Jinsi Ya Kuendelea Kuwa Na Makala Zinazoenda Hewani Kila Siku Hata Kama Huna Mtandao Kila Siku.

Moja ya hitaji muhimu la kuweza kukuza blog yako kupata wasomaji wanaokuamini na kukufuatilia, ni kuwa na makala mpya kila siku. Msomaji anajijengea mazoea kwamba kila siku akija kwenye blog yako, kipo kitu kipya ambacho anajifunza. Lakini msomaji anapokuja na kukuta hakuna makala mpya, akirudi tena na hali ikawa hivyo, anaacha kuitegemea blog yako, kwa sababu hana uhakika ni wakati gani kutakuwa na makala mpya.

Pamoja na umuhimu huo wa kuwa na makala kila siku kwenye blog, maisha hayajanyooka kama mstari. Siyo kila wakati unakuwa kwenye maeneo rafiki kwako kuweza kuhakikisha makala inaenda hewani kila siku.

Wakati mwingine unaweza kuwa umesafiri eneo ambalo hakuna mtandao wa intaneti na hivyo kushindwa kupost makala, hata kama unaweza kuandika. Wakati mwingine unaweza kusafiri eneo ambalo huwezi kuandika kila siku, labda ni umeme hakuna, au mazingira hayakupi nafasi ya kuweza kuandika kila siku.

Je unafanya nini kwenye nyakati kama hizo ili kuhakikisha wasomaji wako wanaendelea kupata makala mpya kila siku?

Shukrani ziende kwenye huduma zote za blogu, iwe ni BLOGGER au WORDPRESS, kuna kitu kinaitwa SCHEDULE. Hapo unaweza kupanga makala ziende hewani muda ambao wewe mwenyewe hutakuwa hewani. Unachofanya ni kuandika makala, kuiweka kwenye blog, lakini badala ya ku PUBLISH moja kwa moja unaenda kwenye ku SCHEDULE. Hapo unachagua makala iende hewani siku gani (tarehe) ana saa ngapi. Hapo unaweza kuchagua siku, mwezi, mwaka na saa na dakika ambayo unataka makala hiyo iende hewani. Ukishakamilisha hilo, wewe unaendelea na mambo yako, hivyo muda ukifikia, makala itaenda hewani, hata kama wewe haupo hewani.

Hivyo kama unasafiri kwa wiki moja, na unaona hutaweza kuandika kipindi hicho, jipange kabla ya safari uandike makala zote za wiki, uziweke kwenye blog kwa kuschedule kwa wiki nzima. Makala zitaendelea kwenda hewani na wasomaji kuendelea kupata maarifa.

Kama unasafiri eneo ambalo halina umeme, unaweza pia kuandika makala zako kabla ya safari na kuziweka kwenye blog kwa kuschedule. Kama unasafiri kwa muda mrefu kwenye eneo ambalo halina umeme, unaweza kujipa utaratibu kwa kutafuta eneo lenye umeme kila wiki na kuandika na kupost makala zako za wiki nzima kwa kuschedule.

SOMA;Kabla Hujafikiria Kulipwa Kwenye Mtandao, Andika Kwanza Makala 100.

Iwapo kuandika na kuweka makala hizo kwa wakati mmoja ni nyingi, basi punguza idadi ya makala, lakini usiache kabisa kupost. Kama safari yako au kazi yako ni ya muda mrefu, basi unaweza kubadili, badala ya kuweka makala zinazoenda hewani kila siku, ukaweka makala zinazoenda hewani kila baada ya siku moja. Yaani leo ikienda, kesho haiendi, au unaweza kupanga makala ziende hewani jumatatu, jumatano na ijumaa. Kwa njia hii, wasomaji wako hawatakusahau kabisa.

Usikubali changamoto yoyote ikuzuie wewe kuwawekea wasomaji wako makala kila siku. Jipange kulingana na hali unayopitia na hakikisha wasomaji wako wanaendelea kupata maarifa kupitia blog yako. Umeshafanya kazi kubwa kuwapata, usikubali kuwapoteza kirahisi.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Leave a Reply