Je Unawezaje Kuandika Kuhusu Mafanikio Iwapo Wewe Hujafanikiwa?

Msomaji mmoja wa blog hii ya MTAALAMU ameniuliza swali kwamba yeye anapenda sana kuandika kuhusu mafanikio, ila anawezaje kuandika kuhusu mafanikio wakati yeye mwenyewe ndiyo kwanza anaanza na hana mafanikio makubwa?

Nikagundua swali la aina hii linaweza kuwa linawakwamisha wengi wasiwe waandishi. Wengi wanataka kuandika juu ya jambo fulani, lakini wanajizuia kwa kuona hawawezi, labda hawana utaalamu wa kutosha, au maisha yao hayaendani na kile wanachotaka kuandika.

Hivyo wanaona kama watakuwa wanadanganya watu, na kudanganya siyo kuzuri.

Nakubaliana kabisa na hilo, ya kwamba kama mwandishi ambaye unataka mafanikio, hupaswi kudanganya, kwa sababu watu hawapendi kuwa wafuasi wa mtu mwongo.

Lakini kwenye kuandika kuhusu mafanikio wakati wewe bado hujafanikiwa, hupaswi kujizuia hata kidogo.

Katika uandishi wa jambo lolote, kuna sehemu tatu kuu unaweza kusimama kama mwandishi.

Sehemu ya kwanza ni kuandika kuripoti, yaani wewe unatoa taarifa na maarifa kama ambavyo umeyapokea kutoka kwa wengine. Huhitaji kuwa umefanya chochote, wewe unawaambia tu watu zile taarifa ambazo zipo.

Sehemu ya pili ni kuandika yale unayojifunza. Hapa unawashirikisha watu yale ambayo unajifunza, unakuwa ni mwanafunzi wa kitu fulani, na kila unachojifunza unawashirikisha wengine.

Sehemu ya tatu ni kuandika kutoa uzoefu. Hapa sasa unakuwa umeshafanya kitu, una uzoefu na hivyo unawashirikisha wengine umepita wapi na umewezaje kufika pale ambapo umefika.

Sehemu zote hizi tatu ni muhimu, japo wengi huangalia sehemu ya tatu pekee, ya kuandika kutoa uzoefu, hivyo wakiwa hawana uzoefu, wanaogopa kuandika.

SOMA;Njia Ya Uhakika Ya Kuondokana Na Hofu Ya Kuandika.

Hivyo basi, iwapo unataka kuandika kuhusu mafanikio, na bado unajiona hujafanikiwa, zingatia haya;

  1. Mafanikio ni dhana pana, hakuna mtu ambaye hana mafanikio, kuwa hai leo ni mafanikio. Unaweza kuwashirikisha watu kuhusu changamoto ulizowahi kupitia kwenye maisha yako na ukaweza kuzivuka. Hata kama ni changamoto ndogo, wapo wanaopambana na changamoto za aina hiyo, ambazo wakijifunza kutoka kwako itawasaidia.
  2. Anza safari ya mafanikio makubwa zaidi na washirikishe wasomaji wako kila unachojifunza kwenye safari hiyo ya mafanikio. Jifunze mbinu za mafanikio, jifunze kutoka kwa waliofanikiwa, kisha washirikishe wasomaji wako kile ambacho unajifunza.
  3. Wape watu taarifa zinazoendelea kwenye ulimwengu wa mafanikio. Labda kuna watu fulani ambao wametoka chini na kuweza kufanya makubwa, wape wasomaji wako taarifa hizo. Labda kuna tafiti fulani zimefanywa kuhusu mafanikio, washirikishe wasomaji wako. Chochote ambacho unakipata na unaona kinaweza kukusaidia wewe, basi washirikishe wasomaji wako pia.
  4. Soma vitabu vya mafanikio na wachambulie wasomaji wako. Watu wengi hawapendi kusoma vitabu au hawawezi kutenga muda wa kusoma vitabu, fanya hilo na washirikishe mambo muhimu kutoka kwenye vitabu mbalimbali vya mafanikio, na watakufuatilia kwa karibu kujifunza.

Kama ambavyo tumeona hapo, kuna mengi sana ya kuandika kuhusu mafanikio, hata kama wewe mwenyewe unajiona hujafanikiwa.

Muhimu sana ni uwe mkweli kwa watu, usijaribu kujionesha kwa namna ambayo siyo kweli, watu watakuja kujua na hawatakuamini tena.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

5 thoughts on “Je Unawezaje Kuandika Kuhusu Mafanikio Iwapo Wewe Hujafanikiwa?

  1. Pingback: Usiangalie Umepata Likes Ngapi, Angalia Umegusa Watu Wangapi. | MTAALAMU Network

  2. Pingback: Pamoja Na Kuandika Kile Unachopenda, Angalia Pia Idadi Ya Wanaokipenda Pia. | MTAALAMU Network

  3. Pingback: Weka Damu Yako Kwenye Kile Unachoandika, Hapo Ndipo Nguvu Ilipo. | MTAALAMU Network

  4. Pingback: Usiwahadae Watu Kusoma, Utawapata Wengi, Lakini Hawatakuwa Muhimu Kwako. | MTAALAMU Network

  5. Pingback: Kujitofautisha Na Wengine, Andika Na Kushauri Kile Unachofanyia Kazi Wewe Mwenyewe. | MTAALAMU Network

Leave a Reply