Sababu Tatu Za Mkwamo Ua Uandishi (Writer’s Block) Na Jinsi Ya Kuondoka Kwenye Mkwamo Huo.

Huwa inatokea kwenye uandishi kwamba unataka kuandika lakini kila ukikaa uandike, hakuna kitu kinachokuja. Unaweza kujaribu kuandika kitu kimoja, ukafuta, ukaandika kingine ukafuta na kurudia hivyo mara nyingi mno.

Yaani ni sawa na mtu anayekamua juisi ya muwa au chungwa na amefikia hatua ambayo hata akikamua kwa nguvu hakuna kinachotoka tena. Unaona kama akili imekwama na hakuna tena kinachoweza kutoka.

Hii ni hali ya kuumiza kama unategemea uandishi kama sehemu kuu ya kazi yako. Hivyo ni muhimu kujua sababu za mkwamo wa uandishi na jinsi ya kuondoka kwenye mwamo huo.

Blank notepad and pencil

Sababu zipo nyingi, lakini hapa tutaangalia sababu tatu kuu;

Moja; kuandika katika muda mbaya.

Kila mtu ana muda wake maalumu ambapo akili yake inakuwa kwenye uwezo wa hali ya juu sana. Kuna ambao muda huo ni asubuhi na mapema, wengine ni usiku wa manane.

Kama hujajua muda wako ni upi, na hivyo unaandika muda wowote unaojisikia, utateseka sana na mwamo wa uandishi. Kwa sababu utakuwa unailazimisha akili kufikiri kwa kina wakati ambapo siyo mzuri kwake.

Mbili; hofu.

Sababu nyingine inayowafanya wengi kukwama ni hofu, hapa mtu anakuwa anahofia kutoa kazi yake kwenye ulimwengu akiona labda wengine watamchukuliaje. Hofu inasababisha akili kukataa kabisa kutoa mawazo mazuri.

Sababu nyingine inayoendana na hii ni kujiona hujakamilika. Waandishi wengi hutaka wame wamekamilika kwenye kila jambo ndiyo waandikie. Sasa kwa kuwa ukamilifu ni mgumu sana kufikiwa kwa sisi binadamu, wanakwama kuandika.

Tatu; kelele na usumbufu.

Wote tunajua usumbufu wa zama hizi, siyo kelele za mashine wala watu wanaopita nje. Unaweza kuwa umejifungia kwenye chumba chako mwenyewe, lakini ukawa na usumbufu mkubwa sana, ambao unatokana na simu yako.

Akili yako inaposumbuliwa kila mara kwa simu au jumbe zinazoingia kwenye simu yako, haiwezi kutulia na kutoa mawazo mazuri. Hivyo itakuwa rahisi kwako kuacha na kuingia kwenye usumbufu unaokuzunguka.

SOMA; Tengeneza Hamasa Ya Kuandika, Na Siyo Kusubiri Mpaka Upate Hamasa.

Njia za kuondokana na mkwamo wa kiuandishi;

  1. Chagua muda maalumu kwako kuandika, muda ambao akili yako ipo kwenye uwezo wa hali ya juu. Jijue kama wewe ni mtu wa asubuhi au mtu wa usiku.
  2. Jikubali kwa vile ulivyo na andika kile ulichonacho, jua kuna wengi kitawasaidia.
  3. Kuwa eneo tulivu wakati wa kuandika, simu yako uwe umeizima au iwe mbali kabisa na wewe, isiwe kwenye hali ya kupiga kelele, kukujulisha kuna ujumbe au simu imeingia.
  4. Andika kwa mtindo huru, jiruhusu kuandika chochote, hata kama hutakichapisha, wewe andika tu.
  5. Badili mazingira yako, kama umekaa eneo moja kwa muda mrefu nenda eneo jingine.
  6. Soma kitabu ambacho hujawahi kusoma, kinachohusiana na mambo tofauti kabisa na unayojihusisha nayo wewe.
  7. Fanya mazoezi ya viungo, yanachangamsha mwili na akili pia.
  8. Sikiliza muziki unaoupenda, muziki huchangamsha akili.
  9. Orodhesha mawazo kumi kuhusu jambo lolote, uliza swali lolote kisha ipe kazi akili yako kuja na mambo kumi.
  10. Usiruhusu usumbufu pale unapokuwa kwenye mkwamo, kama kuangalia tv au kuperuzi mitandao ya kijamii, hilo linakuza tatizo zaidi na haileti matokeo mzuri.

Usikubali mkwamo wa kiuandishi uwe kikwazo kwako kuandika na kutoa kazi nzuri kwa wasomaji wako. Jijengee utaratibu mzuri wa kuandika, na wa kuwa na hamasa ili uweze kuandika kila siku.

Tumia ujuzi, utaalamu na uzoefu wako kutengeneza kipato kwenye mtandao wa intaneti kupitia MTAALAMU NETWORK. Kupata ushauri wa blog na jinsi ya kutengeneza kipato tuma ujumbe wasap namba 0717 396 253.

Makirita Amani,

Kupata blog yako ya kitaalamu na kuweza kutengeneza fedha kwenye mtandao, BONYEZA MAANDISHI HAYA.

Kupata kitabu cha JINSI YA KUTENGENEZA FEDHA KWENYE MTANDAO KWA KUTUMIA BLOG, bonyeza maandishi haya.

KUPOKEA MAKALA NA MAARIFA YA KUTENGENEZA FEDHA KWA BLOG KWENYE EMAIL YAKO BONYEZA MAANDISHI HAYA NA UJAZE FOMU.

Leave a Reply