Anza Kumwandikia Mtu Huyu Mmoja, Na Itakuwa Rahisi Kuwafikia Watu 1000.

Nimewahi kukushirikisha kuhusu sheria ya mashabiki wa kweli 1000. Sheria ambayo inasema kuweza kutengeneza kipato cha kutosha kama msanii wa aina yoyote yule, iwe ni mwandishi, mwanamuziki au mchoraji, unahitaji kuwa na mashabiki wa ukweli 1000. Hawa siyo watembeleaji au wasomaji, bali watu ambao wanakukubali sana. Watu ambao wako tayari kulipia kila huduma unayoitoa.

Sasa 1000 ni namba kubwa, hasa kama ndiyo unaanza safari yako ya uandishi. Ni namba ambayo ukiiangalia unaweza kukata tamaa, na kuona huna nguvu au muda wa kufikisha namna hiyo.

Leo nataka nikupe njia ya kufikia namba hiyo kwa uhakika, japo siyo kwa urahisi au kwa uharaka. Lakini kwa kufuata njia hii, bila ya kukata tamaa, utaweza kuwafikia watu 1000 na zaidi.

Njia ninayokwenda kukushirikisha leo ni kumwandikia mtu mmoja pekee. Anza kwa kumwandikia mtu mmoja, ambaye unahakikisha unamwandalia kitu ambacho kitamsaidia kutatua matatizo yake, au kufanya maamuzi bora ya maisha yake.

Fikiria mtu moja ambaye amekwama mahali kwa kukosa maarifa ambayo wewe unaweza kumpatia kupitia uandishi wako wa makala. Kisha andika makala ya kumsaidia mtu huyo. Andika makala ambayo itaongea na mtu huyu moja kwa moja. Halafu mkaribishe mtu huyu muongee kwa kina zaidi. Mkaribishe aulize swali au aombe ushauri kupitia kutoa maoni au kukutumia email. Mjue zaidi angependa kujifunza nini, kisha mpatie maarifa zaidi. Kwa njia hiyo utaanza na mmoja, na wengi wa aina hiyo watakuja, kabla ya muda utajikuta unao watu 10, 100 na hata kuendelea.

Naomba unielewe vizuri hapa, sizungumzii wale wasomaji, ambao unaweza kuona ni wengi. Nazungumzia mashabiki wako, wale wasomaji ambao wanakukubali mno. Hawa ndiyo nataka uanze kuwatengeneza hapa, kwa kuanza na mmoja. Ndiyo maana nasema uandike kitu kinachoongea naye moja kwa moja, kiasi kwamba atakutafuta, kwa kutaka kujifunza zaidi au kwa kuomba ushauri.

Ndiyo maana nimekuwa nasisitiza sana, blog yako inapaswa kuwa nyumbani kwako kwenye mtandao wa intaneti. Na unapaswa kuwa na email list, ambayo utaitumia kuwa karibu zaidi na mashabiki wako wa ukweli.

SOMA;Jinsi Unavyoweza Kupata Mawazo Ya Kuandika Makala Kila Siku Kwenye Blog Yako.

Kama hujui ni mtu yupi uanze kuongea naye moja kwa moja, anza na wewe mwenyewe. Ni kitu gani ungependa kujua ili kuwa bora zaidi? Ni mahali gani umekwama na ungependa kupiga hatua zaidi? Tatua hayo yako, halafu andika makala ya kuongea na mtu aliyekwama kama ulivyokuwa umekwama wewe, ukimpa hatua za kumsaidia, na hatosita kukutafuta na kutaka kujifunza zaidi.

Kitu kimoja unachopaswa kujua ni kwamba, kila changamoto au tatizo unalopitia wewe, wapo wengine pia ambao wanalipitia. Matatizo na changamoto za watu ni zile zile, sema tu zinakuwa na sura tofauti kulingana na mazingira ambayo mtu huyo yupo. Hivyo kila changamoto unayotatua, kila hatua unayopiga, msaidie mwingine pia. Hii ni njia nzuri ya kutengeneza mashabiki wako wa ukweli, ambao mtaweza kwenda pamoja na kufanya biashara kwenye mtandao wa intaneti.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

1 thought on “Anza Kumwandikia Mtu Huyu Mmoja, Na Itakuwa Rahisi Kuwafikia Watu 1000.

  1. Pingback: Kuuza Kwa Uhaba Na Kuuza Kwa Mapenzi, Njia Bora Ya Kutumia Kupata Wanunuzi Wa Kazi Zako. | MTAALAMU Network

Leave a Reply