnaokutana kwenye mitandao ya kijamii, wanaweza kutembelea blog yako na kujifunza zaidi.

Pia unahitaji kuwa na mfumo wa kukusanya taarifa na mawasiliano ya wasomaji wako ili kuwapa maarifa zaidi na hatimaye kuwapa huduma na bidhaa zako. Hapo unahitaji kuwa na email list ambapo utakusanya mawasiliano ya wasomaji wako, na kuendelea kuwatumia email zinazowapa maarifa zaidi. Kupitia email hizo pia unaweza kuwauzia kwa urahisi zaidi kuliko kuuza moja kwa moja kwenye mitandao ya kijamii.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

2 thoughts on “Hichi Ndiyo Kitu Kinachowavutia Watu Kwenye Mitandao Ya Kijamii, Na Jinsi Ya Kukitumia Kutengeneza Kipato.

  1. Pingback: Kwenye Mitandao Ya Kijamii, Wewe Ndiyo Bidhaa, Hivyo Hakikisha Na Wewe Una Bidhaa Pia. | MTAALAMU Network

Leave a Reply