Njia Ya Uhakika Ya Kujenga Jina Lako Kwenye Mtandao; TAFUTA UTAKACHOSIMAMIA.

Moja ya matumizi mazuri ya mtandao wa intaneti na mitandao ya kijamii, ni kujenga jina lako kupitia kazi unazofanya au biashara zako. Mitandao ya kijamii ni uwakilishi wako kwa watu ambao hawajawahi kukutana na wewe. Mtu anapotembelea mitandao yako ya kijamii, au blog yako, kwa kupitia yale unayoandika, anajijengea picha wewe ni mtu wa aina gani, hata kama hajawahi kukutana na wewe.

Hii ni dhana muhimu sana tunayopaswa kuielewa na kuitumia vizuri kwenye kujijengea jina lako, kama unavyotaka liwe. Yaani vile ambavyo unataka watu wakuchukulie, unaweza kutumia mitandao ya kijamii kutengeneza hilo.

Hapa unachopaswa kufanya, ni kuchagua kitu kimoja au vichache ambavyo utavisimamia. Na ninaposema kuvisimamia namaanisha kweli unavisimamia, unaamini katika vitu hivyo kiasi kwamba huoni aibu kuitangazia dunia juu ya hilo. Chochote unachoandika kwenye mitandao hii, kinakuwa kinaendana na kile ambacho unasimamia.

Mtu anapokutana na kazi zako, kupitia mtandao wa intaneti, anajionea wazi kabisa unasimama upande gani. Kadiri msimamo wako unavyokuwa wazi, ndivyo watu wanavyoweza kukutegemea linapokuja swala linalohusiana na kile unachosimamia.

Lakini pia kusimamia kitu kunakuja na changamoto zake. Na moja ya changamoto hizo ni kukosolewa na kupingwa na wale ambao wanaamini tofauti na unachosimamia. Chochote kile utakachosimamia, hata kama kingekuwa kizuri kiasi gani, wapo watu ambao watakupinga, na kukukosoa. Na kadiri unavyokuwa na msimamo mkali, ndivyo wa kukukosoa na kukupinga wanavyozidi kuwa wengi. Hivyo jiandae kwa hilo na usitetereke.

Jua unaposimamia jambo lolote, wapo watu wanaokubaliana na wewe na wanakufuatilia, hata kama hawakuambii chochote. Hivyo usikate tamaa unapokutana na changamoto yoyote kwenye lile unalosimamia.

Huwezi kusimamia kila kitu, huwezi kukubali kila kitu. Chagua jambo moja au machache ambayo unayaamini kweli, kisha yasimamie kwa uhakika. Kila ujumbe unaotoa, uwe unaunga mkono kile ambacho unasimamia. Jiandae kwa kupingwa ila usikubali mtu akusababishe uache kile unachosimamia.

SOMA;Sheria Muhimu Ya Kwenye Mtandao, Kwanza Kuwa Mtu Halisi.

Unaposimamia kitu hasa, jina lako linahusishwa na kitu kile. Hivyo mtu anapokuwa na jambo lolote linalohusiana na kitu kile, moja kwa moja anaambiwa aje kwako. Hata wanaokupinga, watakuongezea watu kwa sababu lazima wakutumie wewe kama mfano wa watu wenye msimamo ambao wao hawakubaliani nao.

Muhimu sana; unachosimamia kiwe kitu sahihi na chenye manufaa kwako na wanaokuzunguka pia. Usisimamie kitu ambacho unakipenda lakini kina madhara kwako au kwa wengine.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Leave a Reply